Mojawapo ya mambo ninayopenda kutafakari pamoja na wasomaji wa Tanzaniasports ni kuibuka kwa makocha wa Burundi katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Makocha wazawa wanaweza kuwa na faida ya gharama nafuu kuishi nchini, kutotakiwa kuwa na vibali vya kazi kutoka serikalini. Makocha wazawa wanahitaji leseni ya TFF pekee pamoja na huduma za klabu zenyewe katika timu zao. Mahitaji mengine ya kitaaluma yanafahamika na hivyo sio hoja yangu.
Hata hivyo kwa miaka ya karibuni tumeona timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zikivuka mipaka kuajiri makocha wa nje. Ajira ya makocha wa kigeni ilikuwa ikizunguka kwa klabu za Yanga, Simba, Azam na Mtibwa, huku zingine zikijitutumua pasipo mafanikio.
Makocha kutoka Kenya, Uganda, Malawi kwa nchi za Afrika mashariki, kati na kusini ndizo zimekuwa zikitoa makocha wengi. Mbali ya hapo ni makocha kutoka bara la Ulaya, kwenye nchi za Ulaya mashariki,magharibi na kati.
Msingi wa hoja yangu unajengwa katika dhana ya makocha wa kigeni kuja VPL kuzinoa timu mbalimbali. Taifa la Burundi limeondokea kuwa na makocha wengi wanaozinoa timu timu za Ligi Kuu Tanzania Bara. Hilo ni bila kujali kama wanaendelea na kazi hizo hadi sasa.
Kwa miaka hivi karibuni kumekuwa na wimbi la makocha kutoka Burundi wanaoajiriwa kuzinoa timu za VPL. Ettiene Ndayiragije ni kocha wa Burundi aliyefanya kazi kuanzia ngazi ya chini hadi juu. Nina maana alianzia klabu ndogo ya Mbao FC kisha akaenda kujiunga na timu KMC hadi Azam FC na sasa Taifa Stars.
Masoud Djuma Irambonaimana alikuja kujiunga na mabingwa wa soka Simba. Masoud Djuma alikuja Tanzania akitokea nchini Rwanda naye ni raia wa Burundi.
Hitimana naye alikuja kujiunga na timu ndogo ya Stand United ya mkoani Shinyanga na baadaye akatimkia KMC ya Kinondoni Dar es salaam kuchukua nafasi ya Ettiene Ndayiragije, alipotua Azam.
Baadaye Thiery Hitimana akaenda kujiunga Namungo F.C. vilevile Haruna Harerimana yeye alikuwa kocha wa Mwadui FC. baadaye akatimkia Lipuli F.C.
Pia Ramadhani Swazurimo alikuja kuwa kocha wa Mbeya City kuchukua nafasi ya Kinnah Phiri kabla ya baadaye kutimkia Singida United ya mkoani Singida.
Yupo Bahati Vivier ambaye ni kocha msaidizi wa Azam, naye ni raia wa Burundi akifanya kazi sambamba na Mzambia, Goerge Lwandamina. Kocha wa makipa wa Yanga, Vladimir Niyonkuru ambaye anafanya kazi pamoja na raia mwenzake Cedric Kaze wa Burundi.
Ingawaje kwa sasa makocha wazawa ndio wanaozinoa klabu nyini za VPL hadi naandika makala haya lakini haiondoi ukweli kuwa Burundi ni nchi iliyotoa makocha wengi miaka ya karibuni katika vilabu vyetu.
Vilabu vyetu vyenye makocha wazawa ni kama vile Tanzania Prisons (Salum Mayanga), Polisi Tanzania (Male Hamsini),Ruvu Shooting(Boniface Mkwasa), Namungo (Hemed Morroco), Simba (Seleman Matola), Mwadui (Amri Said), Dodoma Mji (Choki Abeid) na wengineo.
Kwa upande wa vilabu vyenye makocha wa kigeni ni Biashara United (Francis Baraza), Azam (George Lwandamina), Yanga (Cedric Kaze), Mbeya City (Mathias Lulee) na Mtibwa Sugar (Thiery Hitimana).
Kimsingi tunahitaji maarifa kutoka kwingine hususani nchi ambazo zimetuzidi uwezo na maendeleo ya soka ambako msingi wa elimu ya ukocha umekuwa mzuri zaidi kuanzia ngazi za watoto.
Ukiwachunguza makocha wanaotoka Burundi na kuja Tanzania utagundua wanachotuzidi hawa ni uzoefu wa kupata maarifa nje ya nchi yao. Wenzetu huwa wanatoka nje ya nchi kujifunza maarifa ya ukocha pamoja na kuzinoa klabu mbalimbali hata kama kuanzia ngazi za timu za watoto za klabu hizo.
Ndio maana makocha wa Burundi wanasambaa sana Tanzania, lakini makocha wetu wazawa hawatoki nje kujifunza elimu mpya ya ukocha. Tunahitaji maarifa kutoka ng’ambo ambako wametuzidi.elimu ya michezo.
Tanzania tunaweza kuwa na makocha wazuri, lakini ukweli ni kwamba wengi walicheza mpira usio na msingi. Vilevile makocha wetu lazima wahamasishwe kutafuta maarifa nje ya nchi katika mataifa jirani kama vile Musmbiji, Malawi, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Somalia, Sudan kusini, Sudan, Zambia, Zimbabwe na mengine ya karibu kwa kuanzia. Hata kuzinoa timu za vijana katika mataifa ya nje inawezekana pia kuwapa nafasi ya kujifunza mengi.
Pili, ili kuboresha nafasi za makocha ni kuhakikisha timu zinakuwa na wakurugenzi wa ufundi kikanuni yaani chini maagizo ya TFF. Wakurugenzi wenye uzoefu mkubwa wa soka wanaweza kuwa chachu ya mafanikio ya makocha wazawa kwani watasaidiwa maeneo kadhaa ambayo wataonesha upungufu ama kuongezewa ubora.
Si vibaya kuwapata wakurugenzi wa ufundi wenye viwango kama Kim Poulsen, Marcio Maximo, Victor Stanculescu, na wengi wenye kaliba zao.
Upande wa serikali bado haijawekeza vya kutosha kwenye sekta ya michezo. Kwamba hatuna la maana kwa kuwa mfumo wa kuibua vipaji na kuvilea na kuvikuza na kuviendeleza kuleta matunda.
Serikali inachoweza kuhakikisha inawezesha mazingira ya walimu wa soka nchini wanazalishwa na kwenda nje kujifunza zaidi masuala ya soka na michezo.