MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania umeanza. Macho na masikio yatakuwa kwa timu za Yanga,Simba,Azam ambazo zinabariwa kunyakua taji la Ligi kuu. Lakini idadi kubwa ya washabiki wanazitazama Simba na Yanga kwa jicho la tatu na ndizo ambazo zinachochea mvuto wa Ligi Kuu.
Ni timu mbili ambazo ni kioo cha soka la Bongo. Simba na Yanga zimeanza Ligi Kuu msimu mpya kwa namna tofauti. Yanga waliibanjua Kagera Sugar, kabla ya kuvaana na Geita Gold wikiendi iliyopita. Simba walianza mkoani Mara kwa kupepetana na Biashara United na kutoka suluhu, kabla ya kuitandika Dodoma Jiji wikiendi iliyopita.
TOFAUTI ZAO
Katika michezo yao miwili hadi sasa Simba wamekuwa walewale, wanacheza pasi fupi fupi, kuandaa mashambulizi kutoka nyuma, kwenda langoni mwa adui. Kwa lakini kwa Yanga wamekuwa mahiri katika maeneo ya winga na mabeki wa pembeni.
Eneo la beki wa kati linaonekana kuwa imara zaidi huku mabeki wake wakiwa na umri mdogo. Dickson Job na Bakari Mwamyeto wanaongoza jahazi la Yanga. Pia mabeki wao wa pembeni kulia Djuma Shaban, beki wa kushoto Kibwana Shomari na winga wa kulia Jesus Moloko na kushoto Farid Mussa wameanza msimu kwa kuzisumbua safu za ulinzi.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga ina Yacouba Sogne, Herieter Makambo, Yusuf Athuman, Ditram Nchimbi na Foston Mayele. Ni uamuzi wa kocha Nasredine Nabi kuoanga mshambuliaji wa kuanza naye.
Kwa Simba wameanza msimu wakikabiliwa na majeruhi wengi, Sadio Kanoute,Shomari Kapombe,Ousamane Sakho,Joash Onyango,Thadeo Lwanga na Kennedy Juma. Hii inampa wakati mgumu kocha wao Didier Gomes kupanga kikosi cha kwanza. Katika michezo miwili Simba wamepata pointi nne.
Tofauti za timu hizo mbili ni kwamba kwamba Simba wanacheza kwa falsafa yao, lakini Yanga bado hawaonekani kucheza kitimu kama walivyo wapinzani wake. Yanga wana ukuta mgumu,kiungo kigumu na safu hodari ya ushambuliaji lakini ingali haina kasi na muunganiko mahususi katika mbinu zao.
MASTAA WAO
Yanga wana viungo wawili wapya Yannick bangala na Khalid Aucho. Halafu wa golikipa mgumu na akili nyingi Djigui Diarra, kisha wana miguu ya kupachika mabao ya kutosha pale mbele iwe kwa mfumo wa kupanga washambuliaji wawili au mmoja lakini Makambo,Mayele,Sogne,Athuman na Nchimbi wana uwezo wa kupachika mabao ya kutosha.
Simba wana kiungo hodari Sadio Kanuote na mawinga wawili hatari Peter Banda na Duncan Nyoni wote kutoka nchini Malawi. Bado wana miguu yao yenye mabao ya kutosha kutoka kwa nahodha John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere.
Mastaa wa timu hizo mbili wanacheza kusaka ushindi, lakini kwa kiasi fulani Simba wanacheza mpira wao wa kutafuta ushindi huku wakionesha burudani. Yanga wameleta shughuli pevu katika mechi zao mbili.
MATARAJIO KWA VIPAJI VIPYA
Simba wamesajili nyota wapya Peter Banda, Duncan Nyoni raia wa Malawi, na wengine Sadio Kanoute,Pape Osmane Sakho kutoka Senegal, Yusuf Mhilu, Jimmy Mwandike. Mashabiki wanataka kuona vipai vipya vikiziba mapengo ya Cletous Chama na Luis Miquissone, wakati Yanga hawataki kukumbuka ukame wa mabao wa Ditram Nchimbi na Michael Sarpong.
