Kila msimu unapoanza uongozi wa Azam Fc hujiwekea malengo lakini msimu unapomalizika tathmini inaonesha kuwa wanakuwa katika mazingira yaleyale kama misimu mingine iliyopita….
AGOSTI mwaka huu 2023 Ligi Kuu Tanzania itarejea ulingoni huku timu zikiwa zimekamilisha maandalizi yake. Azam Fc ni miongoni mwa timu zilizoanza mapema maandalizi ya msimu mpya kwa kuweka kambi huko Soussie nchini Tunisia
TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu matano ambayo kocha huyo anatakiwa kuyaonesha msimu ujao.
MAKUNDI SHIRIKISHO
Azam ilimaliza nafasi ya tatu msimu ulioisha, na kupata nafasi ya kuwakilisha katika michuano ya Kimataifa. chanzo habari kimeiambia TANZANIASPORTS kuwa kocha wa Azam Yousouf Dabo na benchi lake la ufundi pamoja na mchambuzi wa mifumo ya timu pinzani Ibrahim Diop wanatakiwa kuifikisha timu hiyo katika hatua ya Makundi. Uongozi wa Azam umepania na kuweka malengo kuwa timu yao lazima itinge hatua ya Makundi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho. Kibarua hiki kinamkabili kocha Dabo ambacho hakuna kocha ambaye amewahi kuifikisha Azam Fc kwenye hatua hiyo. Msimu uliopita Azam Fc ilitolewa kwa tofauti ya bao na wapinzani wao kutoka Libya. Kwa maana hiyo hiki ni kibarua kigumu na kinatakiwa kufikiwa na kocha mpya.
KUWARIDHISHA MASTAA
Sio Siri Azam Fc imesajili majembe ya uhakika katika kikosi chao. Wachezaji wengi wa kigeni wakiongozwa na James Akiminko, Issah Ndala, Kipre Junior, Prince Dube ni miongoni mwa nyota ambao wanahitaji kitu cha ziada kuendelea kutumikia miamba hiyo. Matarajio ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu yalipotea ikiwa chini ya kocha Kali Ongala licha ya kuonesha uwezo mkubwa. Wachezaji nyota kama hao na hasa kutoka nje, wanaweza kufika mahali wakachoka ikiwa timu haiwapi kile wanachotegemea. Ushahidu unaonesha baadhi ya wachezaji huamua kuhama timu pale wanapogundua kuwa hakuna uwezekano wa wao kutwaa mataji wanahitarajia. Nyota kutoka Ivory coast, Ghana na kwingineko wanaweza kuachana na timu hiyo kwa kigezo hiki. Nyota wengi wamepita Azam bila kutwaa Kombe lolote licha ya mishahara minono bado wakishindwa kubaki hata kama waliondoka kwa sababu nyingine lakini kukosa motisha ya makombe ni mojawapo. Hivyo kocha mpya ana kibarua kigumu kuwaridhisha na kuwahakikisha mastaa wa timu hiyo juu ya uwezekano wa kuchukua makombe.
ZIMWI LA MAFANIKIO
Tangu uwepo wa kocha Stewart Hall klabu ya Azam imepita nyakati nzuri na mbaya. Nyakati nzuri ni zile za mashindano ya Kombe la Kagame, pamoja na Ligi Kuu. Tangu Azam haikawahi kufurukuta kwenye kandanda Ligi Kuu, Afrika Mashariki, kusini na Afrika kwa ujumla wake. Licha ya uwezo mkubwa wa kifedha kufanya uwekezaji mkubwa na mzuri bado Azam Fc hawajapata mafanikio makubwa ndani na nje. Hii Ina maana kocha Dabo anatakiwa kupambana na zimwi hili na kulitokomeza katika viunga vya Azam Complex.
KILA MSIMU KUANZA UPYA
Kila msimu unapoanza uongozi wa Azam Fc hujiwekea malengo lakini msimu unapomalizika tathmini inaonesha kuwa wanakuwa katika mazingira yaleyale kama misimu mingine iliyopita. Baada kuwa katika mazingira hayo wamejikuta wanabomoa timu yao na kuanza upya. Usajili wa wachezaji wa malengo ya msimu mmoja ni kitu ambacho kimezidi kuizamisga timu hiyo tangu ilipokibomoa kikosi cha dhahabu cha Aishi Manula,Erasto Nyoni,Aggrey Morris,John Bocco, Salum Abubakar na wengineo. Hilo linachangia kila msimu kuanza na msingi mpya kuunda mgongo wa timu. Hii ina maana badala ya kuongeza nguvu, timu imekuwa ikiundwa upya.
VIRAGO KWA MAKOCHA
Makocha waliofukuzwa Azam Fc wamekuwa wahanga wa malengo ambayo hayatimii. Makocha wengi wameondolewa kwa sababu za kutofikia malengo lakini uongozi umekuwa uleule ambao nao haujatimiza malengo. Kocha Yousouph Dabo na benchi wanakabiliwa na mzigo mzito wa kuonesha wao ni wakali wa mafanikio na ufundi. Wanatakiwa kuleta matunda mazuri sio kuwapa matumaini mashabiki wa Azam na viongozi wake. Ikiwa itakuwa kinyume chake bila shaka makocha hao nao watafuata nyayo za waliowatangulia kwa kutupiwa virago.