Menu
in , , ,

LIGI YA MABINGWA ULAYA:

 

Man City SAFI, United wabanwa

 

Manchester City wamepiga hatua nzuri kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), baada ya kuwafunga Sevilla 2-1 kwenye mechi iliyopigwa nyumbani Etihad.

Alikuwa kiungo aliyesajiliwa kutoka Wolfsburg, Kevin de Bruyne aliyetia bao la pili la ushindi dakika ya 91, wakati washabiki wakiamini kwamba timu zingetoshana nguvu kutokana na bao la Yevhen Konoplyanka aliyekuwa nyota wa mchezo na la Sevilla kujifunga wenyewe.

De Bruyne alidhihirisha thamani yake ya pauni milioni 54 aliyonunuliwa nayo, ambapo kikosi cha Manuel Pellegrini kilionesha tatizo kiasi kwenye ushambuliaji, hasa wakati huu ambapo mshambuliaji wa kati, Sergio Aguero yu majeruhi.

Wahispania hao waliongoza kwa bao la dakika ya 30 lakini dakika sita tu baadaye City wakajibu mapigo, pale kiki ya karibu ya Wilfried Bony ilipomparaza Adil Rami baada ya kazi nzuri ya Yaya Toure na kujaa wavuni.

Sevilla walikuwa wazuri katika mashambulizi ya kushitukiza na mara kadhaa City walikuwa hatarini kukubali kichapo. Hizi ni pointi tatu muhimu ambazo Pellegrini amezipata katika mchezo wa pili mfululizo, tena katika dakika za lala salama kwenye mechi zote.

City sasa wapo pointi moja nyuma ya vinara wa kundi hilo, Juventus, ambao walilazimishwa sare na Borussia Monchengladbach. City wapo juu ya Sevilla kwa pointi tatu. Kazi kubwa kwa City ni kwamba mechi zao zote tatu za marudiano ni ugenini, wakianza na kwenda Hispania ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

Kabla ya safari yao watakuwa na mechi dhidi ya watani zao wa jadi – Manchester United, kwenye mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL) Jumapili hii, ambapo lazima Pellegrini aiweke sawa ngome yake ikiwa anataka kujihakikishia kuendelea kuongoza ligi.

City wameruhusu walau bao moja katika mechi saba zilizopita msimu huu, ambapo beki yao inayowashirikisha Eliaquim Mangala na Nicolas Otamendi – waliogharimu pauni milioni 70 kwa pamoja wakishindwa kucheza vyema pamoja.

Mabeki wa pembeni nao, Pablo Zabaleta na Bacary Sagna, wanaonekana kutocheza vyema, pengine kutokana na mfumo wa 4-4-2 unaowatupa akina De Bruyne na Jesus Navas kwenye wingi.

MANCHESTER UNITED WABANWA URUSI
Anthony Martial, akiifungia manchester united goli muhimu
Anthony Martial, akiifungia manchester united goli muhimu

Anthony Martial amewaokolea Manchester United pointi moja, baada ya kusawazisha bao katika dakika ya 65 dhidi ya CSKA Moscow.

Yalikuwa makosa ya Martial ya kuunawa mpira awali yaliyosababisha bao kwa wenyeji, likitiwa kimiani na Seydou Doumbia. Kipa wa United, David de Gea aliokoa penati iliyotolewa baada ya Martial kushika mpira, ikiwa imepigwa na Roman Eremenko.

Hata hivyo, United walioanza mechi hiyo wakionekana kutokuwa makini, walishindwa kumsaidia De Gea kufagia mpira huo, hivyo Doumbia akaukwamisha kimiani mara moja.

Martial alirekebisha makosa yake kwa kuhangaika kutafuta bao na akafanikiwa kufunga kwa kichwa kufuatia majalo ya Antonio Valencia. United sasa wanashika nafasi ya pili kwenye kundi lao wakiwa na pointi nne sawa na CSKA Moscow wakati PSV Eindhoven wakiwa nazo tatu. Wolfsburg wanaongoza kwa pointi sita baada ya kuwapiga PSV kwenye mzunguko huu wa tatu.

Nahodha wa United, Wayne Rooney ni kana kwamba hakuwapo uwanjani, ambapo ameendelea kushindwa kuwika na kutopata bao kwenye mechi za karibuni. Mechi ilichezwa katika hali ya hewa ya baridi kali, na itarejewa Old Trafford Novemba 3.

Katika mechi nyingine, Paris Saint-Germain (PSG) walikwenda suluhu na Real Madrid, Malmo FF wakawafunga Shakter Donetsk 1-0, Atletico Madrid wakawasasambua FC Antana 4-0, Galatasaray wakawazidi nguvu Benfica kwa 2-1.

Katika kundi A, timu zinazoongoza ni Real Madrid na PSG, kundi B ni Wolfsburg na Man United, Kundi C Benfica na Atletico Madrid, Kundi D Juventus na Man City. Katika kundi E Barcelona na Bayern Leverkusen wanashika usukani, Kundi F Bayern Munich na Olympiakos, Kundi G Porto na Dynamo Kiev, wakati kwenye Kundi H ni Zenit St Petersburg na Valencia.

Advertisement

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version