*Man United, Spurs sare, Man City washinda
*Chelsea washinda baada ya kubanwa awali
Mzunguko wa 13 wa Ligi Kuu ya England umekamilika kwa kishindo, ambapo Liverpool waliokuwa wakichanja mbuga vyema wamepigwa pasipo kutarajia.
Liverpool walikuwa ugenini wakicheza na Hull City waliopanda daraja msimu huu tu na kuambulia kisago cha mabao 3-1.
Kocha Brendan Rodgers hakuamini mwenendo wa timu yake, ambayo ilianza kufungwa kabla ya kusawazisha kwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na nahodha Steven Gerrard.
Hata hivyo, Hull wakihamasishwa na maelfu ya washabiki wao walipata bao la pili na kisha beki wa Liverpool, Martin Skirtel akajifunga kwa kichwa akidhani anaokoa hatari, na kipa wake Simon Mignolet akienda upande mwingine wa goli na kuwa zahama kwa wageni hao.
SPURS, MAN UNITED WABANANA 2-2
Katika mechi ya kwanza Jumapili hii alasiri jijini London, Tottenham Hotspur walionekana kufufuka baada ya kichapo cha mabao 6-0 kutoka kwa Manchester City wiki iliyopita, ambapo walikabiliana na mabingwa watetezi, Manchester United.
Spurs walicheza vyema na hata kupata bao la kuongoza kupitia kwa Kyle Walker lakini Man U walisawazisha kwa mpira wa Wayne Rooney, Sandro akawafungia bao jingine lililofutwa tena na mkwaju wa penati wa Rooney na kufanya mchezo kumalizika kwa sare.
MANCHESTER CITY MBELE KWA MBELE
Vijana wa Manchester City wanaofundishwa na kocha raia wa Peru, Manuel Pellegrini wameendeleza mchakamchaka kwa wapinzani wao.
Jumapili hii waliwapiga Swansea kwa mabao – na kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi kwa kuwafunga Swansea 3-0.
Mabao ya washindi waliokuwa Etihad yalifungwa na Alvaro Negredo aliyefungua kitabu na Samir Nasri aliyebandika mawili.
CHELSEA WACHOMOA NA KUSHINDA
Chelsea walifanikiwa kupata pointi tatu muhimu kwa jasho, baada ya kutangulia kufungwa na Southampton katika uwanja wa Stamford Bridge.
Chelsea walikuwa nyuma kwa 1-0 hadi wakati wa mapumziko, bao lililofungwa sekunde ya 14 na Jay Rodriguez baada ya mchezaji wa Chelsea, Michael Essien kukosea katika kurudisha mpira kwa kipa wake Petr Cech.
Hata hivyo, kocha Jose Mourinho alitangulia kwenye vyumba vya kubadili nguo hivyo kwamba wachezaji walimkuta huko baada ya nusu ya kwanza, na waliporejea uwanjani waligangamala hadi kupata ushindi huo muhimu wa 3-1.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Garry Cahill 55, John Terry na Demba Ba.
Chelsea walicheza hovyo mechi iliyopita ambapo walifungwa na Basel ya Uswisi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo hata hivyo walishafuzu.
MSIMAMO WA LIGI KUU ENGLAND
Kwa matokeo ya wikiendi hii, Arsenal wanaendelea kuongoza kwa pointi zao 31 wakifuatiwa na Chelsea wenye pointi 27, Man City 25, Liverpool na Everton 24 kila moja.
Nafasi ya sita inashikwa na Newcastle wenye pointi 23 wakifuatiwa na 23, Southampton na Manchester United wana 22 kila moja, Spurs ni wa tisa kwa pointi 21 wakifuatiwa na Hull 17, Aston Villa 16, West Bromwich Albion na Swansea 15 kila moja.
Nafasi ya 14 inashikwa na Norwich wenye ponti 14 wakifuatiwa na West Ham, Stoke na Cardiff kila moja wakiwa wamejikusanyia pointi 13.
Nafasi ya 18 wapo Fulham wenye pointi 10, ya 19 Sunderland point inane na mkiani wapo Crystal Palace wenye pointi saba.