Ilikuwa Barcelona wamuuze Alexis Sanchez kwa Liverpool kwa sababu walitoa kitita kizuri kuliko Arsenal, lakini raia huyo wa Chile alikataa kwenda Merseyside.
Liverpool walishatenga pauni milioni tatu zaidi ya Arsenal, hivyo wakawa na uhakika wa kumpata azibe pengo la Luis Suarez waliyemuuza Barcelona, lakini Sanchez akasisitiza kwamba anataka kuwa na Arsene Wenger.
Sanchez alisajiliwa majira ya kiangazi kutoka Barcelona kwa pauni milioni 32 hivi wakati Liverpool walikuwa tayari kutoa pauni milioni 35 au pungufu kidogo ya hapo.
Hata hivyo, Barca nao hawakuonekana kutoa shinikizo kwake, ikizingatiwa pia Arsenal walikuwa wamewauzia beki wa kati na nahodha wao, Thomas Vermaelen aliyekuwa anataka kwenda Manchester United. Arsenal pia waliwauzia viungo Alex Song na Cesc Fabregas miaka iliyopita.
Sanchez (25) ameshapachika mabao 10 katika mechi 15 alizopiga akiwa na Arsenal na aliondoka Barca kwa sababu hakuwa akipata muda wa kutosha wa kucheza. Amekuwa akicheza vyema na Danny Welbeck aliyesajiliwa kutoka Man United.
Tangu ahamie Arsenal, Sanchez ametokea kuwa kipendi cha washabiki wakati Liverpool walimpata Mario Balotelli ambaye ameshindwa kucheka na nyavu, akicheza namba tisa.