Mabingwa wa soka wa zamani nchini klabu ya Yanga inatarajia kuanza kunolewa na Kocha mpya, Cedric Kaze raia wa Burundi. Yanga wamelazimika kusaka kocha mpya baada ya kumtimua Zlatko Krmpotic kutokana na sababu za kiufundi. Licha ya ukubwa wa klabu hiyo kwa sasa imepitia vipindi tofauti vyenye taswira chanya na hasi. Baada ya kuondolewa kocha mkuu, Yanga iliendelea kuwa chini ya kocha Juma Mwambusi ambaye alishirikiana na Said Maulid kusimamia kikosi hicho katika mechi za kirafiki. Ujio wa kocha mpya una maana kubwa mashabiki wa Yanga, na yafuatayo ni mambo kumi yanayomkabilia kocha mpya.
1. Kusambaratisha ufalme wa klabu ya Simba Ligi Kuu
Hakuna jambo linalowaumiza kichwa mashabiki wa Yanga na viongozi wao kama namna ya kupata majibu sahihi kwa swali; ni vipi wanaweza kubomoa ufalme wa Simba katika Ligi kuu Tanzania Bara. Makocha waliopata kuzinoa yanga tangu msimu wa 2017/2-18 hawajafanikiwa kubomoa umwamba wa Simba. Simba ni mabingwa wa soka misimu mitatu mfululizo; 2017- 2018, 2018-2019, 2019-2020. Kwa kipindi chote hicho mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiishi kinyonge mbele ya wale wa Simba. Ni kama vile Simba wamejimilikisha LigiKuu Tanzania Bara kwani hakuna timu iliyofanikiwa kutikisa kwenye mbio za ubingwa. Kwahiyo kocha anayenoa Yanga anatakiwa kuleta ubingwa wa Ligi Kuu, nje ya hapo atakuwa kwenye nafasi finyu kuendelea kukinoa kikosi hicho.
2. Yanga kumfunga mtani kadiri wanavyojisikia
Pambano la mwisho Yanga walifungwa mabao 4-1 na Simba. Ushindi wa Simba ulikuwa ni kama bile kisasi cha kufungwa 1-0 na Yanga ambapo mfungaji alikuwa Mghana Bernard Morrison. Kipigo cha mabao 4-1 bado kinawapa wakati mgumu sana Yanga. Ni namna gani wataweza kupindua meza angalau wao washinde zaidi ya idadi hiyo. Ikumbuke Simba inayo historia ya kuifunga Yanga mabao 5 wakati ikiwa chini ya mshambuliaji mkali Emmanuel Okwi. Hiki ni kibarua kingine cha kocha mpya wa Yanga, ni lazima ahakikishe anawachapa Simba mabao ya kutosha.
3. Kuhimili presha kubwa ya Yanga
Katika ulimwengu wa soka wapo wachezaji wanaweza kutamba katika timu ndogo lakini wakashindwa kung’ara ndani ya jezi za Simba na Yanga. Ipo hivyo hivyo kwa baadhi ya makocha ambao wamekuwa wakitamba kwenye timu mbalimbali lakini wanapopewa kazi ya kuzinoa Simba au Yanga wanafeli. Presha ya timu hizo mara nyingi zimesababisha makocha hao kutupiwa virago na namna ambayo mashabiki wengi wanashindwa kuelewa kinachomtokea licha ya sifa kuwa alikuwa mahiri mahali kwingine. Kwa vile Yanga na Simba zimeweka viwango vya ushindani kwahiyo kila mmoja anatakiwa kumshinda mwenzake kudhihirisha utemi wake kwenye kandanda. Kocha anatakiwa kuhimili presha inayomkabili ili aweze kuipatia ushindi Yanga. Kocha mpya anatakiwa kuelewa Yanga wana matamanio mengi, hivyo presha hii itakuwa dhidi yake.
4. Yanga wanataka ubingwa sio kusindikiza
Kiu kubwa ya mashabiki wa Yanga na viongozi wao ni kuona klabu yao inachukua ubingwa. Ndiyo, kuna raha yake ya kuchukua ubingwa mbele ya mtani wao Simba. Kabla ya Simba kuibuka wababe misimu mitatu mfululizo kama ilivyokuwa Yanga ya Yusuf Manji, sasa wanataka kurejesha utamu wa ubingwa. Kocha mpya anatakiwa kulielewa jambo hili kuwa ujio wake Yanga ni kutakiwa kuleta ubingwa tu. Mashabiki wanaweza kumsamehe kocha wao mpya ikiwa ataifunga Simba tu, hata kama atakosa ubingwa. Kumchapa mtani na kutwaa ubingwa itakuwa bonsai ya aina yake.
