*Mbivu na mbichi kujulikana Ijumaa Brazil
*Hurst, Cafu, Zidane, Cannavaro kuchagua
Tunaikaribia siku kubwa ambapo Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) litapanga makundi ya timu kwenye fainali za Kombe la Dunia linalofanyika Brazil 2014.
Fifa itaweka hadharani makundi hayo Ijumaa hii, na eneo la kupangia ni Costa do Sauipe, jimbo la Bahia, Brazil ili watu wajue kipute kutakachoanza Juni 12 hadi Julai 13 mwakani kitakwendaje.
Haya ni mashindano ya 20, na ya kwanza kufanyika Brazil tangu 1950 ambapo wenyeji walipoteza mechi ya fainali kwa Uruguay.
Mwaka ujao zitashiriki timu 32.
Uchukuaji wa vipira kwa ajili ya kupanga nchi kwenye makundi tofauti utafanywa na wanasoka mahiri wa zaman. Hao ni pamoja na Mwingereza Sir Geoff Hurst aliyepiga hat-trick mwaka 1966, Mfaransa Zinedine Zidane, Mbrazili Cafu na Fabio Cannavaro wa Italia.
Itakuwa hafla kubwa itakayojawa burudani kutoka kwa waigizaji wa Brazil, Fernanda Lima na Rodrigo Hilbert watakuwa wakuu wa sakafu.
Kwa upande mwingine, waimbaji Margareth Menezes, Olodum na Emicida wakiwa kwenye shoo ya ufunguzi iliyopangwa kuonesha uzuri wa asili wa taifa hilo mwenyeji la Amerika.
Nchi hizo zimewekwa tayari kwenye mafungu mbalimbali ili kuhakikisha baadhi hazikutani zenyewe, kundi la kwanza likiwa ni nchi nane bora zaidi kisoka.
Hizo zipo kwenye chungu cha kwanzo nazo ni Brazil, Hispania, Argentina, Ubelgiji, Colombia, Ujerumani, Uswisi na Uruguay. Hawa hawatakutana katika awamu ya kwanza.
Wengine ambao hawawezi kuwekwa pamoja ni Ivory Coast, Ghana, Algeria, Nigeria, Cameroon, Chile na Ecuador.
Kundi la tatu linajumuisha Japan, Iran, Korea Kusini, Australia, Marekani, Mexico, Costa Rica na Honduras.
Chungu cha nne kinajumuisha mataifa ya Bosnia-Hercegovina, Croatia, England, Ugiriki, Italia, Uholanzi, Ureno, Urusi na Ufaransa.
Ijumaa jioni itashuhudia nchi hizi 32 zikigawanywa katika makundi manane ya timu nne nne, ambapo mbili zitakazoshika nafasi za kwanza zitasonga mbele kwenye hatua ya mtoano.
Hapatakuwa na zaidi ya timu mbili za Ulaya kwenye kundi moja wakati kwa Amerika Kusini itakuwapo moja moja tu.
Tayari Brazili wamepangwa katika Kundi A wakati timu saba zilizobaki miongoni mwa zile nane bora za kundi la kwanza zitapangwa kuanzia Kundi B hadi H bila kufuata utaratibu maalumu.
Timu hizo katika chungu cha kwanza ndizo zinashika nafasi za juu kwa kiwango cha soka duniani kwa mujibu wa Fifa na hivyo zinapata faida ya kutocheza na wababe wenzao, bali zitapangwa dhidi ya hizi nyingine 24.