Liverpool wawachapa Newcastle
Liverpool wamejirekebisha zaidi na kufika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya kuwafunga Newcastle 2-0.
Raheem Sterling anayesuasua kusaini mkataba mpya alifunga bao la kwanza mapema dakika ya tisa na la pili likafungwa na Joe Allen.
Ufungaji huo umewafanya Liverpool kuwa na wafungaji 18 tofauti msimu huu.
Sterling aliyekataa kujadili mkataba mpya ambao angepata mshahara wa pauni 100,000 kwa wiki, ameingia kwenye tatizo jingine kwa kupigwa picha akivuta gesi aina ya nitrous oxide sebuleni mwake.
Tayari kocha wake, Brendan Rodgers amesema licha ya kwamba ni halali kisheria kuitumia, hadhani kwamba mwanasoka wa kulipwa anatakiwa kuivuta na kwamba atateta naye juu ya hilo.
Newcastle kwa kupoteza mchezo huo wameweka rekodi ya kufungwa mechi tano mfululizo, lakini Newcastle wataona wameonewa kwa kunyimwa penati ya wazi na pia mchezaji wao Moussa Sissoko alitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na rafu mbili alizofanya dhidi ya Lucas Leiva ambaye, hata hivyo, hakuumia.
Liverpool wamefikisha pointi 57 nyuma ya Manchester City wenye 61, Manchester United 65, Arsenal 66 na Chelsea 73.
Southampton wanashika nafasi ya sita wakiwa na pointi 56, Tottenham Hotspur wakiwa was aba na pointi 54, Swansea wana 47, West Ham 43 na Stoke wanafunga 10 bora kwa pointi 43.
Mkiani wamebaki Leicester wenye pointi 25, Burnley 26 sawa na QPR.