Menu
in , ,

MAHADHI WAKUMBUKE MAZEMBE UJIFUNGE MASOMBO

Tanzania Sports

Najua ushapitia nyakati tofauti zenye majira tofauti sana katika
maisha yako, na kuna wakati mambo yako yalienda shoto na yakarudi
upogo kwa sababu mbalimbali na kuna nyakati mambo yako yalitembea
kwenye mstaari mnyoofu.

Nyakati hizi zilikuwa na maana kubwa sana kwenye maisha yako kwa
sababu maisha ya mwanadamu hukamilika kipindi ulimi wake unapoonja
pilipili na asali.

Maisha hayawezi kuitwa maisha kama yatakuwa na upande mmoja wa
shilingi, ndiyo maana tunatakiwa tuwe dhabiti pindi kombo
anapotutembelea sebuleni kwetu.

Kuna wakati miguu yako ilikuwa mizito kwa kila hatua uliyokuwa
unajaribu kupiga ili usogee kwenda mbele.

Mbele yako hukuona mwangaza wowote, giza lilikuwa linatawala mboni
zako za macho kiasi kilichopelekea wewe kutoiona njia sahihi
uliyotakiwa kuifuata ili kufika ulipokuwa unatamani kupafikia kabla
hujakanyaga jiji la Dar es Salaam.

Jiji ambalo hutia upofu wa akili kipindi unapotanguliza kichwa
kukanyaga ardhi yake na kuipa miguu jukumu la kuona na kufikiria kwa
sababu tu inauwezo wa kupiga hatua.

Jiji ambalo lilikufanya usahau uliyokuwa unayaota kipindi ambacho upo
Coastal Union.

Kipindi ambacho ulikuwa unafanya mazoezi kwa jitihada kubwa ili
ufanikiwe kufika kariakoo ukiamini ndiyo njia sahihi kwenda
alipofanikiwa kwenda Nonda Shabani.

Hapana shaka habari zake zilikuwa zinakupa matamanio ya kufikia hatua
kubwa ya mafaniko, ukaongeza jitihada za mazoezi kila uchwao.

Jitihada ambazo zilizaa matunda ya wewe kufika Kariakoo, sehemu ambayo
ina mengi mapya ya kuvutia machoni mwa mgeni yoyote.

Mapya ambayo huyumbisha kwa kiasi kikubwa malengo ambayo awali mgeni
yoyote huwa anayapanga kabla hajafika Kariakoo, na kusahau kabisa
umuhimu wa kufanya kilichokupeleka.

Ndiyo maana ulipunguza juhudi za kufanya mazoezi mara baada ya
kukanyaga ardhi ya Kariakoo, na ukawezeka bidii zako sehemu nyingine
tofauti na ile iliyokupeleka Kariakoo

Bidii za kubadilisha muonekano wa mwili zikazidi bidii za kufanya
mazoezi kwa juhudi na kusikiliza walimu wa mpira, masikio yako yakawa
yanatamani kumsikiliza mwalimu wa mitindo ili akupe mbinu za
uanamitindo zilizokufanya bidii zako uziwekeze huku.

Ukafanikiwa kuwa na muonekano uliowavuta warembo wa kariakoo ambao
walikutia upofu na mapenzi yao mazito.

Akili yako ikawa inawaza zaidi nani ana penzi tamu kati ya Mwajuma na
Asha na kusahau kabisa kujiuliza nani atakuangalia uwanjani ili
akupeleke alipofanikiwa kwenda Nonda Shabani

Akili yako ikajaa ukungu, na ukawa unaona kucheza mechi na Asha kuna
umuhimu mkubwa kuliko kwenda kucheza timu moja na Lukaku.

Ukamuonesha ushirikiano Asha, hukutosheka ukamuongeza Mwajuma ambaye
alikufunza kutumia vileo ambavyo vilikuondoa kwenye mstari uliokuwepo
awali.

Mstari ambao ulikuwa unaonesha uko kwenye daraja la kuwa mchezaji bora
baadaye kutokana na kipaji chako.

Kipaji ambacho kilikuwa madhubuti na murua, kipaji ambacho kiliwaacha
hoi TP Mazembe walipokuja kucheza na Yanga kwenye uwanja wa Taifa

Mechi ambayo ilionesha njaa uliyokuwa nayo kipindi hicho, mechi ambayo
ilionesha dhahiri una lengo la kufika mbali.

Ulikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza katika kiwango ƙkikubwa sana,
kiwango ambacho kama ungetulia na kukiendeleza leo hii ungekuwa mtu
unayemfuata Simon Msuva.

Nakumbuka mpaka nywele zako ulivyokuwa umeziweka siku ile, nakumbuka
mpaka rangi ya viatu ulivyotumia siku ile hii ni kwa sababu ulikuwa
nyota wa mchezo ule.

Lakini kwa sasa nyota yako ishafifia kwa kiasi ƙkikubwa, hakuna
jitihada kubwa unayoionesha kufikia malengo yako makubwa uliyokuwa
unayahubiri kipindi ulipokuwa unahojiwa na vyombo vya habari.

Kuna wakati inauma sana unapoona kipaji kama chako kikikosa mwelekeo
sahihi, kipaji ambacho unaamini kingeweza kuwa na faida kubwa kwa
taifa kama kingepata msimamizi sahihi wa hicho kipaji.

Hapo ndipo huwa tunajikwaa mara kwa mara bila kuchukua tahadhari
yoyote, vipaji vingi havina wasimamizi wazuri ndiyo maana ni rahisi
kupeperushwa hata kwa upepo wa mluzi.

Inawezekana ni eneo ambalo haliangaliwi kwa jicho pana, lakini ni eneo
muhimu katika makuzi ya kipaji cha mchezaji.

Juma Mahadhi alikosa mtu mzuri wa kukisimamia kipaji chake ndiyo maana
akaenda njia tofaufi na njia yake ya awali, natamani awe anaiangalia
mara kwa mara mechi aliyocheza dhidi ya TP Mazembe natumaini
itamsaidia kurudi kwenye njia yake sahihi, hajachelewa bado ana muda
wa kukaa na kujirekebisha.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version