Liverpool wamepoteza mechi ya fainali ya Kombe la Europa baada ya
‘kukatika’ kwenye kipindi cha pili na kuwaruhusu Sevilla wa Hispania
kufunga mabao matatu na kutetea ubingwa huo kwa mara ya tatu.
Awali, vijana wa Jurgen Klopp walionekana wangefanikisha ndoto za
kutwaa kombe hilo ili msimu ujao waingie kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya
(UCL), ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika walikuwa mbele kwa
bao la Daniel Sturridge.
Hata hivyo, kazi yao nzuri waliyoianza jijini Basel, Uswisi ilianza
kuharibiwa na Sevilla sekunde 17 tu za kipindi cha pili kwa Kevin
Gameiro kuiingiza kimiani majalo ya Mariano Ferreira.
Liverpool ambao kocha wao amepoteza fainali nyingine nne kama hizi,
walifungwa bao la pili na la tatu kupitia kwa mchezaji Andújar Moreno
na kuimaliza ndoto yao. Walitarajia kuingia UCL hivyo kuvutia
wachezaji wa kiwango cha juu kwa msimu ujao.
Kwa matokeo hayo, Manchester City wameondokana na hofu kwamba
wangeondolewa kwenye UCL ili kuwapisha Liverpool, kwani City wanashika
nafasi ya nne. Watatakiwa, hata hivyo, kuingia kwa kucheza kwanza
hatua ya mtoano mechi moja nyumbani na nyingine ugenini dhidi ya timu
watakayopangiwa.
Leicester, Arsenal na Tottenham Hotspur wanaingia moja kwa moja kwenye
UCL kutokana na kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu kwa mtiririko
huo wakati Manchester United na Southampton watakuwa na kibarua kigumu
cha Ligi ya Europa inayojumuisha mechi nyingi na safari ndefu za
kuchosha.