*Man City, United, wapata ushindi
Liverpool walikuwa wenye furaha jioni ya Jumamosi hii baada ya kupata ushindi muhimu dhidi ya Crystal Palace na kukamata usukani wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Washambuliaji wa vijana hao wa Brendan Rodgers, Luis Suarez na Daniel Sturridge walitikisa nyavu mapema, na kuweka mazingira ya kutokea karamu ya mabao.
Hata hivyo, vijana wa Ian Holloway waligangamala lakini waliachia bao moja zaidi kwa njia ya penati iliyofungwa na nahodha wa Redds, Steven Gerrrad kabla ya kupata bao la kufutia machozi.
Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Suarez katika uwanja wa nyumbani wa Anfield tangu alipofungiwa Aprili, kwani alifungiwa mechi 10 kwa kumng’ata mchezaji wa Chelsea, Branislav Ivanovich.
Palace walipata faraja kwa bao la kichwa la Dwight Gayle, lakini waliwahakikishia Liverpool kubaki kileleni kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Arsenal wanaocheza na West Bromwich Albion Jumapili hii.
Crystal Palace wamebaki wa pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi, wakiwa na pointi tatu, mbili tu mbele ya Sunderland ambao nao walipoteza mechi ya Jumamosi hii.
Katika mechi nyingine, Manchester City walifanikiwa kuvunja mwiko wa Everton kutofungwa msimu huu, baada ya kuwachapa mabao 3-1 kwenye uwanja wa Etihad.
Mabao ya City yalifungwa na Alvaro Negredo, Sergio Aguero na Howard alijifunga mwenyewe wakati Romelu Lukaku ndiye alitangulia kuwafungia Everton bao mapema kipindi cha kwanza.
City walifarijika kwa sababu ndio walikuwa wametoka kuchakazwa na Bayern Munich 3-1 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwanzoni mwa wiki.
Lukaku aliye kwa mkopo Everton kutoka Chelsea, ameshafunga mabao saba katika mechi sita tu za EPL, akiwa amecheza jumla ya dakika 302 tu, kumaanisha ni bao moja katika kila dakika 43 alizokuwa uwanjani.
Bao lake lilikuwa la kwanza kwa City kukubali msimu huu katika kipindi cha kwanza, lakini matokeo hayo yamewafikisha Man City nafasi ya pili nyuma ya Arsenal na Everton ya tano nyuma ya Tottenham Hotspur.
Katika mechi nyingine, Manchester United walifanikiwa kukomboa bao walilotangulia kufungwa nyumbani kwa Sunderland na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Hata hivyo, ushindi wa United haukuja kirahisi wala haukupitia kwa washambuliaji wala wachezaji wake mahiri, bali kwa kijana Adnan Januzaj aliyemfichia aibu kocha wake, David Moyes.
Sunderland walipachika bao la mapema kupitia kwa Craig Gardner na kumweka Moyes na wachezaji wake roho juu hadi kijana huyo alipowaokoa baada ya nusu ya kwanza.
United angeweza kulia zaidi kama si jitihada za kipa wao, David De Gea dhidi ya kazi nzuri ya Emanuele Giaccherini aliyeelekeza mpira wa kichwa kimiani, muda mfupi kabla Januzaj (18) kupata bao lake la kwanza katika EPL.
Machester wamefanikiwa kupanda kidogo hadi nafasi ya tisa wakati Sunderland wamebaki mkiani kwa pointi yao moja tu.
Matokeo mengine yalishuhudia Newcastle wakipata ushindi mgumu wa mabao 2-1 dhidi ya Cardiff, Fulham wakiwafunga Stoke 1-0 na Hull wakienda suluhu na Aston Villa.
Norwich wanawakaribisha Chelsea, Southampton ni wenyeji wa Swansea, West Ham wanakuwa wageni wa Spurs wakati Arsenal wanasafiri hadi West Bromwich Albion kwa mechi za kukamilisha mzunguko wa saba.