Nilibaguliwa kwa rangi yangu
Mmoja wa wachezaji maridadi waliowika kwenye kikosi cha Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia 1998 ni Lilian Thuram ambaye jina lake kamili ni Ruddy Lilian Thuram-Ulein.
Huyu ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwakilisha taifa hilo katika mechi nyingi zaidi, akiwa amecheza huko mechi 124 tangu 1994 hadi 2008. Anafurahia jinsi kulivyotokea usawa miongoni mwa weusi na weupe baada ya ushindi wa kikosi ambacho waliokuwa weusi ni wengi.
Lakini anaweka bayana katika kitabu chake kipya kwamba awali alikabiliwa na ubaguzi, ambapo wanafunzi wenzake darasani walimhukumu kwa rangi ya ngozi yake. Tangu ahame Guadeloupe alianza kukabiliwa na ubaguzi wa rangu.
Mwenendo aliokabiliana nao akiwa mvulana ulimtisha kiasi kwamba alipomaliza muda wake wa kucheza soka, aliamua kuelekeza nguvu zake kwenye vita dhidi ya ubaguzi wa rangi kama mwanaharakati.
Kwa zile wiki chache baada ya raha ya kutwaa Kombe la Dunia, Thuram alijawa faraja kubwa kuona jinsi watu wa Ufaransa walivyowatendea sawa wachezaji wote bila kujali rangi za ngozi au asili zao.
“Haikuwa marejeo tu kwa timu ya soka, ilikuwa kuhusu jamii yote. Mie ni mtu mwenye uzoefu wa mambo na najua kwamba nje ya soka watu hawachukuliwi sawa. Hawaruhusiwi kuota juu ya mambo kwa usawa. Kutegemeana na rangi ya ngozi au asili yako, huwezi kupata fursa sawa. Kwa hiyo ndiyo maana nina rah asana kwa sababu walau kwa muda kulikuwapo na kutambuliwa na kupewa sifa bila kujali rangi nyeusi au asili,” anasema.
Amefungua taasisi yake yenye makao makuu wilayani Odéon katikati ya Jiji la Paris, ikienda kwa jina la Fondation Lilian Thuram baada ya kuondoka kwenye klabu yake ya mwisho kuchezea – Barcelona mwaka 2008.
Lengo lake kubwa lilikuwa kuwaelimisha watoto na vijana juu ya mizizi ya ubaguzi wa rangi na kwa nini ni mbaya. Yeye ni mweusi lakini ameweka rekodi ya kuchezea timu ya taifa mara nyingi zaidi katika historia ya timu hiyo – Les Bleus au Bluu kwa Kiswahili.
Anapambana vikali na ubaguzi wa rangi hivyo kwamb a amekuwa mmoja wa wanaharakati wanaoongoza katika kizazi chake, akisafiri kwenda maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya kuzungumzia mambo hayo katika shule, vyuo vikuu na mikutano.
Thuram amejikuta katikati ya tufani kwenye vyombo vya Habari baada ya kufanya mahojiano na gazeti la Italia – ‘Corriere dello Sport’ kujadili ubaguzi wa rangi kwenye Ligi Kuu ya Italia – Serie A ambapo alikuwa na haya ya kusema: “Lazima uwe na ujasiri wa kusema kwamba watu weupe wanaamini kwamba wao ni bora zaidi.”
Sentenso hiyo iliwaudhi baadhi ya wananchi wenzake wa Ufaransa, na kusababisha mwandishi wa Habari za michezo, Pierre Ménès kusema; “tatizo la kweli kwa Ufaransa, kwenye soka kwa namna yoyote ni ubaguzi dhidi ya weupe.”
Utata huo uliozuka ulimfanya Thuram kukataa kupokea ombi la mahojiano mengine, lakini mwezi mmoja baadaye alikubali kukutana na kuyafanya na akaonekana alikuwa poa.
