Simba Sports Club 3 Dar Young Africans 1
*Man City, Man U, Newcastle washinda
Kaimu Nahodha wa Liverpool, Luis Suarez amewaongoza wenzake kuwaadhibu Cardiff kwa 3-1 na kushika uongozi wa ligi. Kwa pointi 36.
Akiwa ndio kwanza ametoka kusaini mkataba mpya wa muda mrefu katika klabu hiyo aliyokuwa akitaka kuikimbia hvi karibuni, Suarez alifungua kitabu cha mabao kabla ya Raheem Sterling kufunga la pili na Suarez kufunga la tatu.
Wekundu hao wanaofundishwa na Brendan Rodgers walifurahia kiasi mchezo huo wa nyumbai japokuwa hawakupata karamu ya mabao waliyotarajia, kwa kukabwa na vijana wa Malky Mackay anayeshinikizwa kujiuzulu na mmiliki Vincent Tan. Cardiff walipata bao lao kupitia kwa Jordon Mutch.
Ushindi huo umewavusha kwa pointi mbili juu ya Arsenal walioongoza kwa muda, japokuwa wana mchezo mmoja mkononi, ambapo wanapepetana na Chelsea Jumapili hii.
Kwingineko Manchester City walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Fulham na kushika nafasi ya pili wakiwa sawa kwa pointi na Arsenal – 35 lakini wana uwiano mzuri wa mabao.
Walitikisa nyavu kupitia kwa kiungo Yaya Touré, beki wa kati Vincent Kompany, kiungo James Milner na mshambuliaji Jesús Navas huku Fulham wakipatiwa mabao yao na Richardson na Nahodha wa Man City, Kompany kujifunga mwenyewe.
Manchester United nao walipata ushindi dhidi ya West Ham wa mabao 3-1. Danny Welbeck alifunga bao la kwanza msimu huu Old Trafford na kinda Adnan Januzaj akaweka jingine kabla ya Ashley Young kupachika la tatu. Bao la kufutia machozi la West Ham lilifungwa na Carlton Cole.
Welbeck hakuwa amepata kufunga katika uwanja huo wa nyumbani tangu Oktoba 20 mwaka jana. Hata hivyo, alionekana kuumia goti na kutoka nje akichechemea na kuwaoa Man U hofu, kwani tayari Robin van Persie na Wayne Rooney wanauguza majeraha.
Matokeo mengine yalishuhudia Newcastle wakiwasasambua Crystal Palace 3-0, Stoke wakiwapiga Aston Villa 2-1, Sunderland na Norwich wakienda suluhu wakati West Bromwich Albion wakienda sare ya 1-1 na Hull.