HAKIMU; “Ndugu Feisal Salum Abdallah, maarufu kama Fei Toto, siku hizi wengine wanakuita Zanzibar
Feisal unashtakiwa na waajiri wako klabu ya Yanga katika mahakama hii kwa kosa la kuvunja mkataba
bila kufuata taratibu. Je unakubali kutenda kosa hilo? Na kama hukubali, je utakuwa tayari kuadhibiwa
kwa mujibu wa sheria na taratibu iwapo utapatikana na hatia?”
FEI TOTO; “Nashukuru sana mheshimiwa hakimu kwa kunipa nafasi kuwa mzungumzaji wa kwanza
katika shauri hili. Mheshimiwa hakimu nakiri mbele yako na mbele ya mahakama hii tukufu kwamba
nilivunja mkataba kwa kufuata utaratibu unaopaswa. Iwapo mahakama hii itagundua kwamba nilifanya
kosa au nilikiuka taratibu yoyote katika uvunjaji wa mkataba wangu na Yanga, nipo tayari kuadhibiwa
kwa mujibu wa sheria na taratibu.”
HAKIMU; “Ningependa utulivu uwepo wakati natoa nafasi kwa wakili namba moja upande wa utetezi
kuzungumza kwa niaba ya mshtakiwa. ikumbukwe karani wa korti yupo makini kurekodi kila tukio
linaloendelea kortini. Nizidi kusisitiza utulivu kutoka kwa wasikilizaji ili kumrahisishia kazi karani. Kama
upo tayari, ndugu wakili unaweza kuendelea.”
WAKILI NO 1; “Mheshimiwa hakimu nasimama kwa niaba ya mshitakiwa! Kama alivyokiri mteja wangu,
ni kweli kwamba ndugu Fey aliwasilisha barua ya kuvunja mkataba wake na Yanga katika tarehe tajwa
hapo awali. Kitu pekee tusichokubali ni kwamba, mteja wetu alifuata taratibu zote alizopaswa kufuata
katika mchakato wa kuvunja mkataba na waajiri wake wa zamani.”
“Mheshimiwa hakimu hii ni nakala ya mkataba walioingia Feisal Salum na Yanga miaka miwili iliyopita.
Katika mkataba huu, kipengele cha 14.7 kinatoa maelekezo jinsi ya mteja wetu kuvunja mkataba iwapo
ataona haja ya kufanya hivyo. Kipengele hicho kinaeleza kwamba, Feisal Salum atalazimika kulipa ada
ya usajili aliyoipokea wakati wa kusaini mkataba huu, pia atalazimika kulipa walau mshahara wa miezi
mitatu.”
“Mteja wetu alizingatia yote haya kama vilivoanisha vipengele vya mkataba ambao nimeuwasilisha
katika meza yako. Hivyo, mteja wangu hana kosa lolote na ninaomba mahakama hii tukufu ifutilie mbali
kesi hii.”
HAKIMU; “Wakili namba mbili upande wa mshitaki sasa ni nafasi yako”
WAKILI NO 2; “Mheshimiwa hakimu, ni kweli kipo na tunakitambua kipengele alichokizungumza ndugu
wakili. Lakini katika kipengele hicho, kimeelekeza vema kwamba mshitakiwa anaweza kuvunja mkataba
iwapo tu kutakuwa na hali isiyo ya kawaida.”
“Katika barua ya mshitakiwa hakueleza sababu ya kuvunja ya mkataba kama anavohitajika na kipendele
hiki. Aidha, mamlaka ya kusimamia soka duniani inaelekeza kwamba hali isiyo ya kawaida ni kama
kutokulipwa mshahara ndani ya miezi mitatu, kutocheza kwa muda mrefu na sababu zinazofanana.
Hivyo, mshitakiwa hakuwa na haki ya kuvunja ya mkataba huu. Ninaomba mahakama yako iamuru
Feisal Salum kuwa mali ya Yanga na sisi tutamchukulia hatua kulingana na sheria zetu.”
HAKIMU “Nitoe muda wa mapumziko wakati tukiendelea kujadili kabla ya kutoa hukumu. Tutaendelea
baada ya masaa mwili.”
(Wadau walipokutana nje muda wa mapumziko)
MDAU 1 ” Nimezungumza na Fey Toto, pale Yanga anaonewa sana. Hata mimi ningekuwa yeye,
ningeondoka. Fikiria kazi anayofanya na mshahara anaolipwa. Haviendani kabisa. Wale wageni
wanapewa pesa nyingi halafu hawafanyi kazi kubwa. Bora Fei Toto aondoke”
MDAU 2 “Tumia akili kidogo. Fei Toto hakulazimishwa kusaini mkataba na Yanga. wakati anasaini
alikuwa na akili timamu. Alikubali kulipwa mshahara anaolipwa kwa sasa. Kama analipwa mshahara
mdogo, angekataa kipindi ameitwa mezani kusaini mkataba”
MDAU 1 ” Fei Toto hataki kabisa kucheza Yanga. Bora wamuache aondoke kuliko kuwa na mchezaji
ambae hana mapenzi ya dhati na klabu”
MDAU 2 “Kwahiyo kila mchezaji akitaka kuondoka aseme sina mapenzi na hii klabu halafu aachiwe
huru? Kikubwa kama anataka kuondoka akae chini na Yanga wazungumze. Wakubaliane kiasi
anachopaswa kulipa kisha wamalizane. Au kama kuna timu inamtaka, wakae chini na Yanga
wamalizane”
MDAU 1 “Naona muda wa kusikia hukumu umefika. Twende ndani tukasikilize.”
HAKIMU “Baada ya kusikiliza pande zote mbili, mahakama hii imeamua kwamba mchezaji Feisal Salum
ni mali ya Yanga. Hivyo Feisal anapaswa kurejea Yanga na taratibu zingine zifuate. Aidha,nafasi ya rufaa
ipo wazi. Hivyo, mshitakiwa anaweza kukata rufaa katika mahakama ya juu zaidi.”