Washambuliaji wa Yanga wana kazi ya kufanya msimu huu, sawa na wachezaji wapya wa Simba ambao wanatarajiwa kuchukua nafasi za Chama na Miquissone. Matarajio hayo ndiyo yataamua kuwa wamefanikiwa au hawajafnikiwa. Matarajio makubwa waliyonayo mashabiki wa pande zote mbili ndiyo presha inayowakabili pia wachezaji wao.
WALINZI NA WAFUMANIA NYAVU
Ili timu iweze kuchukua ubingwa inatakiwa kuruhusu mabao machache kuingia katika lao. Pia ni lazima timu iweze kupachika mabao mengi ya ushindi ili pointi tatu zipatikane.
Ushindani uliopo katika safu ya ushambuliaji Simba ndiyo itakuwa chachu ya kutetea ubingwa wao. John Bocco,Chriss Mugalu,Meddie Kagere watakuwa na jukumu la kupachika mabao ya kutosha ili kuipa nafasi Simba kutetea ubingwa wao. Ili kazi za washambuliaji ziwe rahisi inatakiwa mawinga wao Yusuf Mhilu,Peter Banda na Duncan Nyoni watengeneze mabao.
Yacouba Sogne,Herieter Makambo,Yusf Athuman,Fiston Mayele na Ditram Nchimbi wanatakiwa kupachika mabao ya kutosha kuipa ubingwa Yanga kwa mara kwanza baada ya kuukosa kwa miaka minne mfululizo. Ili washambuliaji wa Yanga wafanye kazi kwa ufanisi ni lazima mawinga wao Farid Mussa,Deus Kaseke, Jesus Moloko, wazalishe nafasi nyingi za magoli.
UKUTA WA KIUNGO
Khalid Aucho, Yannick Bangala, Tonombe Mukoko watakuwa na kazi ya kumlinda Feisal Salum ili afanye kazi yake kwa ufanisi. Viungo hao wakabaji watakuwa na jukumu kujenga ukuta wa kiungo ambao hautakuwa rahisi kuwaruhusu wapinzani kuwakaribia mabeki wao.
Taddeo Lwanga,Sadio Kanoute,Jonas Mkude,Muzamiru Yassin, watakuwa na kazi kubwa ya kuijenga ukuta wa timu na kuhakikisha Rarry Bwalya anafanya kazi yake kwa ufanisi kwa kuzalisha nafasi za kutosha za mabao.
GOLINI KUNA WAGUMU
Aishi manula ni glikipa namba moja nchini Tanzania. huyu amedumu kikosi kwa muda mrefu tangu alipohamia akitokea Azam FC miaka minne iliyopita. Kwa mantiki hiyo eneo la golikipa lina mtu imara mwenye kila sifa za kuwa mlindamlango hodari katika soka la kisasa Tanzania.
Yanga wamesajili golikipa mpya huyo raia wa Mali. Djigui Diarra ni bonge la golikipa. Uwezo wake langni si wa kutiliwa shaka. Silaha ya tatu ni uwezo wa golikipa Djigui Diarra ambaye anacheza kama makipa wa kisasa. Djigui anaweza mkubwa kupiga pasi kuwafikia walengwa ili kuanzisha mashambulizi, anacheza kama sentahafu ikiwemo kuosha hatari langoni mwake.
UAMUZI WA MBINU
Kwa Simba mfumo wa 4-2-3-1 au 3-2-4-1 ndiyo njia yao ya kupata mafanikio. Simba wanao viungo wann wakabaji, Taddeo Lwanga,Jonas Mkude,Muzamiru Yassin na Sadio Kanoute, ambao mwalimu wao Didier Gomes ataamua nani aanze kikosi cha kwanza.
Yanga wanaonekana kujikita katika mfuo 4-2-3-1 au 4-2-1-3-1 na 4-5-1. Mifumo hii kutokana na aina ya viungo na washambuliaji walionao. Yanga waanza na viungo wakabaji wawili Yannick Bangala,Zawadi Mauya,Khalid Aucho ua Tonombe Mukoko. Utakuwa uamuzi wa kocha mwenyewe nani aanze mchezo.