*Wenyeji sare, Gabon wawafyatua Burkina Faso
Wenyeji wa michuano ya 30 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Guinea ya Ikweta nusura waanze kwa ushindi, baada ya kuwa mbele kwa bao moja hadi dakika tatu kabla ya mechi kumalizika, Kongo Brazzaville waliposawazisha.
Guinea wanaochukuliwa kuwa si wazuri, walipata bao kupitia kwa mchezaji wa Middlesbrough ya England, Emilio Nsue dakika ya 16 tu, na walililinda vyema hadi dakika za mwisho mwisho walipozidiwa.
Kwenye mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Bata, washabiki walianza kufurahia ushindi lakini Kongo walijizatiti kipindi cha pili kwa mashambulizi mfululizo, ambapo mpira wa Francis N’Ganga uligonga mwambakabla ya mshambuliaji wa West Bromwich Albion, Thievy Bifouma kusawazisha dakika ya 87.
Ilikuwa mechi ya fungua dimba iliyoanza vyema, licha ya kuwapo na wasiwasi kutoka kwa baadhi ya watu juu ya utayari wa taifa hilo dogo kuandaa mashindano hayo peke yake na kwa notisi ya muda mfupi. Mwaka 2012 walikuwa wenyeji wenza na Gabon.
Taifa hilo, ambalo timu yake inajulikana kwa jina la National Thunder (Radi ya Taifa) liliandaa michuano hii kutokana na Morocco waliokuwa waandae kutaka isogezwe mbele kwa hofu ya maradhi ya Ebola yaliyozikumba nchi za Liberia na Sierra Leone, kisha wakajitoa.
Katika mechi nyingine, Gabon waliwapiga Burkina Faso kwa mabao 2-0. Burkina Faso walikuwa washindi wa pili kwenye michuano ya mwaka jana. Mabao ya washindi yalifungwa na mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang na Malick Evouna.
Burkina Faso walikuwa na mchezo mzuri, hata hivyo, huku mshambuliaji wa Chelsea aliye kwa mkopo Vitesse Arnhem, Bertrand Traore akionesha makali yake, lakini kipa wa Gabon, Didier Ovono alikuwa kizingiti kikubwa kwake.