Menu
in , , ,

MAAJABU YA SIMBA KWA MUFULIRA WANDERERS 1979

NCHI ya Tanzania, ndani ya miaka 51 ya uhuru wake, imekuwa na matukio ya kusisimua yanayohusu soka yake kama vile Cosmopolitan ya jijini Dar es Salaam kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kuiwakilisha nchi yetu kwenye mashindano ya vilabu ya bara hili mwaka 1967.
Kuna kipigo cha Yanga kwa Simba (wakati huo Sunderland) cha mabao 5-0 mwaka 1969, Yanga kutupwa nje ya mashindano ya klabu bingwa Afrika na Asante Kotoko ya Ghana kwa kura ya shilingi jijini Dar es Salaam mwaka 1969 na Simba kubeba ubingwa wa kwanza wa vilabu vya Afrika Mashariki katika mashindano ya kwanza kabisa mwaka 1974 jijini Dar es Salaam.
DSC03050
Kuna tukio la Mseto ya Morogoro kubeba ubingwa wa Tanzania ikiwa klabu ya kwanza kutoka Dar es Salaam kufanya hivyo mwaka 1975 baada ya kuilaza kwenye fainali Nyota ya Mtwara kwa mabao 3-1. Hiyo ilikuwa fainali isiyo ya Yanga na Simba kwani enzi hizo za bingwa wetu kupatikana kwa mtoano, fainali zilikuwa baina ya Yanga na Simba tu, ukiondoa mwaka 1973 zilipokutana kwenye nusu fainali, Simba kuilaza Yanga 1-0, kucheza fainali na Lake Stars ya Kigoma, kushinda 2-0 na kubeba ubingwa.
Lipo tukio la Simba kufika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa ya Afrika mwaka 1974, mwaka ambao ulikuwa wa mechi ya Yanga na Simba inayoongoza kwa msisimko hadi sasa ya Nyamagana Mwanza ambapo kwenye dakika ya 87, Yanga ilisawazisha bao la Simba la dakika ya 16 na kupata la ushindi kwenye dakika 30 za nyongeza. Bao la Simba lilifungwa na Adam Sabu aliyeingia badala ya Saad Ali aliyeumia vibaya. Bao la kusawazisha lilifungwa na Gibson Sembuli na la ushindi Sunday Manara.
Kuna lile la Yanga kufukuza wachezaji karibu wote wa kikosi cha kwanza mwaka 1976 na kupigwa 6-0 na Simba mwaka mmoja baadaye wakiwa wameshajisuka vya kutosha.
Tukio kubwa kuliko yote ni lile la timu yetu ya Taifa kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria, tulipofungwa 3-1na Nigeria, 2-1 na Misri na kumaliza kwa sare ya 1-1 na Ivory Coast. Tuna pointi moja ya mashindano hayo huku kukiwa na timu miaka hii zinazomaliza bila pointi!
Tukio la kushangaza kuliko yote ni la mwaka 1979 ambapo Simba
ililala hapa 0-4 kwa Mufurira Wanderers ya Zambia kwenye mashindano ya ubingwa wa Afrika lakini ugenini wenyeji Mufurira Wanderers walilala 0-5 kwa Simba. Tukio hili lilikuwa na maajabu mengi ambapo tumechagua matano kulingana na idadi ya magoli waliyofunga Simba ugenini na kuvuka hadi raundi iliyofuata. Maajabu hayo ni:-
  • Goli la kwanza– Maajabu ni kwamba si rahisi sana kwa timu ya Afrika kulala 4-0 nyumbani na kwenda kushinda ugenini 5-0.
  • Goli la pili- mabao matano ya Simba yalifungwa na wachezaji wawili tu, Thuwen Ally matatu na George “Best” Kulagwa mawili.
  • Goli la tatu- Mchezaji Willy Mwaijibe, ambaye hakuwa akicheza kwa muda mrefu alicheza vizuri mno mechi hiyo kama kuaga kwani baada ya hapo hakucheza tena mpaka alipofariki dunia mwaka 1991.
  • Goli la nne- Kocha wa Simba aliyefanikisha ushindi huo ni mpenzi mkubwa na mwanachama mtiifu wa Yanga, Joel Nkaya Bendera ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
  •  Goli la tano- Rais wa Zambia wa wakati huo, Kenneth Kaunda alikuwepo uwanjani akishuhudia vijana wake wakiadhirika.
Baadaye, Simba ikapambana na Racca Rovers ya Nigeria na kutupwa nje ya mashindano kwa jumla ya mabao 2-0 baadaya ya kufungwa 2-0 kwenye pambano la ugenini lililofuatia lile la suluhu la Dar es Salaam. Kwenye pambano la hapa, beki chipukizi wa Simba, Hussein Tindwa, alianguka uwanjani na kufariki dunia kabla hajafikishwa hospitalini Muhimbili kwa tatizo la kubana pumzi lililokuwa la kawaida kwa mchezaji huyo kwa waliomfahamu.
Mwaka 1979 Simba wanafanya maajabu nchini Zambia kwa kupindua kipigo cha 4-0 nyumbani kwa kipigo cha 5-0 nchini Zambia na halafu mwaka huo huo timu yetu ya Taifa, baada ya ushindi wa nyumbani wa bao 1-0 la Mohammed “Adolph” Rishard, tunapata sare nchini Zambia ya 1-1 kwa bao la kusawazisha la Peter Tino, mbele ya Rais Kaunda tena, na kukata tiketi ya fainali ya mataifa (huru) ya Afrika nchini Nigeria.
Hiyo ndiyo soka ya ukweli ya miaka hiyo iliyojaa kila aina ya weledi.Inaleta raha sana kuikumbuka soka hiyo ikiwa ni ishara isiyo na utata ya uongozi bora wa miaka hiyo wa nyanja na ngazi tofauti. Riadha, masumbwi, netiboli na michezo ya mtu mmoja mmoja vyote vilikuwa juu kipindi hicho, ikithibitishwa na medali pamoja na makombe tuliyokuwa tunapata.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version