Menu
in , , ,

Man City: £60m kwa De Bruyne

*Mtikisiko Arsenal: Szczesny, Flamini haoo
*Man U, City wampigania Ramos, Otamendi

Manchester City wanajiandaa ‘kuvunja benki’ kumnasa kiungo mshambuliaji wa Wolfsburg, Kevin de Bruyne, 24.

Mchezaji huyo ameshawaambia klabuni kwamba anataka kuondoka kwenda kucheza Etihad. Matajiri hao wa England wanaingiza dau hilo kubwa baada ya wiki jana tu kumnasa mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling kwa pauni milioni 49.

City wanaaminika kuanza na ofa ya pauni milioni 40 lakini inavyoonekana watapanda hadi pauni milioni 60 kumnasa mchezaji ambaye Chelsea waliachana naye wakisema hana kiwango, wakamuuza kwa pauni milioni 18.

Hii itavunja rekodi ya usajili wa wachezaji kwa klabu za England inayoshikiliwa na winga wa Manchester United, Angel Di Maria aliyesajiliwa kwa pauni milioni 59.7 kutoka Real Madrid mwaka jana.

Tena huenda Di Maria akawarahisishia City kumpata De Bruyne, kwani Paris Saint-Germain (PSG) wameachana na mpango wa kumsajili Mbelgiji huyo na badala yake wanamtaka Di Maria.

De Bruyne, 24, awali alitaka kubaki Wolfsburg lakini sasa anasema ana kiu ya kutwaa mataji na City na sasa anatarajiwa kupewa ofa ya mshahara wa £200,000 kwa wiki.
PSG wametoa ofa ya awali ya pauni milioni 45 kwa winga Di Maria mwenye umri wa miaka 27.

MTIKISIKO ARSENAL: SZCZESNY AONDOKA

huyooo Roma....
huyooo Roma….

Golikipa wa Arsenal, Wojciech Szczesny, 25, anaondoka klabuni hapo kujiunga na Roma kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja.

Szczesny aliruhusiwa na Arsenal kufanya mazungumzo na Roma juu ya maslahi yake, kwani tayari wanaye Petr Cech aliyesajiliwa kutoka Chelsea na David Ospina aliyempoka Szczesny namba yake katikati ya msimu uliopita.

Kusajiliwa kwa Cech kumemaanisha kwamba Szczesny anakuwa chaguo la tatu wakati anataka kupata muda zaidi wa kusakata soka katika umri wake wa miaka 25. Roma wamekuwa wakitaka kumsajili moja kwa moja lakini Arsene Wenger hataki kuachana na Mpolandi huyo.

Roma wanatarajiwa kuwalipa Arsenal pauni 250,000 za kuanzia kabla ya kuweka sawa ada kamili ya uhamisho huo.

Arsenal wameeleza kutaka kumsajili kiungo mkabaji wa Barcelona, Sergi Samper, 20, lakini mkataba wake unataka klabu inayomtaka itoe pauni milioni 8.5. Porto, Everton na Stoke wamemuuliza mchezaji huyo pia,
Wenger alijaribu kumsajili Samper 2011 alipomleta Emirates, Hector Bellerin.

Katika tukio jingine, kiungo mkongwe wa Arsenal aliyesajiliwa kama mchezaji huru, akijiunga na Arsenal kwa mara ya pili, Mathieu Flamini anatarajiwa kuondoka Emirates na kujiunga na Galatasaray nchini Uturuki.

Inasemekana kwamba Galatasaray wamewalipa Arsenal pauni milioni nne kwa ajili ya Flamini (31) na sasa ataungana na mchezaji mwenzake aliyekuwa Arsenal, Lukas Podolski.

Flamini alijiunga na Arsenal kwa mara ya pili akitoka AC Milan 2013, baada ya kuwa amefanya kazi na Wenger tangu 2004 hadi 2008 akiwa na kiwango kikubwa tofauti na sasa.

BENTEKE KAMILI LIVER, PEDRO, RAMOS BADO

Benteke.

Liverpool wamekamilisha usajili wa mshambuliaji wa kati, Christian Benteke kutoka Aston Villa kwa pauni milioni 32.5 katika jitihada za kuhakikisha wanakuwa wakali kwenye ushambuliaji, kwani Daniel Sturridge bado hana utimamu wa mwili.

Mshambuliaji wa PSG, Zlatan Ibrahimovic, 33, amesema kwamba hatima yake ipo kwa wakala wake, huku kukiwa na tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kuhamia Manchester United.

Mshambuliaji wa Barcelona asiye na namba kwenye kikosi cha kwanza, Pedro, 27, amesema angependa kujiunga na Manchester United. Kocha wake, Luis Enrique amesema anaweza kuondoka ilimradi klabu inayomhitaji itoe pauni milioni 22, ikiwa ni masharti yaliyo kwenye mkataba wake.

Real Madrid wanaendelea kumsisitiza mlinzi wake, Sergio Ramos, 29, kuachana na mipango yake ya kujiunga na Manchester United. Anatarajiwa kufanya mazungumzo na rais wa klabu, Florentino Perez.

Bosi wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema anaweza kuamua kuingia kwenye vita ya kumsajili Ramos na mchezaji wa Valencia, Nicolas Otamendi, 27 hivyo kuwavuruga jirani zao, United.

Bayern Munich wamekataa kuwauzia Manchester United mshambuliaji wao Mjerumani, Thomas Muller, 25, kwani bado wanamhitaji.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version