Menu
in , ,

MAKHIRIKHRI ILIKUWA NGOMA NZITO KWA YANGA

Tanzania Sports

Moja ya vitu ambavyo vilikuwa vinaonesha utofauti kati ya Yanga na
Township Rollers katika mechi ya jana ni utulivu wa timu zote mbili.

Utulivu ambao ulifanya kutengeneza mstari wa utofauti wa utengenezaji
na matumizi ya nafasi.

Township Rollers hawakuwa na presha kubwa ndani yao, kitu ambacho
kiliwafanya wawe watulivu na kufanya maamuzi ya uhakika ndani ya timu.

Maamuzi ambayo yalienda sambamba na ushirikiano wa timu kwa ujumla.
Timu ilipokuwa inaenda kushambulia, wachezaji wote walionekana
kushirikiana kwenda kushambulia na timu ilipokuwa inashambuliwa
wachezaji wote walishirikiana kukaba kwa pamoja na kwa nidhamu.

Nidhamu ambayo iliwafanya wajijenge vizuri na kuonekana bora kwa kila
kitu walichokuwa wanakifanya ndani ya uwanja.

Ukamilifu wa timu unaletwa na wachezaji kamilifu kwenye kila idara,
Township Rollers walikuwa wakamilifu kwenye mechi ya jana.

Hii ilikuwa tofauti sana na kwa upande wa Yanga, mfano eneo la
katikati la Yanga ambalo lilikuwa na Pato Ngonyani na Papy Kabamba
lilikuwa na ushirikiano hafifu.

Kwanini nasema hivo? Pato Ngonyani alionekana na msaada mkubwa sana
kipindi ambacho timu ilikuwa inakaba, lakini timu ilipokuwa inataka
kushambulia msaada wake haikuwa mkubwa sana kwa sababu Pato Ngonyani
hakuwa anaisukuma timu kwenda mbele.

Hali ambayo ilikuwa inamlazimu Papy Kabamba kuwa na jukumu yeye kama
yeye bila msaada wowote, majukumu yalikuwa mengi kwake tena dhidi ya
wachezaji ambao walikuwa wamekamilika.

Kitu hiki kiliwasababisha kina Emmanuel Martin na Pius Buswita
kutopata mipira mingi.

Hata wakati ambao kina Emmanuel Martin , Pius Buswita, Ibrahim Ajib
walipokuwa wanahitajika kusaidia kuchukua mipira katikati hawakuwa na
uwezo, hali ambayo iliwafanya wapwaye kwa kiasi kikubwa.

Hakukuwepo na mchezaji ambaye angeweza kuibeba timu kwenye wakati huo
mgumu kwa sababu Yanga ilikuwa imejaza wachezaji wa kawaida kwenye
timu isiyo ya kawaida ndiyo maana wanapata matokeo ya kawaida.

Hata kwenye benchi hakukuwepo na mchezaji ambaye angeweza kuingia na
kubadilisha hali ya mchezo ndani ya mchezo.

Kwenye mashindano haya ya kimataifa unatakiwa uwe na wachezaji wa
hadhi ya michuano hii ili timu ifike mbali.

Ni ngumu kupata matokeo makubwa kama unawachezaji wengi wa kawaida
ndani ya timu yako.

Yanga walipofika robo fainali ya kombe la shirikisho misimu miwili
iliyopita, ilikuwa na wachezaji wengi ambao walikuwa na uwezo wa
kubadilisha matokeo dakika yoyote.

Kipindi hiki Yanga haina tena wachezaji hao kwenye kikosi hiki, wana
wachezaji wengi sana wa kawaida ndani ya kikosi chao.

Ni kitu ambacho wanatakiwa kujifunza zaidi, wanapozidi kupata nafasi
ya uwakilishi wa kimataifa, wanatakiwa kupata wachezaji ambao wana
hadhi ya mashindano husika.

Huwezi kufika mbali kama unaidadi kubwa ya wachezaji ambao
hawajajengeka kwa kiasi kikubwa.

Ni jambo jema kuwaona kina Ramadhani Kabwili kuwaona wakianza kwenye
michuano mikubwa kama hii, lakini wachezaji hawa vijana wanatakiwa
wazungukwe na wachezaki wa madaraja ya juu ili wawe na uwezo wa
kujengeka na kuimarika katika misingi ya ushindi ndani yao.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version