“Ukweli kwamba suala juu ya ubaguzi linajadiliwa zaidi na zaidi ni jambo jema. Na kama nashambuliwa inamaanisha kwamba kwa namna fulani matendo yangu hayawafurahisi baadhi ya watu. Wanajihisi kuwa hatarini, ambayo tena, ni ishara nzuri. Usisahau kwamba Nelson Mandela alituhumiwa kuwa mbaguzi wa weupe. Kadhalika Martin Luther King,” anasema Thuram.
Mfaransa huyu mweusi hajifikiri kuwa Mandela au King ajaye, lakini idadi ya vitabu kwenye shubaka lake ofisini vilivyowekwa kwa ajili ya watu wawili hao wazito, inaonesha kwamba anafurahishwa sana nao na anawapenda.
Mzaliwa huyu wa French West Indies, amekuwa akiguswa na masuala ya ubaguzi wa rangi tangu mama yake alipohamishia familia yake Paris mwaka 1981.
“Kilichonigusa san ani kwamba nilipowasili ni kwamba baadhi ya wanafunzi darasani kwangu walikuwa wakinihukumu kutokana na rangi ya ngozi yangu. Walinifanya niamini kwamba rangi ya ngozi yangu ilikuwa ya hadhi ya chini kulinganisha na yao na kwamba kuwa mweupe ni vyema zaidi,” anasema.
“Hao walikuwa watoto wenye umri wa miaka tisa tu. Hawakuzaliwa wabaguzi lakini tayari walianza kuendekeza kwamba wao ni bora. Tangu wakati huo nikaanza kujiuliza maswali; ‘kwa nini wananibeza? Hii inatokea wapi?’. Mama yangu hakuweza kunipa majibu, alichukuliwa kwamba ndivyo ilivyo tu. Kwamba kuna wabaguzi na hawatabadilika,” anaongeza.
Kutokana na kutoridhishwa na majibu ya mama yake, Thuram alijichmbia kwenye vitabu ili kupata maelezo mazuri zaidi, akijifunza matukio yaliyojenga uono huo potofu.
“Kihistoria tuliweka watu katika madaraja. Tuliweka watu juu kulingana na rangi ya ngozi zao. Tuliwaelimisha watu weupe kuona kwamba wao ni watawala dhidi ya wengine. Ni kama tulivyowafanya wanaume kuwatawala wanawake. Ni matatizo,” anasema.
Thuram alikuzwa na mama yake aliyekuwa mfanya usafi kwenye Halmashauri ya Les Fougères huko Avon, kusini mwa Jiji la Paris. Anayajua maisha magumu na jinsi ya kupambana na soka ilimpa heshima kubwa na sifa dhidi yaw engine kwenye jamii iliyokuwa na wahamiaji kutoka kila kona ya dunia.
“Nilicheza na watoto waliotoka Pakistan, Lebanon, Vietnam, Congo, Algeria … dunia yote ilikuwa pale. Soka ina nguvu kubwa ya kuleta watu pamoja na kuwafanya wajihisi kwamba ni sehemu ya kitu,” anasema.
Ulimwengu wa Thuram ulibadilika baada ya Arsène Wenger kumwingiza klabuni Monaco akiwa na umri wa miaka 17, ndipo akaanza safari ndefu iliyojaa kutwaa vikombe mbalimbali. Alikuja kwenda Italia akachezea Parma na Juventus na huko alikutana na ubaguzi, ikiwa ni pamoja na kutolewa sauti za nyani.
Babu yake alizaliwa mwaka 1908, ikiwa ni miaka 60 baada ya kumalizwa kwa utumwa huko Guadeloupe. Mama yake alizaliwa 1947 na wakati huo kulikuwa na ubaguzi katika Marekani. Mwenyewe alizaliwa 1972 na kulikuwapo ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Anasema ubaguzi mkali Ufaransa ulimalizika miaka ya ’60, lakini kuna wanaodhani kwamba leo upo zaidi ya wakati huo, jambo analosema si kweli.