*Arsenal wawazabua Everton
Liverpool wamewaharibia Manchester City mbio za kutetea ubingwa wao, baada ya kuwafunga mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL) dimbani Anfield.
Liver waliojivuta hadi nafasi ya tano na kuwasababishia City wabaki nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi tano huku vinara wakiwa na mchezo mmoja mkononi walionesha nia ya ushindi mapema.
Alikuwa Jordan Henderson aliyecheka na nyavu mapema dakika ya 11 lakini City wakachomoa dakika 14 baadaye kwa bao la Edin Dzeko. City walizidiwa dakika ya 75 pale Philippe Coutinho alipofunga bao la ushindi.
Liverpool walioanza ligi kwa kusuasua wakifungwa mechi nyingi, hawajapoteza mchezo kwenye EPL tangu mwaka huu uanze, jambo ambalo ni faraja kwa kocha Brendan Rodgers aliyekuwa keshatishiwa kufutwa kazi.
Vijana wa Manuel Pellegrini wamebaki na historia ya kutopata ushindi Anfield tangu Mei 2003.
Katika mashindano kama haya mwaka jana, Liverpool waliwafunga City 2-1 pia, wakafukuzana kwenye ubingwa lakini hatimaye ni City waliotwaa taji.
Pellegrini alieleza umumuhimu wa mechi hiyo kabla, akisema ni ili kuendeleza mpambano wa ubingwa, lakini vijana wake wakashindwa kuonesha vitu uwanjani.
Liverpool wanaonekana kuwa na mwenendo mzuri na si ajabu wakapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao kwani wamevuna pointi 26 kutoka 30 ambazo wangeweza kupata kwenye mechi 10 zilizopita.
Waliwasili Ijumaa nyumbani baada ya kutolewa na Besiktas kwa mikwaju ya penati kwenye Ligi ya Europa lakini wakaonesha kiwango uwanjani.
ARSENAL WAWAZIDI KETE EVERTON
Arsenal wamepata ushindi mzuri dhidi ya Everton, ukiwa ni wa tatu mfululizo katika EPL, kwa mabao ya Olivier Giroud na Thomas Rosiscy aliyetokea benchi dakika ya 82.
Kwa ushindi huo, wamechupa hadi nafasi ya tatu wakiwashusha Manchester United. Wenger alimchezesha Giroud licha ya kutofanya vyema kwenye mechi ya UCL dhidi ya Monaco walipoambulia kipigo cha 3-1.
Giroud alifunga kwa jitihada kubwa kutokana na mpira wa kona wa Mesut Ozil, akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Everton.
Everton walifanya jitihada za kupata mabao, hasa kupitia kwa Romelu Lukaku lakini yote yaliishia kwa mabeki wa Arsenal kusafisha au kwa kipa David Ospina.
Beki mpya wa kati kutoka Villarreal, Gabriel Paulista alianza mechi kwa mara ya kwanza kwenye EPL badala ya nahodha msaidizi Per Mertesacker na uchaguzi huo wa kocha Arsene Wenger ulionesha mafanikio.
Awali Paulista alishindwa kufanya uamuzi vyema hadi Lukaku akamfikia Ospina aliyeokoa, lakini washabiki wa nyumbani walimshangilia sana alipomkabili mapema Mbelgiji huyo aliyetishia kuichana ngome ya Arsenal.