Liverpool wawakatalia Chelsea
WAKATI Manchester City wakifurahia ushindi wa tabu dhidi ya Tottenham Hotspur, Liverpool wameridhika na sare dhidi ya Chelsea.
City walikuwa nyuma, lakini Sergio Aguero alisawazisha dakika ya 65 kabla ya Edin Dzeko kufunga dakika ya 88 na City kutoka kushinda 2-1.
Spurs walioanza vyema chini ya kocha Andre Villas-Boas walipata bao la kuongoza kupitia kwa Steven Caulker dakika ya 21.
Kufungwa huko kumewapunguza morali, na wataingia Emirates mchana wa Jumamosi ijayo kuwakabili Arsenal kwa hadhari, wakiwazidi Gunners kwa pointi moja tu, wakishika nafasi ya saba.
Ama kwa upande wa City, ushindi umekuwa ahueni kubwa kwa kocha Roberto Mancini anayeandamwa kwa madai ya kuishiwa mbinu.
Kadhalika yamekuwapo madai kwamba anaivuruga timu kwa kuwabadilishia wachezaji mfumo. Kuvurunda kwao kwenye Ligi ya Mabingwa kumemfanya Mancini kujawa hasira na hata ikadaiwa palikuwapo uasi Etihad miongoni mwa wachezaji.
Hata hivyo, Dzeko ambaye amekuwa na kawaida ya kuanzishwa benchi hado mambo yanapoharibika aitwe kuokoa jahazi, ametuma ujumbe kwa Mancini.
Mserbia huyo asiyependa kuitwa ‘super sub’ alimwambia mtangazaji wa televisheni kwamba ujumbe wake kwa Mancini ni magoli yake tu.
Aliingia zikiwa zimebaki dakika pungufu ya tano. Hii si mara ya kwanza kuwaokoa City, na amekuwa akisema klabu haimwoneshi heshima anayostahili.
Kwa ushindi huo, City wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 25 nyuma ya Manchester United wenye pointi 27.
Katika mchezo mwingine muhimu Jumapili hii, Liverpool wanaoendelea na mapinduzi yao chini ya kocha Brendan Rodgers, wamefanikiwa kufikisha mechi sita za ligi bila kupoteza, licha ya kuingia Stamford Bridge kwa wasiwasi.
Alikuwa nahodha John Terry aliyerejea baada ya kufungiwa mechi nne za nyumbani aliyefunga bao kwa kichwa kutokana na kona na Juan Mata dakika ya 20 ya mchezo.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana ni mapumziko mengine ya muda, Terry alilazimika kutoka nje dakika 15 tu baadaye, kutokana na kuumia goti alipogongana na mshambuliaji hatari wa Liverpool, Luis Suarez.
Ni Suarez huyo huyo aliyekuja kuwakomboa Liverpool kwa kupachika bao la kusawazisha dakika ya 73, kutokana na kazi nzuri ya Jamie Carragher baada ya kona iliyochongwa na Suso (Jesús Joaquín Fernández Sáenz de la Torre).
Liverpool walitawala zaidi nusu ya kwanza ya mchezo, lakini iliwawia ngumu kufyatua makombora langoni mwa Chelsea.
Licha ya sare hiyo kuwaacha Liverpool nafasi ya 13, ugumu wa timu waliyocheza nayo ugenini ni dhihirisho kwamba kikosi kinajengeka vyema kadiri siku zinavyokwenda. Chelsea wanashika nafasi ya tatu kwa pointi 24.
Newcastle United wenye kawaida ya kuchanua vizuri kitaifa na kwenye Michuano ya Europa, wameshikishwa adabu nyumbani na West Ham United.
Newcastle walishindwa kuhimili vishindo vya vijana wa Sam Allardyce, wakishindwa kukomboa bao la dakika ya 37 la mchezaji wao wa zamani, Kevin Nolan.
West Ham imechupa hadi nafasi muhimu ya sita, ambapo jitihada zote za Newcastle kusawazisha ziliishia ama mikononi mwa golikipa Jussi Jaaskelainen au kutoka nje ya lango.
Newcastle wanabaki nafasi ya 10 wanapojiandaa kuwavaa Swansea City wikiendi ijayo.