Kocha wa Makombe karibu kwenye familia ya Wananchi” ni ujumbe rasmi kutoka klabu ya Yanga kumkaribisha mtaalamu huyo…
KAULI mbiu yao inasema “Daima mbele, nyuma mwiko”. Hivi ndivyo waweza kuamini juu ya mwelekeo wa Mabingwa wa soka nchini Tanzania, Yanga ambao wamemtangaza rasmi kocha wao mpya. Yanga wamemtangaza kocha mpya wakiwa na matumaini makubwa ya kupata mafanikio kama yale aliyoleta Nasreddine Nabi aliyetimka klabuni hapo mapema mwezi huu.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Yanga, Rais wa klabu hiyo Hersi Ali Said amemtangaza Miguel Angel Gamondi kuwa kocha mpya wa Mabingwa hao. Hivyo vijana wa Jangwani Young Africans watauanza msimu mpya wa 2023/2024 wakiwa na kocha mpya.
UJUMBE WA KARIBU
“Kocha wa Makombe karibu kwenye familia ya Wananchi” ni ujumbe rasmi kutoka klabu ya Yanga kumkaribisha mtaalamu huyo.
KOCHA WA MABINGWA, ANALIJUA SOKA LA AFRIKA
TANZANIASPORTS imefuatilia taarifa mbalimbali kumhusu kocha Miguel Angel Gamondi na kubaini kuwa ni miongoni mwa walimu wa kigeni wanolifahamu vema Soka la Afrika. Ingawaje kocha huyo hajawahi kufundisha mpira wa miguu timu za Afrika Mashariki lakini anaonekana kuwa na ufahamu juu ya soka Afrika.
Miguel Angel Gamondi ana uzoefu wa soka la Afrika kwa takribani miaka 20, ambapo amefundisha klabu za Wydad Casablanca (Morocco), USM Alger (Argentina), Mamelodi Sundowns(Afrika kusini), CR Belouizdad (Algeria) na Esperance de Tunis (Tunisia).
orodha ya timu alizofundisha hapo juu ni zile ambazo zimekuwa Mabingwa na miamba ya soka barani Afrika. Hakuna asiyejua ubora wa Mamelodi Sundowns, Wydad, Esperance na nyingine. Hii ina maana kocha huyo amekuwa kwenye kibarua Cha kuzinoa timu zenye presha kubwa kutoka kwa mashabiki. Ni kocha ambaye amezoea presha ya mashabiki wenye shauku ya kuona anabeba makombe.
KIVULI CHA NABI
Katika hali halisi Miguel Angel Gamondi anaingia katika klabu ya Yanga akiwa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kufunika kivuli kikubwa cha mtangulizi wake, Nasreddine Nabi.
Katika umri wa miaka 56 kocha mpya wa Yanga atakuwa na uzoefu mkubwa wa kuvaa viatu vya mtangulizi wake, lakini anapaswa kuonesha kuwa vinamtosha na anaweza kuvuka mafanikio yaliyofikiwa na Nabi. Miguel anajiunga na timu ambayo imetetea mataji yake matatu (Ligi Kuu, Ngao ya Jamii,ASFC) na kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako iliukosa ubingwa kwa tofauti ya goli moja tu. Katika mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ilikubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya USM Alger kisha wakashinda ugenini 1-0.
DAMU YA AMERIKA KUSINI
Miguel Gamondi ni raia wa Argentina, nchi ambayo inatoka Amerika ya kusini mahali penye vipaji vya soka vinavyotikisa dunia. Baadhi ya matukio kadhaa Miguel Angel Gamondi anaonekana akiwa na marehemu Diego Maradona ambaye ni gwiji wa soka duniani. Ukitaja Argentina, unalitaja Taifa kubwa Kisoka na lenye mvuto na elimu nzuri. Bila shaka Gamondi analeta utaalamu toka kwao Amerika kusini.