Menu
in

MALIPO :UCHAMBUZI WA MICHEZO NI WAJIBU

Baadhi ya wachambuzi wa Michezo

Toka uandishi wa habari ulipobuniwa na Warumi na Wahindi zaidi ya karne ishirini zilizopita nafasi yake katika jamii imesimama sambamba na uongozi wa serikali, maoni ya waendesha taifa na dunia. Mwanahabari wa kwanza kutajirika kutokana na kazi hii alikuwa Mmarekani Joseph Pullitzer aliyefariki mwaka 1911 akiwa milionea.

MALIPO YA KAZI ZA UANDISHI NA UCHAMBUZI WA MAKALA NI WAJIBU WA KILA MWAJIRI

Pullitzer aliyeendesha gazeti la St Louis Post- Dispatch, alikuwa wakili, mjasria mali na alisaidia maskini na walalahoi. Pullitzer anaheshimika kiasi ambacho Wamarekani wanaoipeleka jamii mbele kisanii na kiuanahabari hutunikiwa tuzo kwa heshima ya jina lake. Mfano mzuri ni mtunzi na mwana  muziki wa Rap, Kendrick Lamar aliyetunukiwa zawadi maalum ya muziki mwaka 2018.

Joseph Pullitzer anatukumbusha kuwa uanahabari ni kazi maalum, kazi ya heshima na kazi yenye weledi unaotakiwa malipo ya hali na mali. Mbali na hilo Pullitzer kama baba wa uanahabari alichangia sana kuthibitisha nguzo na aina kadhaa za uanahabari.

Nguzo hizo ni uandishi wa matukio -ikiwepo utangazaji wa habari zinavyotokea kwa redio au runinga- uanahabari wa kuchunguza, kufichua na kutafiti (kwa mfano kutafuta mauaji au siri fulani katika jumuiya bila wahusika kufahamu), uanahabari wa starehe, michezo na kuchangamsha kadamnasi, uanahabari wa kutoa maoni, unaopitia zaidi wanasafu na wataalamu waliobobea katika mada- yanayoweza kuchangia fikra za jamii na wanaoiendesha.

Nikifanya kipindi cha michezo
Nikifanya kipindi cha michezo

Tunaweza pia kuchangia uanahabari wa mitandaoni tuliouzoea miaka hii. Uanahabari huu umechangia katika habari kutangazwa haraka na kuwepo kwa wanahabari huria wasiosomea sana taaluma hii ila wanaochangia kutufahamisha baadhi ya matukio makubwa.

Sasa bila kwenda ndani sana katika historia, basi inabidi wataalamu wetu, viongozi wetu, wahusika wa vyombo vya habari na utamaduni kuelewa kuwa uanahabari si suala la kuchezea chezea. Na ndiyo maana viongozi wengi wanaposhinda kura, wanapotawala, wanapomiliki nchi,  wanapochukua madaraka hukakikisha kuwa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe mitaani na maofisini wanawekwa mifukoni.

Kama wakiwa tishio mara nyingi wanaondolewa. Mfano mzuri wa karibuni ni mwanahabari maarufu wa Saudi Arabia,  Jamal Kashoggi, aliyeuawa kwa njia za ajabau ajabu kwenye ubalozi wa Uturuki, mwaka 2018. Hadi leo mauaji yake ya utata yanazungumziwa ulimwenguni.

Kutokana na namna habari zinavyotangazwa leo, kuwepo kwa mitandao huria, vyombo mbalimbali vya kutangazia habari kama You Tube  na Facebook kunazuka dhana kuwa wanahabari ni watu wanaobangaiza.

Kwamba unaweza tu mtu kukurupuka tu ukaanza kuandika andika au kutangaza tukio lolote ili mradi una simu au kamera na mitambo mingine. Kutokana na hilo baadhi ya wahariri wanapuuza malipo au jasho la wanahabari waliobobea na watafiti wanaokaa chini wakatafuta habari, wakajenga hoja na kutoka jasho kabla ya kutoa walichokipata.

Ni muhimu kwetu sote tuelewe kuwa uanahabari ni taaluma yenye heshima na nafasi kubwa sana katika jamii. Kwamba mwanahabari anaweza kushtakiwa, anaweza kuuawa, anaweza kuumia kutokana na kazi yake. Kwamba anachokisema ni kumbukumbu muhimu sana katika jumuiya na stahili yake ya malipo ni lazima. Wala sio jambo la kuchezea chezea au kudharau.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version