Christmas ya mpira wa miguu imemaliza jana, Christmas ambayo itabaki kwenye vitabu vya kumbukumbu kama michuano ambayo Ufaransa walikuwa mabingwa wa kombe la dunia.
Tena kuna wino utapita na kukoleza kuwa aliyewahi kuwa nahodha wa zamani wa Ufaransa na kufanikiwa kuchukua kombe la dunia la mwaka 1998. Miaka 20 imepita akiwa kama kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps amefanikiwa tena kubeba kombe la dunia kama kocha.
Kocha ambaye ameongoza vipaji vingi, vipaji ambavyo vilimfikisha fainali ya Euro ya mwaka 2016. Vipaji ambavyo leo hii vinaongelewa kwa jicho tofauti.
Kuna macho yanajaribu kuvitazama vipaji hivi kwa kuimba jina la mtu mmoja. Ndipo hapo wimbo Kylan Mbappe unapokuwa maarufu kuliko wimbo wa mchezaji yoyote katika michuano hii.
Inawezekana uzito wa wimbo wa Kylan Mbappe umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kutolewa mapema kwa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi katika michuano hii.
Hakuwepo mtu mwenye haiba ya mauzo kwenye vyombo vingi vya habari. Nafsi zetu ziliamua kumchagua Kylan Mbappe kwa sababu alibaki kama mchezaji pekee mwenye haiba ya mauzo kwenye vyombo vingi vya habari duniani.
Haiba ambayo inaweza ikasababisha kumpa Ballon D’or mbele ya Luka Modric, kiungo ambaye ni mtayarishaji bora wa mpira miguu.
Utawaja wapiga gitaa bora duniani, ukawapa sifa kedekede, na kuwavika umahiri wote kana kwamba hakuna wapiga gitaa wengine duniani.
Ni kama ambavyo Mimi ninavyoiamini mikono ya Martha Argerich kama mpiga piano bora kuwahi kutokea duniani, basi Luka Modric atabaki kuwa Wolfgang Amadeus Mozart wa mpira wa miguu kwa sasa.
Kila ladha inayotoka katika miguu yake inatengeneza chakula kitamu na bora cha macho yote. Huchoki kumwangalia na hukinai kumtazama.
Muda wote akili yake inafikiria namna ambavyo anaweza kutengeneza wimbo bora kupitia miguu yake.
Miguu yake imejaa dhahabu yenye thamani kubwa duniani, lakini uso wake hauendani na thamani ya miguu yake.
Na hii ni kwa sababu hakuzaliwa na uso wa Waigizaji wa Hollywood. Utapenda kuitazama miguu yake tu kwa muda mrefu lakini utaangalia uso wake kwa muda mfupi.
Hakuna pesa nyingi kwenye uso wa Luka Modric. Inawezekana hata biashara yake haiwezi kuwa kubwa kama biashara ya Kylan Mbappe.
Hata wasichana wengi wanaweza wasitamani kuwa naye kimapenzi kwa sababu uzuri wa Luka Modric uliwekwa miguuni.
Sehemu ambayo ni mara chache sana kuiona tofauti na usoni. Na hapa ndipo tunapokuja kumwadhibu Luka Modric.
Tutaushusha ufalme wake kwa sababu hana uso wa biashara tena tutajitahidi kumhukumu kuwa miguu yake haifungi sana ndiyo maana hastahili taji.
Dunia iliwahi kumvika taji Fabio Cannavaro kwa sababu ya ukomavu wake wa miguu, tangu hapo tumejisahau kuwa kila mchezaji ana nafasi kubwa ya kuwa mchezaji bora wa dunia na kupewa Ballon D’or.
Kama ambavyo nafsi yangu inatamani kumuona golikipa akichukua Ballon D’or ndivyo hivo nafsi yangu ina shauku na tamaa ya kumuona Luka Modric akichukua Ballon D’or mwaka huu , lakini sitoshangaa sana kwa sababu siyo kila mfalme huvikwa taji.
Siyo jambo la kushangaa kutoona Luka Modric asipovikwa taji lolote mpaka, lakini Ufalme wake utabaki na alama kubwa sana.
Ufalme wa Daver Sucker hakuvikwa taji lakini alama zake tunazikumbuka kila uchwao. Dunia inaweza isimkumbuke Luka Modric kama mchezaji ambaye alifanikiwa kupewa Ballon D’or lakini itamkumbuka kama mchezaji aliyeibeba timu ambayo haikupewa nafasi ya kufika mbali ambako wengi hawakuwa wanategemea kama watafika.
Lakini miguu yake ilikuwa na nguvu katika kutengeneza ladha yenye nguvu imara iliyoifikisha Croatia katika hatua ya fainali. Leo hii vitabu vitaiandika Croatia kama timu ambayo iliwahi kufika fainali na itakoleza kuwa ilifanikiwa kutoa mchezaji bora wa mashindano, mchezaji ambaye wengi hawamuoni kwa jicho la upendeleo kwa sababu hakuzaliwa Hollywood.