Viongozi watendaji wa klabu ya Arsenal wameamua kujipunguzia sehemu ya mishahara yao kwa ajili ya kufidia kwa kiasi athari za virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Jopo hilo la watendaji ambao kimsingi ndio mabosi, wataachia theluthi ya mishahara yao kwa kipindi cha miezi 12 ijayo, ikiwa ni kutolea kwao kusaidia wengine wanaoathirika, wakati huu ambapo Ligi Kuu ya England (EPL) imesimama.
Taarifa ya Washika Bunduki wa London imesema kwamba waajiriwa wengine wataendelea kulipwa mishahara yao mizima pasipo kukatwa kitu, na kwamba klabu haitajitumbukiza kwenye kukata mishahara na kuweka waaajiriwa chini ya mpango wa serikali ambao huwapa fidia kiasi.
Mazungumzo binafsi yalikuwa yakiendelea na wachezaji kuona kipi wanaweza kufanya kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kifedha zilizo mbele pamoja na kukabili madhara ya Covid-19. Kocha wao, Mikel Arteta, alipata homa hiyo lakini alishapona.
Baadhi ya klabu za ndani na nje ya nchi zilitangaza kuwakata wachezaji wao mishahara, kutowalipa sehemu ya mishahara wafanyakazi ambao si wachezaji au kuwapeleka likizo na kutegemea serikali iwasaidie.
Mazungumzo ya pamoja katika ya mamlaka mbalimbali za soka nchini na wachezaji hayakufikia mwafaka ambapo EPL walikuwa wakitaka klabu ziwakate wachezaji asilimia 30 ya mishahara yao. Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kilinga wachezaji kukatwa mishahara, kikieleza kwamba kungeathiri michango ya kodi inayoelekezwa kwenye Idara ya Huduma za Afya (NHS).
Arsenal wakasema katika taarifa yao kwamba tangu kuanzishwa kwa klabu miaka 134 iliyopita, rekodi zinaonesha kwamba hiki ni moja ya vipindi vigumu zaidi.
“Ni moja ya vipindi vigumu zaidi katka historia yetu ya miaka 134 na changamoto ni kubwa. Kwa hivyo, ni mujimu kuchukua hatua, kuwajibika vyema kwa kufanya jambo kukabiliana na athari inayotarajiwa kwenye sekta ya fedha kwa ajili ya kuilinda Arsenal dhidi ya kile kinachoweza kutokea katika miezi ijayo,” ikasema taarifa hiyo.
Hadi ligi inasimamishwa, Arsenal walikuwa kwenye nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi, ambapo walikuwa wameanza kupata ‘uhai’ zaidi na kushinda mechi, baada ya kuanza ligi kwa tabu chini ya kocha Unai Emery.
Bodi ya Arsenal pia imeamua kwamba ikiwa mechi zilizosalia itaamuliwa na mamlaka na wadau zichezwe bila watazamaji au mechi husika kufutwa kabisa, basi washabiki wake watapata marejesho ya fedha za tiketi walizokuwa wamenunue au kufidiwa kwa namna nyingine itakayoonekana inafaa.
Ama kwa vibarua ambao hufanya kazi siku za mechi za nyumbani tu kwenye Uwanja wa Emirates, Arsenal wanasema watalipwa kiwango chote ambacho walikuwa wakipata. Soka ya England imesitishwa kwa muda usiojulikana hadi visa vya Congid-19 vimalizike na serikali kufuta amri za watu kukaa ndani