*KWA KUSHINDA TAJI LA DHAHABU MARA YA TANO*
Mshindi wa taji la Balloon d’Or ( mpira wa dhahabu kwa Kifaransa) mwaka 2015 ni “mchawi” wa soka, Lionel Messi aliyepata kura 41.33. Messi ,kiungo na mshambuliaji wa timu ya Barcelona, alimpiku Cristiano Ronaldo ( kura 27.76), aliyeshika nafasi ya pili na mwenzake wa Barcelona, mshambuliaji Neymar Santos Junior (kura 7.86), wa tatu.
Ronaldo ambaye amesakamwa kuwa uchezaji wake umefifia karibuni aliwaambia wanahabari kuwa “ bado ana uwezo wa kucheza vizuri.” Tetesi zimeenezwa kuwa huenda akahamia St Paris Germain ya Ufaransa baada ya mwaka wa utata, Real Madrid.
Balloon d’Or ilianzishwa na gazeti la Kifaransa, France Football, mwaka 1956 ila kuunganishwa na la Mchezaji Bora Wa FIFA – mwaka 2010.
Lionel Messi alishinda tuzo hiyo mwaka 2009, 2010, 2011 na halafu 2008, 2013 na 2014 ikawsa zamu yake Cristiano Ronaldo. Kwa kushinda taji hilo Messi amekuwa mshindi mara tano na kuwapita wachezaji wengine wote. Tuzo hili lilipoanzishwa mwaka 1956 lilikabidhiwa mshambuliaji na mpiga chenga maarufu wa Uingereza, Stanley Mathews aliyestaafu akiwa na miaka 50 mwaka 1965. Stanley Mathews alichezea timu za Blackpool na Stoke, ambazo kwa leo si timu kubwa kama enzi zake alizpoziwezesha kushinda vikombe mbalimbali kama FA Cup ya England mwaka 1953.
Balloon d’Or hutolewa si tu kwa sababu za ufundi wa kucheza bali pia mchezaji kuiwezesha timu yake kushinda vikombe. Kura za ushindi hutoka kwa manahodha na makocha mbalimbali wa kimataifa. Haieleweki kama timu za Kiafrika zimehusika katika uchaguzi wa 2015.
Toka taji hilo lianze ni Mwafrika mmoja tu aliyezawadiwa. George Weah wa Liberia alishinda mwaka 1996 na yumo kati ya fungu la wachezaji 100 bora kuzidi wote ulimwenguni lililotayarishwa na FIFA kwa uchaguzi wa mfalme wa soka, Pele. Mchezaji mwingine wa Afrika ndani ya wastahiwa na mabingwa hawa 100, ni Roger Milla (Cameroon) aliyewika kombe la dunia miaka 25 iliyopita.
Wengine wanaomkaribia Messi ni Michel Platini na Zinedine Zidane, kocha wa sasa wa Real Madrid na kiungo- mshambualiaji na nahodha wa timu ya Ufaransa iliyoshinda kombe la dunia la 1998. Zidane (43), alitwaa taji hili lilipoitwa la FIFA mwaka 1998, 2002 na 2003. Michel Platini (60) ambaye karibuni amesikika katika kashfa ya kifisadi ya FIFA, alishinda taji la Balloon d’Or , 1983, 1984 na 1985.
Wachezaji wengine wastaafu na maarufu ni Kevin Keegan aliyekuwa kocha wa Uingereza (1999) na mchezaji wa Liverpool, Newcsatle na Hamburg ya Ujerumani miaka ya 1970. Keegan alitwaa Balloon d’Or m 1978 na 1979. Mchezaji, nahodha na kocha maarufu wa Ujerumani Franz Beckenbauer aliyekabidhiwa tuzo la 1972 na 1976. Pia, George Best (Manchester United na Ireland,1968), Eusobio (Ureno, 1965), Ruud Gullit (Uholanzi, 1987) na Alfredo Di Stefano (Real Madrid na Argentina, 1959).
Di Stefano aliyefariki mwaka juzi akiwa na umri wa miaka 88, anahesabika kama mmoja wa wachezaji bora kuzidi wote kutokana na ufundi wa kucheza nafasi yeyote uwanjani, iwe mbele au nyuma. Kama alivyokuwa Pele, Stefano alijaaliwa nguvu , kasi na chenga zilizobabaisha na kusaidia mabao mengi.
Lionel Messi lakini amewapiku wote.
Moja ya picha za Messi katika magazeti ya jana zinamwonesha kakaa na Ronaldo na Neymar, huku mkewe, Antonella Roccuzzo akimsalimia Cristiano Ronaldo.
Ingawa hawajaoana rasmi, Antonella ameshamzalia Messi watoto wawili wa kiume, Thiago na Mateo. Messi aliyezaliwa mwaka 1987 kitongoji cha kimaskini Argentina alikua kwa shida sana. Akiwa mtoto alisakamwa na maradhi yanayoathiri tezi ubongo na kumfanya mtoto asikue sawasawa.
Kilichomwokoa ni kipaji chake cha mpira ambapo timu ya Barcelona ilimdhamini akiwa na miaka 13 na kuahidi kulipia matibabu ili awasakatie kabumbu baadaye. Labda hilo ndilo linalomfanya Messi awaambie wanahabari na wasambaza tetesi wanaomtaka ahamie ligi ya England kuwa hatoki pale.
Messi alisema ataendelea kuichezea Barcelona hadi atakapostaafu. Zamani Pele hakuhama timu yake ya Santos hadi alipostaafu kwa kuhamia Marekani. Mwaka jana Steve Gerrard wa Liverpool naye alistaafu baada ya kukataa kuhama muda mrefu licha ya kuoneshwa mamilioni ya Chelsea iliyomtaka sana.