Menu
in , , ,

Lucas Moura amevurugwa Brazil, PSG

KUNA mawinga wachache sana kwenye dunia hii wenye uwezo wa kuchza soka kiwango cha juu. Kuna wachezaji waliojaliwa kucheza nafasi tofauti bila kujali uwezo wao wa kucheza nafasi nyingine.

Kuna mawinga wazuri katika kikosi cha timu yoyote. Zamani Said Maulid alitumiwa na Marcio Maximo alipokuwa akiinoa Taifa Stars.

Baada ya nyakati zake kupita, akaja Mrisho Ngassa ambaye sasa anasaidia majukumu hayo na Simon Msuva. 

Ukimwondoa Msuva utakutana na aina nyingine tofauti kabisa ya soka kutoka kwa Mcha Hamisi Mcha au aliyewahi kupewa nafasi, Edward Christopher.

Mawinga hawa wanacheza kwa kasi mno na wanatukumbusha zama za akina Akida Makunda.  Lakini kwa Brazil kuna winga mmoja mwenye aina ya soka la mastaa wetu, Lucas Moura.

Luiz Felipe Scolari alimwacha Moura kwenye kikosi cha Kombe la Dunia. 
Carlos Dunga naye amemwacha winga huyo kwenye kikosi kipya alichokiongoza kwenye mechi za kirafiki.

Kingine ni kwamba Carlos Dunga amemteua Neymar Junior da Silva kuwa nahodha wa muda wa kikosi cha Brazil. 

Kilichonishangaza kwenye uteuzi huu ni kwamba kinda huyo bado sioni kama amepevuka kuwa kapteni wa timu, lakini uamuzi wa Dunga unatakiwa kuheshimiwa. 

Ukiachana na hilo kuna jingine lililonipa mshangao; vijana watatu sasa wanakuja vizuri na wamekuwa mastaa zaidi kwenye kikosi cha Brazil.

Wawili ni mastaa wa kweli, lakini mmoja amekuwa hapewi sifa ingawa anacheza kwa soka la aina yake. 
Kuna Oscar dos Santos na Neymar Junior.

Halafu kuna Danilo ambaye amerudi kikosi cha Brazil baada ya kupotea kwa muda. 

Aliyekuwa kocha wa Brazil, Mano Menezes alifanikiwa kumpa nafasi Danilo mara kadhaa lakini hakuwa chaguo la kwanza.
Dunga amerejesha baadhi ya wanasoka wanaocheza Brazil na safu ya ushambuliaji amemleta Tardeli.
 
Nyuma amewaongeza Gil na Felipe Luis. Kwenye kiungo amemwongeza Philipe Coutinho kutoka Liverpool.

Lakini wote hao hawajawahi kuwa mastaa kama Lucas Moura. Alex Ferguson alipambana kutaka kumsajili Lucas Moura lakini alizidiwa kete na matajiri wa PSG ambao walimwaga fedha za kutosha kwa klabu ya Sao Paulo iliyomruhusu kwenda Ufaransa.

Kwa Wabrazil, PSG ina historia nzuri kwao kwani Ronaldinho Gaucho mtaalamu wa soka alicheza kwenye timu hiyo. 
Lucas Moura alikuwa staa wa kweli kwenye kikosi cha vijana cha Brazil kilichojumuisha Neymar Junior na Oscar.

Moura akiwa na miaka 19 akapandishwa kuichezea timu ya wakubwa na kuwaacha Oscar na Neymar wakiendelea kupanda kwa hatua za kutoka timu chini ya miaka 17 kisha 20 na 23 hadi kikosi cha wakubwa.

Lucas Moura aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini kwa vijana chini ya miaka 19 mwaka 2011. 
Umahiri wa Moura na mategemeo makubwa ya Wabrazil vilimfanya aonekane kuwa tegemeo kubwa mbele ya Neymar.

Kwa hiyo kwenye kikosi cha vijana Lucas Moura alikuwa staa. Lakini sasa hivi kila nikitazama Ligi ya Ufaransa najiuliza swali moja; kulikoni Lucas Moura? Nini kimemkuta nyota huyo? Amevurugwa na nini?
Kiufundi Lucas Moura ni mchezaji mwenye msaada mkubwa kwa timu akicheza wingi ya kulia au kushoto. Kasi yake na chenga vinamfanya awe winga hatari zaidi kwa timu pinzani.

Chelsea wanakumbuka hilo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya walipocheza na PSG. Kwamba Moura ni winga ambaye anaweza kuivuta safu nzima ya ulinzi na akaipenya na kutengeneza mabao mazuri.

Moura si mfungaji mzuri, lakini ni mtengenezaji mzuri mno na ana vitu vyenye kumvutia kocha. Tatizo lake kubwa kama ilivyo kwa mawinga Simon Msuva, Mrisho Ngassa na Said Maulid, ilikuwa kucheza nje ya timu.

Kuna wakati timu inamhitaji Moura kama mchezaji wa kitimu. Lakini anaweza kucheza mpira kibinafsi akiwa nje ya nafasi.

Kuna wakati anaweza kupoteza uelewano na timu pale anapohitajika aichezeshe timu kutokea wingi ya kulia au anapokuwa na mpira. Kila nikimtazama kinda huyo, namwona kama alichakachuliwa. Amevurugwa!
Kwamba aliwahishwa kupandishwa timu ya wakubwa bila kupata maendeleo mazuri tofauti na walivyo Neymar na Oscar waliopandishwa taratibu.

Edward Christopher alipokuwa Simba naye aliteuliwa kuwa kikosi cha Taifa Stars, lakini kukosa maendeleo mazuri klabuni kukamfanya apoteze namba.

Lakini tatizo halikuwa yeye, bali kuchakachuliwa kutokana na  makocha kuvutiwa na uwezo wake bila kujenga msingi wa maendeleo ya kipaji chake. Na hilo linamtokea Lucas Moura pale PSG na timu ya taifa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version