Menu
in , ,

Liverpool wachangamkia usajili

*Man United waelekea kumkosa Alves
*De Bruyn Man City, Remy ‘out’ Chelsea?

Liverpool wameanza kiangazi kwa kasi za usajili, ambapo baada ya kumsajili kiungo aliyemaliza muda wake Manchester City, James Milner wamemgeukia Danny Ings.

Liverpool wamefanikiwa kumshawishi mshambuliaji wa kati Ings ajiunge nao kutoka Burnley walioshuka daraja msimu huu na mwenyewe anamaliza mkataba wake.

Ings (23) aliye Timu ya Taifa ya England anatarajiwa kuwasili Anfield kuanzia Julai mosi iwapo atafaulu vipimo vya afya.

Hata hivyo, kuna utata juu ya ada wanayotakiwa kuwalipa Burnley kwa Kanuni ya Bosman kwani Ings ni mchezaji chini ya umri wa miaka 24.

Baadhi ya washabiki wa Liverpool walioonekana wakimzomea Raheem Sterling anayekataa kutia saini mkataba mpya, wameeleza kutaka majina makubwa zaidi na si aina ya Milner na Ings tu.

Manchester United wanaelekea kukata tamaa ya kumsajili beki wa kulia wa Barcelona, Dani Alves (32) aliyeashiria kwamba angefurahia kujiunga na AC Milan wa Italia.

United wanataka kukabiliana na Chelsea kupata saini ya kiungo wa Lazio, Felipe Anderson (22) ambaye watakaomnunua huenda wakalazimika kukamua pauni milioni 30.

Golikipa wa Tottenham Hotspur, Hugo Lloris (28) anasema tetesi za kwamba mazungumzo juu ya yeye kujiunga na Manchester United ni porojo za kuokota mitaani tu.

Manchester City wanajiandaa kutoa pauni milioni 40kumnasa kiungo wa Wolfsburg, Kevin De Bruyne (23) aliyeuzwa huko na Chelsea kwa madai ya kutokuwa na kiwango.

City pia wanatarajia kubisha hodi kwa nguvu Liverpool kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji Raheem Sterling (20), lengo lao likiwa kuongeza wachezaji wa ndani kukidbi kanuni, lakini pia kupata huduma za kijana huyu asiyewataka Liverpool.

Spurs wanataka kumsajili mshambuliaji wa Monaco, Anthony Martial (19) akitarajiwa kuwagharimu hadi pauni milioni 18.2.

Newcastle wanatarajiwa kukamilisha ajira ya kocha mpya, Steve McClaren atakayeanza na jukumu la awali la kutafuta wachezaji wa ndani kusajili kwa ajili ya msimu ujao.

Mshambuliaji wa kati wa Arsenal, Joel Campbell (22) anahusishwa na kujiunga na klabu ya kocha David Moyes nchini Hispania, Real Sociedad.

Swansea wanapigishana vikumbo na Crystal Palace na Southampton kumuwania mshambuliaji wa kati wa Chelsea, Loic Remy (28). Remy anataka kupata muda zaidi wa kucheza na si kuwa chaguo la pili kwenye ushambuliaji, hivyo angependa kuondoka Stamford Bridge.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version