*Di Canio kumrithi O’Neill Sunderland?
Wakati Liverpool wameendelea mbio zao kutafuta nafasi za uwakilishi mashindano ya kimataifa, Aston Villa inaelekea pabaya.
Licha ya kucheza nyumbani Villa Park, kupata nafasi nyingi na kutangulia kufunga, Villa waliishia kufungwa mabao 2-1.
Kocha Paul Lambert wa Villa alikuwa akihaha kuwaelekeza wachezaji wake ili kuokoa jahazi, yasije yakamfika ya wajina wake – kocha wa Sunderland, Martin O’Neill aliyefutwa kazi jioni ya Jumamosi.
Liverpool walikwenda mapumziko vichwa chini wakiwa nyuma kwa bao moja lililofungwa na Christian Benteke dakika ya 31 baada ya kunasa mpira uliotoka mguuni mwa mwenzake, Gabriel Agbonlaho.
Kama walivyomalizia robo saa ya kipindi cha kwanza kwa kulishambulia kama nyuki lango la Villa, vijana wa Brendan Rodgers waliingia kipindi cha pili na tamaa hiyo hiyo.
Haikuwachukua muda mrefu kufanikiwa, kwani dakika ya 47 tu, Jordan Henderson alicheka na nyavu, akimwacha kipa Brad Guzan aliyeokoa michomo mingi kabla ya hapo akiwa hana la kufanya.
Mpachika mabao anayeongoza Ligi Kuu ya England (EPL), Luis Suarez alikosa mabao mengi, lakini aliipatia timu yake penati baada ya kuangushwa akienda kumsalimu Guzan.
Nahodha wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Steven Gerrard aliandika bao kwa mkwaju wa penati hiyo, bao lililodumu kuwa la ushindi.
Benteke aliunganisha nyavuni mpira katika dakika za majeruhi kuokoa pointi moja muhimu, lakini kibendera kilishanyooshwa juu, hivyo Lambert akaondoka kwa masikitiko makubwa uwanjani.
Gerrard alikuwa nyota wa mchezo, ambapo licha ya kufunga penati, kusukuma mashambulizi na kumiliki kiungo, aliokoa mpira kwenye mstari kwa kichwa, baada ya Benteke kupiga kichwa safi, kipa Pepe Reina akiwa ameshatoka golini.
Matokeo hayo yanaweka Liverpool nafasi ya saba, wakiwania nafasi za juu zaidi ili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya au Ligi ya Europa waliyoshiriki msimu huu na kutolewa kwenye mzunguko uliopita.
Villa wanabaki na pointi zao 31, wakishika nafasi ya 18; juu ya wapo Wigan wenye pointi 30 na Sunderland wenye 31 na chini yao kuna Queen Park Rangers wenye pointi 23 na Reading wanakokota mkia kwa pointi hizo hizo, lakini wana uwiano mbaya wa mabao, ambao ni -25.
Paolo Di Canio ateta na Sunderland
Saa chache baada ya kufukuzwa kazi kocha wa Sunderland, O’Neill, kocha aliyejiuzulu Swindon, Paolo Di Canio anapewa nafasi kubwa kumrithi.
Baada ya mazungumzo na mmiliki wa klabu hiyo, Mmarekani Ellis Short akiwa jijini London, Mtaliano huyo anadaiwa kutinga makao makuu ya klabu, kaskazini mashariki mwa England.
Short amekasirishwa na mwenendo wa klabu yake hiyo ambayo haijashinda katika mechi nane mfululizo, na kubaki pointi moja tu kuanguka kwenye eneo la kushuka daraja.
Di Canio (44) anajulikana kwa karisma yake kwenye soka, na mpango wa kumchukua ukikamilika, atawaongoza Sunderland kumenyana na Chelsea Stamford Bridge Jumamosi ijayo, kabla ya mechi na watani wao wa Tyne-Wear, Newcastle United katika dimba la St James’s Park.
O’Neill alifukuzwa kibarua saa chache tu baada ya kufungwa bao 0-1 na Manchester United katika dimba la Old Trafford, matokeo yaliyotarajiwa, hata hivyo.