Menu
in ,

Mambo ya Monaco yamwendea kombo Thierry Henry

Tanzania Sports

Thierry Henry akiongea na msaidizi wake Franck Passi

Thiery Henry aliletwa kuokoa jahazi la klabu ya Monaco inayocheza
katika Ligue 1 nchini Ufaransa, lakini sasa mambo yamemuiwa magumu,
na amezongwa na migogoro isiyoisha

Kipigo cha mabao 2-0 nyumbani wiki mbili zilizopita, kiliiacha Monaco
hoi ikiwa inashikilia nafasi ya 19 katika msimamo wa Ligue 1.
Kibaya zaidi, ilichabangwa na Guigamp, timu iliyo mkiani mwa
msimamo wa ligi.

Monaco inapita katika kipindi kigumu ikiwa na majeruhi wengi, huku
ikiwa hatarini kushuka daraja msimu huu.

Katika mechi 12 mfululizo zilizopita kwenye ligi, Monaco
wameshindwa mara tisa. Hii ni rekodi mbaya mno kwao, kwani
kumbukumbu zinaonyesha kuwa huko nyuma waliwahi kushindwa mechi
nyingi kama hizo wakiwa wamecheza mechi 73.

Henry, ambaye alipokelewa kwa shangwe na bashasha, hajaonekana
kuleta mabadiliko makubwa katika mechi 14 alizosimamia akiwa kocha
wao. Alianza na ushindi wa mechi tatu, lakini baada ya hapo imekuwa
balaa juu ya balaa.

Waliposhinda mechi za awali dhidi ya vibonde wenzao, Caen na
Amiens, klabu ilipata matumaini na ari kubwa. Lakini sasa hata
uchezaji wao unaendelea kukosa mvuto uwanjani.

Henry mwenyewe ameshaanza kukata tamaa. Majuzi tu, alijikuta
analuamu timu yake baada ya kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya
Lyon.

Huku akisisitiza kuwa wachezaji wake walipungukiwa na hali ya
kujiamini, alisema: “Ni vigumu kushinda bila tamaa ya ushindi. Ni
vigumu kushinda bila kujituma.”

Licha ya lawama ambazo baadhi ya mashabiki wameanza kummwagia
Henry, makamu wa rais wa klabu hiyo, Vadim Vasilyev, ambaye
amekumbwa na kashfa ya kuchikichia asilimia 10 ya faida iliyotokana
na uhamisho wa wachezaji, amemkingia kifua.

Anasema: “Klabu haikumleta Henry kwa ajili ya mafanikio ya muda
mfupi. Tulimleta kwa ajili ya malengo ya muda mrefu.”

Hata hivyo, Henry mwenyewe haonyeshi kama ana fikra za malengo ya
muda mrefu. Kushindwa kila mara kunaonekana kumkera na kumvunja
moyo.

Hata katika mahojiano na vyombo vya habari kadhaa ameanza kuonyesha
hasira, kama ilivyotokea katika mahojiano na Youri Tielemans baada
ya kuchapwa na Motpellier.

Alifoka: “Niseme mara nani? Kwa Kiingereza, Kwa Kifaransa, unataka
niseme nini zaidi?”

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimekuwa ninamkosoa mfululizo.
Haonekani mwenye hamasa wala furaha, na inaonekana kama ameambukiza
wachezaji wake hali hiyo ya sononeko.

Siku timu yake ilipodundwa na timu mpya iliyopanda daraja msimu
huu, Henry alikiri: “Wamecheza vizuri sana kama ipasavyo
unapochezea uwanja wa nyumbani. Sisi hatukuwa hata na hamasa ya
kucheza. Haikuwepo.”

Ingawa hapa Henry ni jina kubwa katika soka la hapa England, hali
ngumu kwa timu yake hiyo imemfanya naye akose heshima anayostahili
katika medani hii nchini mwake.

Katika wiki chache hizi, timu yake imekumbwa na ongezeko la
majeruhi. Hadi sasa zaidi ya wachezaji 10 mahiri wameumia. Miongoni
mwao ni kipa Danijel Subasic, beki Djibril Sidibé, mshambuliaji
Steven Jovetic, mchezaji mpya kutoka Strasbourg Jean Ahoulou, na
mshambulaji mahiri wa msimu uliopita Rony Lopes.

Kwa sababu hiyo, Henry analazimika kupanga wachezaji wachanga wasio
na uzoefu wala majina makubwa. Kwa mfano, katika mechi ya Ligi ya
Mabingwa, alilazimika kuwapanga viana wadogo Han-Noah Massengo na
Badiashile katika kikosi cha kwanza.

Yoso hawa ndio pekee waliozaliwa katika karne ya 21 miongoni mwa
wachezaji waliopangwa kuanza mechi katika kipindi cha
kwanza.

Hata mustakabali wa klabu upo shakani, maana Rybolovlev, amesema
mara kadhaa kuwa yupo tayari kuuza klabu hiyo.

Huku Henry amekuwa anasisitiza kuwa hafikirii kusajili wachezaji
wapya katika kipindi cha dirisha dogo la nyakati za baridi, walio
juu yake wamekuwa na fikra za kusajili majina makubwa kama Cesc
Fàbregas, Michy Batshuayi na Gary Cahill.

Yeye anakiri: “Kusema kweli tunacheza ili tusishuke daraja. Hakuna
kingine zaidi.”

Mwaka 2011, Monaco ilishuka daraja. Hata ilipokuwa katika ligi
daraja la pili, ilikuwa mkiani kabla ya Christmas ya msimu huo.
Ndipo Rybolovlev aliingiza mabilioni kunusuru klabu
hiyo.

Kwa hali ya sasa, mustakabali wa mmiliki na kocha wa Monaco
haueleweki, kwani licha ya jitihada za kutaka kuiuza, hata dalili
za wanunuzi kujitokeza hazionekani.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version