*Brazil na Cameroon, Ghana na Wajerumani
*England na Italia, walalamikia hali ya hewa
Makundi ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil yamepangwa, ambapo Simba Wasiofugika wa Cameroon wamepangwa kundi moja na Brazil.
Wengine katika kundi hilo la A ni Croatia na Mexico wakati kundi B kuna nchi za Hispania, Uhplanzi, Chile na Australia.
Wawakilishi wengine wa Afrika, Ghana wamepangwa katika kundi lililo na timu ngumu ya Ujerumani, sawa na Ureno ya Cristiano Ronaldo na Marekani.
Katika droo hiyo iliyofanywa Ijumaa hii nchini Brazil, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) linaonesha kwamba Nigeria watakuwa katika kundi moja na Argentina, Bosnia-Hercegovina na Iran.
Ivory Coast wamepangwa na Colombia, Ugiriki na Japan wakati Algeria watakuwa katikati ya Ubelgiji, Urusi na Korea Kusini.
England, nchi yenye ligi inayopendwa zaidi kote duniani, wamepangwa na Italia, Uruguay na Costa Rica, huku Ufaransa inayochukuliwa kuwa dhaifu kutokana na kufuzu kwa mbinde wakiwa kwenye kundi moja na Uswisi, Ecuador na Honduras.
Tayari vyombo vya habari vya Uingereza vimeanza kuumua mambo kwa kusema kwamba England itakwaana na mabingwa mara nne wa kombe hilo Italia katika mechi yao ya fungua dimba Juni 15 mwakani, na Wataliano wamekuwa na kawaida ya kuwaliza Waingereza.
England wanafundishwa na kocha Roy Hodgson na watatakiwa kusafiri umbali wa maili 1,777 kutoka kwenye kambi waliyoamua kuweka jijini Rio kwa ajili ya mechi yao hiyo ya kwanza katika eneo linalotarajiwa kuwa na joto kiasi la Manaus, ndani ya msitu wa Amazon.
Mapema wiki hii, Hodgson aliitaja Manaus kama eneo la kuepuka kwa sababu ya hali yake ya hewa, inayodaiwa kufika hadi nyuzijoto 30 za sentigredi na unyevunyevu kufikia kadiri ya asilimia 80.
Hata hivyo, baada ya matokeo ya droo hiyo kutangazwa, bosi wa England alieleza kufurahishwa na kupangwa na nchi mwenza kutoka Ulaya, akisema kwamba wote watakuwa wakisumbuliwa na hali hiyo.
Uruguay nao walipata kutwaa kombe hilo mara mbili, na wanaye mchezaji tegemeo wa Liverpool, Luis Suarez na Edinson Cavani.