*Ni katika mzunguko wa 3 Kombe la FA
*Arsenal na West Brom, Villa na Spurs
WAKATI homa zikipanda kwa mechi mbili za watani wa jadi wikiendi hii katika Ligi Kuu, ratiba inaonyesha Liverpool watakwaana tena na Manchester United mwezi ujao kwenye Kombe la FA.
Kihistoria, klabu hizo mbili ndio watani wa jadi nchini Uingereza, japokuwa utani wenyewe umepungua kiasi kutokana na kudorora kwa Liverpool miaka ya karibuni.
Hata hivyo, inasukwa upya chini ya Kocha Brendan Rodgers na walianza vyema Ligi Kuu kwa kugawa vichapo katika mechi mbili za mwanzo.
Wakati Liverpool wanakwaana na Manchester United kwenye mechi ya ligi kuu Jumapili hii, mahasimu wa kaskazini mwa London, Arsenal na Tottenham Hotspur wanakutana pia katika mechi inayotarajiwa kuwa ya kusisimua.
Spurs wameanza mechi zao mbili kwa ushindi mwembamba wakati Arsenal walianza kwa kipigo kutoka kwa Aston Villa kabla ya kumalizia hasira kwa Fulham.
Mashetani Wekundu la Liverpool watakapokutana Jumapili hii, Luis Suarez aliyezuiwa kucheza mechi 10 hatakuwapo, lakini ikiwa atabaki Liverpool, atakipiga kwenye mechi ya Kombe la FA (Capital One).
Kombe la Ligi na Kombe la FA ni mataji ambayo yanaweza kuziliwaza timu zinazoshindwa kutwaa ubingwa wa England.
Hapo awali vigogo walikuwa wakiyapuuza na kuchezesha wachezaji yoso, lakini sasa wanachukulia kwa umuhimu mkubwa, japokuwa wamekuwa pia wakifungwa na timu za madaraja ya chini.
Suarez alipigwa marufuku kucheza baada ya kumng’ata mlinzi wa Chelsea, Branislav Ivanovic April mwaka huu na tayari amekosa mechi nne msimu uliopita.
Hata hivyo, amekuwa mtata, akitangaza kutaka kuondoka Anfield ili achezee klabu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Arsenal walitoa ofa ya pauni 40,000,001 iliyokataliwa na Liverpool.
Kwanza walidai hauzwi, baadaye wakadai fedha hizo ni kidogo na thamani yake ni zaidi ya pauni milioni 50, lakini kisha wakashikilia hatauzwa kwa bei yoyote.
Inaaminika kwamba Rodgers ameshamshawishi kubaki Anfield, kwani baada ya kumtenga na kumtaka afanye mazoezi mwenyewe, amemrejesha mazoezini na wenzake, na alisema awali hangemrejesha hadi waelewane na aombe radhi.
Suarez amepata kupigwa faini na kuzuiwa mechi pia kwa kumkashifu kibaguzi Nahodha Msaidizi wa Manchester United, Patrice Evra, ambapo hata baada ya kumaliza kifungo chake, alikataa kumpa mkono. Baadaye aliomba radhi.
Wakati Arsenal walikuwa wanataka kumchukua Suarez (26), baadhi ya wadau, wakiwamo wachezaji wa zamani walilalamika kwamba ni mzigo kutokana na matatizo aliyo nayo yasiyoisha, ikiwamo kukiri kujiangusha ili apate penati.
Manchester United wamepata kukwaana na Liverpool katika nyakati na mizunguko minne tofauti ya Kombe la FA, ambapo mwaka 1983 Liverpool waliwafunga Man U katika fainali Uwanja wa Wembley.
Liverpool pia waliwapa kipigo Mashetani Wekundu hao kwenye fainali ya mwaka 2003 katika Uwanja wa Millennium Cardiff.
Liverpool pia walishinda mechi nyingine ya mzunguko wa kawaida ya FA kwenye uwanja wao wa Anfield Novemba 1985, lakini Manchester walishinda katika mechi pekee ya FA waliyokutana Old Trafford mwaka 1990.
Timu nyingine za Ligi Kuu ya England zimepangwa pamoja, ambapo Aston Villa watawakaribisha Spurs; Arsenal watakuwa wageni wa West Bromwich Albion; West Ham United watakabiliana na Cardiff wakati Everton watacheza na Fulham.
Mabingwa watetezi, Swansea watasafiri hadi jijini Birmingham kucheza na Birmingham walio wanaocheza ngazi ya chini ya Championships.
Manchester City watakuwa wenyeji wa Wigan wakati timu ya League One ya Swindon itakuwa mwenyeji wa Chelsea.
Southampton watawakaribisha Bristol City wa League One’ katika Uwanja wa St Mary’s, wakati Leeds watasafiri kwenda kukabiliana na Newcastle nyumbani kwao.
Norwich watacheza na Watford kwenye dimba la Vicarage Road; Leicester watakabiliana na jirani zao, Derby huku Hull City wakiwakaribisha mahasimu wao wa jiji la Yorkshire, Huddersfield Town.
Katika mzunguko huo wa tatu, Peterborough wataenda kukipiga na Sunderland, Tranmere watawakaribisha Stoke, huku Nottingham Forest wakikutana na Burnley.