Menu
in ,

Mambo matatu yaliyosabisha Juventus kupindua matokeo

Tanzania Sports

Tangu mwaka 1996 Juventus hawajashinda ligi ya mabingwa barani ulaya, na wakati Jana wanaingia kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Stadium, walikuwa hawana matumaini makubwa.

Walikuwa nyuma ya magoli mawili dhidi ya timu ambayo kujilinda kwao ni kawaida sana, yani kwao kazi ya kujilinda ni kazi mama.

Timu ambayo katika mechi 5 zilizopita ilikuwa na clean sheets 5. Timu ambayo kabla ya mechi ya jana ilikuwa imefungwa goli 8 pekee.

Kwa hiyo Atletico Madrid walikuwa wanaonekana tishio kwa sababu ya ubora wao wa safu ya ulinzi kabla ya mechi hii na kizuri zaidi walikuwa na magoli 2 mkononi.

Sasa kipi kilichosababisha Juventus kupindua matokeo haya ?

1: UWEPO WA CRISTIANO RONALDO

Baada ya mechi ya jana kuisha aliongea na Sky Italia. Moja ya kauli ambayo aliisema ni kuwa Juventus walimsajili kwa kazi moja tu, kuongeza morali kwenye aina ya mechi kama hizi.

Mechi ambazo watu wengi hutazama ni ngumu kushinda, lakini ndizo mechi ambazo wachezaji hutakiwa kuamini kuwa bado wana nafasi ya kushinda.

Morali hii ilikuwa inakosekana ndani ya kikosi cha Juventus. Wamejitahidi sana kuonesha ushindani, ndani ya misimu minne iliyopita wameingia fainali Mara 2 lakini hawakufanikiwa kushinda.

Walikuwa wanakosa mwanadamu ambaye ana roho ya ushindi. Na jana alikuwepo. Alifanikiwa kuwaweka Juventus ndani ya mchezo kwa muda mrefu.

Alifanikiwa kuwafanya wachezaji wa Juventus kucheza kwa kujituma kwa kuamini kuwa wana nafasi kubwa ya kupita kwenda robo fainali, na mwisho wa siku Cristiano Ronaldo akafunga hat trick.

2: MBINU ZA KOCHA MAXIMILLIAN ALLEGRI.

Wakati anamwacha benchi Paolo Dyabala niliwaza kitu kimoja, Maxi Allegri anataka kuvunja ubunifu wa mbele na kukata mirija ya huduma kwa Cristiano Ronaldo?

Lakini baada ya mechi niliona umuhimu wa kumwacha benchi Paolo Dyabala na kuwaanzisha kwa pamoja Emre Can, Matuidi na Pjanic.

Hawa watatu walileta uwiano ndani ya Timu. Kwanza walihakikisha viungo wa Atletico Madrid wanakosa nafasi ya kupeleka mipira kwa kina Morata, ilifikia wakati Atletico Madrid wakawa wanatumia mipira mirefu ambayo haikuwa na faida.

Utatu huu ndiyo ulisababisha Atletico Madrid kutopata shot on target hata moja ndani ya dakika 60 za mchezo huu, pia utatu huu ulikuwa unafikisha mipira kwa uharaka eneo la mbele, hivo kuleta uwiano mzuri ndani ya Timu.

3: MASHABIKI WA JUVENTUS.

Huwezi kuzungumzia ushindi huu wa Juventus bila kuwataja mashabiki 40,000 waliokuwa katika uwanja wa Allianz Stadium.

Walionesha dhahiri kwanini wao ni mchezaji wa 12. Muda mwingi mwa mchezo walishiriki sana kuwapa moyo wachezaji wa Juventus kuzidi kupigania ushindi huu.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version