Wababe wa soka miongoni mwa klabu za Ulaya wanaendelea kuoneshana kazi, huku matokeo yakiwa mchanganyiko – baadhi yakitarajiwa lakini mengine yakishitua na kuacha wadau wa soka vinywa wazi.
Wakati mabingwa watetezi wa England, Manchester City waliwachezesha kwata na kuwashinda Real Madrid nyumbani kwao Santiago Bernabeu katika makutano ya kwanza baina ya Pepe Guardiola na Zinedine Zidane, Juventus walikatia pumzi ugenini.
Man City walikwenda kwenye mechi hiyo wakiwa na mawazo juu ya kuzuiwa kwao kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa miaka miwili kuanzia msimu ujao huku matumaini ya kutetea ubingwa wa England yakiwa yameyeyuka.
Hata hivyo, Guardiola alikuwa amewapa moyo vijana wake kwamba wapigane kufa na kupona kwa sababu bado maisha yapo na kwamba wanaweza kushinda rufaa waliyokata Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), na kweli wakafanikiwa kushinda kwa 2-1.
Nahodha wa Madrid, Sergio Ramos atajilaumu na pengine hata wakitolewa kwenye mechi ya mkondo wa pili itakayopigwa Etihad, England washabiki wa ndani na nje ya Madrid na Hispania watamwona ndiye kisababishi, kwani alimkwatua Gabriel Jesus kwenye eneo la penati, akapewa kadi nyekundu na Man City wakafunga kwa penati ya Kevin de Bruyne.
Madrid walianza vyema mchezo lakini hadi wanakwenda mapumziko hakuna waliokuwa wamepata bao. Ilibidi wasubiri hadi saa nzima kumalizika mchezoni Isco alipowanyanyua vitini washabiki. Hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika 17 tu, likasawazishwa na Jesus.
Penati ya dakika ya 83 ilizamisha ndoto za Zidane na kuandika historia mpya kwa Manchester City kushinda kwenye uwanja wa Real Madrid. Baada ya mechi, Guardiola alishindwa kujizuia akisema kwamba hawajazoea mambo kama hayo.
“Kushinda hapa Bernabeu kumetufanya kuridhika kwa kiasi kikubwa. Ni ajabu kuweza kushinda hapa kwa sababu hatujazoea mambo kama haya. Tunaamini itatusaidia kwa nyakati zijazo kujiamini zaidi na kuweza kuingia kwenye uwanja wowote na kucheza kama tulivyofanya dhidi ya Real,” yalikuwa maneno ya Guardiola.
Madrid ndio wanashikilia rekodi ya kutwaa ubingwa mara nyingi zaidi. Hata hivyo, mchezaji wa Madrid, Casemiro, alisema bado mtanange haujaisha, akisema mechi ijayo watapigana kama walivyocheza vyema kwa dakika 75 hapo Bernabeu.
Anasema kama kuna timu inayoweza kupindua meza kwa maana ya kugeuza matokeo, ni Real Madrid. Mechi ya mkondo wa pili itafanyika Machi 17 nchini England.
Lyon wa Ufaransa waliwashangaza Juventus kwa kuwapiga bao 1-0. Walicheza kwa kujituma sana na alikuwa Lucas Tousart aliyefunga bao pekee la mchezo dakika ya 31, Juve wakapigana wakiwa na Cristiano Ronaldo kwa dakika zote zilizobaki lakini hawakuweza kusawazisha bao hilo.
Houssem Aouar, mzaliwa wa Lyon huko huko ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi na ndiye aliyetoa usaidizi wa bao hilo, huku Juventus wakishindwa kulenga hata shuti moja golini. Mechi ya mkondo wa pili itafanyika Allianz Stadium Machi 17.
Kwenye matokeo ya Jumanne, Chelsea walichanwa chanwa na Bayern Munich kwa kupigwa mabao 3-0, mawili kati ya hayo yakitiwa kimiani na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry. Bao jingine lilifungwa na Robert Lewandowsky. Chelsea sasa wamepoteza mechi nane nyumbani katika mashindano yote msimu huu.
Kwingineko, Napoli wakicheza nyumbani Italia waliwabana Barcelona na kwenda nao sare ya 1-1 kwenye mechi ambayo Artur Vidal wa Barca alipewa kadi nyekundu dakika ya 89 kwa kosa la kumchezea vibaya Fabian Ruiz. Mtendwa alipoonesha kuhamaki, Vidal alimsukuma usoni, akapewa kadi mbili za njano na nyekundu haraka haraka.
Bao la Napoli lilifungwa na Dries Mertens nusu saa tangu mechi kuanza kutoka umbali wa yadi 18 wakati la kusawazisha liliwekwa kimiani na Antoine Griezman dakika ya 57 kutokana na majalo ya chini chini ya Nelson Semedo. Watarudiana Machi 18 Camp Nou kwao Barcelona.