JIJI la London na maeneo mengine ya soka duniani, yalitikiswa na ujio wa bilionea, Dk Sulaiman Al Fahim ambaye alishtua dunia pale alipomwekesha rekodi, Robinho kwa kumsajili Manchester City kwa pauni 34.5mil.
Bilionea huyo, tayari ametangaza madau mbalimbali ya kuwanasa wachezaji nyota kwa gharama yoyote. Manchester City imeanza kusikika kutokana na ujio wa tajiri huyo mwenye kumiliki mali ya pauni460bilioni.
Chelsea nayo ilikuwa timu isiyosikika sana, lakini kuja ka Abraham Abramovich ambaye anamiliki mali za pauni 12bilioni ilianza kusikika na hata kutwaa ubingwa wa England 2005 ikiwa ni miaka 50. Mara ya mwisho, Chelsea ilitwa ubingwa 1955.
Hiyo ni mifano michache ambayo inaonyesha kuwa timu zikiwezeshwa zinaweza. Mfano halisi ni Chelsea, ilikuwa haisikiki sana zaidi ya Liverpool, Manchester United, Arsenal, labda na Everton na Tottenham.
Ni hivi majuzi tu, Kampuni ya Bia Tanzania, TBL iliiingia mkataba wa mabilioni ya pesa kudhamini klabu za Simba na Yanga.
TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro itazigharamia timu hizo vifaa, usafiri, mishahara ya wachezaji na kutangaza dau la Sh30mil kwa atakayetwaa ubingwa na Sh10mil kwa mshindi wa pili kwa timu hizo.
Kampuni hiyo imeonyesha kweli inataka kuleta ushindani na maendeleo ya soka kwani udhamini unasaidia kutengeenza morari kwa wachezaji wa timu husika.
Lakini pamoja na hayo, TBL ingeibukia kwa timu nyingine ili kuleta ushindani. Simba na Yanga ni timu kubwa, lakini hata ndogo zikiwezeshwa zitaweza kuibuka.
Moro United ilikuwa kati ya klabu kubwa kutokana na kumilikuwa na Kampuni ya Mafuta ya TIOT japokuwa kwa sasa ipo ipo tu, lakini wakati huo ilikuwa na uwezo wa kuchukua wachezaji wazuri na kutoa ushindani.
Pamoja na kwamba maendeleo ya soka yatakuwepo kwa Simba na Yanga kwa kuwa zina uwezo, bado udhamini huo unadumaza soka kwani Simba na Yanga ambazo tayari zina nguvu, zinazidi kuongezewa nguvu wakati wengine wakiwa taaban.
Kimsingi, huwezi kusema maendeleo ya soka wakati Villa Squad, Moro United, na nyingine hazina wadhamini. Timu kama Ashanti au Pan African zilikuwa na wachezaji wazuri, lakini ilishindwa kujimudu kutokana na kutokuwa na wadhamini na kujiendesha ‘kimkandamkanda’ na hatimaye kushuka daraja.
Timu hizi ambazo si ‘ma-giant’ zingewezeshwa. TBL wangeonyesha kweli wanataka maendeleo ya soka kwa kudhamini klabu za chini nazo ziweze kutoa ushindani.
Kama timu zitawezeshwa kwa kila hali, ushindani ungekuwa mkubwa katika ligi na hata kupatikana timu bora ya taifa.
Ligi inapokuwa ya ushindani, hata timu ya taifa inakuwa nzuri kwani inapata wachezaji walioshindana hasa na kuzoea ushindani katika usawa, lakini kwa hili la kuzisaidia klabu chache tena zenye nguvu ya ziada ya mashabiki, haina maana hata kidogo.
Kusaidia Simba na Yanga pakee hakusaidii kuleta ligi yenye ushindani kwani Miamba hii inapambana na vibonde, klabu masikini ambazo zinaendeshwa kwa kutegemea michango ya wanachama au mikopo.
Lakini iwapo kila timu katika ligi inakuwa na udhamini na kufanya usajili wa kutisha kama ilivyokuwa kwa Man City, kufanya maandalizi ya kutosha, huduma bora na maamuzi ya haki kwenye ligi bila shaka ligi itakuwa na ushindani na kutoa wawakilishi makini.
lakini yote haya yatawezekana iwapo tu wafadhili kama TBL na wengine watakumbuka kufumba macho na kuamua kusahau sifa za magazetini na kusaidia klabu vingine ili kukuza soka letu.