*Southampton, Newcastle sare
Liverpool wameanza msimu vyema baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stoke.
Pamoja na kwamba walisubiri hadi dakika ya 86 kupata bao hilo, ni ushindi unaowapa moyo washabiki na kocha Brendan Rodgers baada ya kuwa na msimu uliopita uliokuwa mbaya.
Alikuwa ni Philippe Coutinho aliyefunga bao zuri kutoka mbali, baada ya pande mbili hizo kuwa zimetoshana nguvu hadi muda huo.
Nusura mchezaji wa zamani wa Liverpool, Glen Johnson aliyejiunga Stoke kama mchezaji huru afunge bao kipindi cha kwanza kama si shuti lake la yadi 12 kuokolewa.
Mkongwe Charlie Adam naye alikaribia kuweka mambo sawa kwa Stoke, lakini shuti lake la adhabu lilipanguliwa na kipa wa Liverpool, Simon Mignolet.
Itakumbukwa kwamba timu mbili hizi zilikutana siku ya mwisho ya msimu uliopita, ambapo Stoke waliwacharaza Liverpool 6-1, kikiwa ni kichapo kikubwa zaidi kwa Liver tangu 1963, na nusura Rodgers apoteze kibarua.
Wengi walikuwa wanamwangalia mshambuliaji mpya wa Liverpool, Christian Benteke lakini mara nyingi aliishia na mipira yake nje ya kasha la penati hivyo hakuwa na madhara.
Benteke alikuwa na mpira mara tano tu ndani ya eneo la penati na si ajabu akawa kama Mario Balotelli, hivyo atatakiwa kuongeza kiwango kwa sababu ana ushindani mkubwa kutoka kwa Roberto Firmino aliyeingia dakika ya 78 na kucheza vyema.
Kadhalika Liverpool wana ‘mashine’ nyingine katika idara ya ushambuliaji kama Danny Ings anayesubiri siku ya kucheza na Daniel Sturridge anayemalizia matibabu yake na huenda akaanza kucheza mwezi ujao.
Liver hawajajua vyema nani awe mtu wao muhimu katika ushambuliaji wa kati tangu walipomuuza Luis Suarez Barcelona na kisha kiangazi hiki kulazimika kukubali shinikizo na kumuuza Raheem Sterling kwa Manchester City.
Stoke hawakuwa wabaya sana, ambapo kocha Mark Hughes aliwajaribisha wachezaji wake wapya, Ibrahim Afellay na Marco van Ginkel waliowaongezea kiwango na huenda watakuwa wazuri kadiri muda unavyokwenda.
Katika mechi nyingine, Southampton walikwenda sare ya 2-2 na Newcastle, wakiashiria zama mpya za kocha Steve McClaren hapo Newcastle.
Shane Long aliwasawazishia Saints dakika 11 kabla ya mechi kumalizika wakati bao lao la kwanza lilitiwa kimiani na Graziano Pelle mapema dakika ya 24 baada ya kuukuta mpira mrefu wa Cedric Soares.
Mabao ya Newcastle yalifungwa na Papiss Cisse dakika ya 42 na mchezaji mpya aliyesajiliwa kwa pauni milioni 14.5, Georginio Wijnaldum dakika sita tu baadaye