Menu
in , ,

Liverpool: Hivi ndivyo wanajisikia na maana ya mwaka huu kwao

Tanzania Sports


HATIMAYE Liverpool wameweka rekodi kwa kuchukua ubingwa wa Ulaya – UCL – Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Licha ya ukweli kwamba walifika katika fainali hizo wakipewa nafasi kubwa ya kuwashinda Tottenham Hotspur, wakiwa na kumbukumbu ya alama nyingi nyumbani bado Reds hao walijizatiti chini ya Mjerumani kocha wao, Jurgen Klopp.

Walihisi kwamba walikuwa wanatakiwa kuhakikisha kwamba ‘majembe’ yote yapo vyema kwa ajili ya kazi, wasije wakapewa aibu na Spurs wa kocha Mauricio Pochettino. Wamethibitisha kwamba ni timu kubwa Ulaya baada ya kuvuka vigingi vingi.

Kikubwa ambacho wengi waliona kingekuwa tabu kilikuwa Barcelona, lakini Liver wakapindua meza na pamoja na kukosa ubingwa wa nyumbani, Liverpool na washabiki wao wana kikubwa cha kujivunia – ubingwa wa Ulaya.

Sasa, hata hivyo wanayo kazi nyingine ya kujipanga upya kwa ligi inayotarajia kuanza Agosti mwaka huu – Ligi Kuu ya England (EPL). Kule Istanbul mwaka 2005, walikuwa ni Liverpool waliokubali kufungwa bao katika dakika ya kwanza tu.

Hata hivyo, jijini Madrid mwaka 2019, walikuwa ni Liverpool waliofanikiwa kupata bao katika dakika ya kwanza kwa mkwaju wa penati. Hata hivyo, mazingira ya Liver kushinda kwa mara ya tano na sita hayangeweza kuwa tofauti zaidi.

Miaka 14 iliyopita kikosi hicho chini ya kocha Rafa Benitez walikuwa wakichukuliwa kuwa timu ndogo sana na wasindikizaji katika Ulaya. Lakini walipokwenda Madrid Jumamosi, kikosi cha Klopp naweza kusema kwamba ndicho kilienda kikiwa bora zaidi Ulaya – walichotakiwa ni kuthibitisha kwa kuonesha mambo uwanjani. Walikuwa wakipewa nafasi kubwa na kimsingi walitakiwa kwenda kushinda, wakafanya hivyo.

Fainali ya pili ya UCL iliweka pwenti ya kuanzia kwa nini Liverpool walikuwa bora zaidi Ulaya, baada ya kuwa wamewafunga mabingwa wa Ufaransa, Ujerumani na Hispania njiani kuelekea Madrid kwa fainali hiyo.

Tangu walipofungwa kule Kiev, wamekuja kuweka rekodi ya klabu kuwa na lama nyingi zaidi kwa ujumla na sasa wameonesha ufanisi bora zaidi katika soka ya Ulaya. Wamekuwa timu wa kwanza kupindua matokeo ya kuwa chini kwa mabao matatu kwenye nusu fainali katika mechi ya mkondo wa pili na walifanya hivyo kwa Barcelona.

Waliwahi kushindwa kwenye fainali mbili na kwa hakika palikuwapo na shinikizo kubwa, japokuwa wachezaji hawakulionesha kivile wakati wakipasha misuli moto kwenye dimba la Wanda Metropolitano siku moja kabla ya gemu lenyewe. Walitulia, wakitabasamu lakini walipewa mazoezi ya nguvu chini ya kocha wa kikosi cha kwanza, Pepijn Lijnders.

Naweza kusema kwamba washabiki ndio walionekana wakiwa na hofu, walipowasili Madrid tayari kwa mtanange huo na wakati mechi ikianza, wakiwaza kwamba jamaa wa Spurs wangewea kuwaadhiri. Kwa jinsi walivyocheza, nafasi walizotengeneza na kukosa mabao, ingekuwa uchungu mkubwa kulikosa tena kombe hilo.

Hata hivyo, kwa washabiki waliokuwa wanafuatilia na kuona jinsi kikosi kilivyokuwa kikisukwa hatua kwa hatua chini ya Klopp ambaye daima huwa hajioneshi kuwa mwenye shinikizo, alijua kwamba mwaka huu wangekuwa na kitu kikubwa kama hicho, licha ya vikwazo nilivyovitaja awali.

Tangu kichapo kile cha Istanbul, Liver wamepokea vingine vinne kwenye fainali za UCL na katika kampeni za EPL wameishia katika nafasi ya pili mara tatu. Kocha alikuwa na mkakati wake kuhakikisha wanasonga mbele vyema. Kwa maneno ya Klopp ni kwamba Liver walitoka kwenye nafasi ya msichana asiyekuwa mrembo zaidi kijijini hadi kuwa ‘supermodel’.

Divock Origi alitokea kuwa shujaa asiyetarajiwa, Mbelgiji huyo akitundika mpira kwenye kamba sambamba na Mohammed Salah aliyezoeleka kiasi cha kuja kupata ushindi wa mabao mawili kwa bila na kuwaacha Spurs wakisikitika.

Mbegu za ushindi wa Liverpool zilisiwa muda mrefu kabisa kabla ya msimu uliomalizika na ulikuwa ni mchakato chini ya wamiliki wa klabu hiyo, Fenway Sports Group, wakiimarisha klabu kila msimu pasipokuwa na papara ya kubadili kocha, bali kuingiza wachezaji wazuri tena ghali kurejesha mapinduzi mekundu Anfield.

Baada ya heshima waliyojenga Madrid, wachezaji walionekana wakitokwa machozi ya furaha wakatiw ashabiki wao wanaokadiriwa kufika 750,000 kuwapokea waliporudi nyumbani Liverpool wakiwa mashujaa. Na hiyo tafsiri yake ni nini? Ndiyo nguvu ya Liverpool kwa sasa baada ya kupata msingi imara.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version