Imekuwa miaka 30 ya kusubiri ubingwa kwa Liverpool wanaoongoza kwa mbali kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Bahati mbaya ni kwamba wakati wamejihakikishia kuwa mabingwa wateule iwapo watashinda mechi chache zijazo, ligi imesimamishwa hadi wakati usiojulikana kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Wakati hayo yakiendelea, wadhamini Nike wamewaambia kwamba ni sawa kwamba wakamilishe msimu wa soka wa 2019/2020 wakiwa wamevaa jezi zenye nembo zao na kwamba watapata haki yao.
Nike wana mkataba mnono wa miaka mitano na Bodi ya Ligi Kuu ambao unatarajiwa kuanza Juni mosi mwaka huu. Kampuni hiyo ya Marekani inataka kuwasukuma Liverpool wanaofundishwa na Jurgen Klopp kuvaa jezi zao kwa mechi zote kuanzia tarehe hiyo husika.
Hii inamaanisha kwamba hueda katika tarehe itakayopangwa, ikiwa itatokea, basi nahodha Jordan Henderson atalinyanyua Kombe la EPL akiwa na jezi ya Nike badala ya zile za Standard Chattered.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba pamekuwapo mazungumzo baina ya Billy Hogan – Mkurugenzi Mtendaji wa Liverpool na Ofisa Biashara Mkuu – na wasambazaji wote, na huenda sasa ikawa ni makubaliano kwamba jezi mpya zianze kutumika kwenye msimu mpya ambao haujulikani utaanza lini, kwani mikusanyiko imezuiwa hadi baada ya Covid-19 kumalizika.
Ofisa mwandamizi wa Nike, akiwa chanzo kingine cha habari, anasema kwamba kisheria utekelezaji ungeweza kuanza katika msimu huu ambao huenda utaendelea baada ya Juni, kwani mkataba unaweka bayana kwamba unaanza Juni mosi. Hata hivyo, anasema hawataki kuingia kwenye malumbano, bali kukubaliana vyema kwa utulivu.
Ilikuwa makubaliano ya awali kwamba Liverpool waanze kuvaa jezi hizo kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya. Janga la ugonjwa huu limesababisha matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa michuano ya Euro 2020 ambayo sasa itafanyika mwakani huku hatma ya michuano ya Olimpiki ikiwa haijulikani.
Liverpool walishinda kesi Mahakama Kuu Oktoba mwaka jana, wakiwashiwa taa ya kijani kwa ajili ya kuingia kwenye mkataba na Nike. Dili lao lina thamani ya pauni milioni 30 kwa Liverpool kwa msimu mmoja. Kadhalika kuna asilimia 20 za mauzo
Mbalimbali na bonasi ya pauni milioni nne iwapo wangeshinda au kushika nafasi ya pili katika Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) ambako wameshatolewa lakini.
Kutokana na maendeleo yao uwanjani, Liverpool wanatarajia kwamba kwa mwaka mkataba unaweza kuwa na thamani ya kati ya pauni milioni 60 na milioni 70. Mkataba wa sasa ni pauni milioni 40 kwa mwaka.
Liverpool wanaendelea kushinikiza kupata ruhusa ya kuendeleza jukwa la upande wa Anfield Road lakini kuna utata wa kufanikiwa. Wafanyakazi wanaendelea kulifanyia kazi hilo wakiwa nyumbani na wanatarajiwa kuwasilisha kwenye Halmashauri ya Jiji la Liverpool Aprili mosi.
Maofisa wa klabu hiyo walisema mwezi jana kwamba mpango huo ni wa gharama ya pauni milioni 60 na kwamba utaongeza viti 7,000 uwanjani Anfield na kufikisha uwezo wa kuchukua washabiki 61,000 kwa ajili ya kuanza msimu wa 2022/2023.