5. Washambuliaji kutupia mabao
Msimamo wa wafungaji wanaoongoza Ligi Kuu hakuna jina la mshambuliaji wa Yanga. Hadi sasa kinara wa kupachika mabao ni mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ambaye amecheka na nyavu mara tano, akifuatiwa na Meddie Kagere mwenye mabao manne na Chriss Mugalu mwenye mabao matatu naye akitokea Simba. Kwahiyo ndani ya wafungaji watatu wanaongoza kwa sasa, wawili wanatoka Simba. Hili nalo linawakera mashabiki wa Yanga. Ni namna gani kocha mpya atawafanya washambuliaji wa Yanga waweze kupachika mabao ya kutosha ili ilikuwapa raha mashabiki wao? Je, mshambuliaji moya Saidi Ntibazonkiza atawapa furaha wanajangwani?
6. Soka la burudani na shangwe kila kona
Zlatko alilaumiwa kwa kuwa na mbinu mbovu za mechi na kuifanya Yanga icheze bila kuwaburudisha mashabiki wao. Mbinu za kocha aliyetimuliwa zilianzia safu ya ulinzi. Zlatko alihakikisha safu ya ulinzi ilikuwa ngumu kufungika hivyo wao kutaka kupata ushindi. Hata hivyo safu ya ushambuliaji haikupewa mbinu mbadala za kupachika mabao ya kutosha. Muundo wa kuitengeneza mabao haukuwa mzuri kwa maana ya washambuliaji kupata mbinu za kiuffundi. Hali hiyo ilisababisha timu iwe inapata ushindi mwembamba mno. Kocha mpya anakabiliwa na kibarua cha kuwapa burudani na ushindi mashabiki wa Yanga.
7. Atafanyaje kumziba mdomo Morrison?
Mashabiki wa Yanga wana hasira na winga Bernard Morrison ambaye amehamia Simba. Yanga wanaamini Morrison amehama timu yao kihuni na hakufanya adabu, hali ambayo ni kawaida kwa wale walioumizwa na jambo. Mashabiki wa Yanga wanataka kumwonesha Morrison kuwa timu yao ni kabambe na inaweza kufanya maajabu kuliko anavyodhani. Yote hayo yanategemea kocha mpya wa Yanga ambaye anatazamwa kwa jicho la ‘kumdiba mdomo’ Morrison kwa namna yoyote ile kila watakapokutana kwenye mechi za Ligi Kuu. Ni namna gani kocha mpya wa Yanga ataweza kuwafurahisha mashabiki na kuwatuliza hasira zao dhidi ya Morrison? Huo ni mtihani mwingine.
8. Kuwaridhisha mastaa kikosi cha kwanza
Yanga kuna mastaa wengi ambao wanatafuta namba katika kikosi cha kwanza. Wapo Tuisila Kisinda, Calinhos, Sarpong, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke,Fei Toto, Haruna Niyonzoma na Tonombe Mukoko kwa kuwataja wachache. Nyota karibu wote Yanga wanataka kupangwa
kikosi cha kwanza. Wote wanaamini wanao uwezo wa kupata namba kikosi cha kwanza. Je, ni namna gani kocha mpya wa Yanga atafanikiwa kuwaridhisha nyota wa klabu hiyo? Ni nani atakuwa kikosi cha kwanza na nani ataridhia kuwekwa benchi? Hilo ni jukumu la kocha mpya ambaye atatakiwa kuamua nani awe kikosi cha kwanza au pili.
9. Ni nyota wazawa au wageni watatoboa?
Iko hivi. Kuna mastaa waazawa wanaamini hawajazidiwa uwezo na wachezaji wa kigeni. Deus Kaseke aliwahi kunukuliwa na gazeti moja la michezo nchini akisema haoni mchezaji mwenye uwezo wa kumweka benchi. Kaseke alikuwa anawasilisha ujumbe kuwa kiwango chake na uwezo wake ni wa juu zaidi hivyo hakuna mchezaji wa kigeni atayesababisha kocha amtupe benchi. Sasa kocha mpya anatakiwa kuhakikisha anawapa nafasi nyota wote, lakini je ataegemea kwa mastaa wa kigeni au wazawa? Hilo nalo litaeleza mwelekeo wa kocha mpya.
10.Nani awe namba moja golini?
Jukumu lingine la kocha mpya ni kuamua nani awe kipa namba moja wa Yanga. Katika klabu hiyo wapo makipa watatu; Ramadhani Kabwili na Metacha Mnata ambao ni watanzania na Mkenya Farouk Shikalo? Ni nani anastahili kupangwa langoni? Je, kocha mpya atakuja na jibu gani katika nafasi hiyo ambayo imekuwa ikiwagawa mashabiki?