*Ni Arsenal na Bayern tena
*Chelsea na Porto, Man City na Juventus
*Man United kujiuliza kwa PSV ya Depay
Ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imetoka, ambapo kwa mara ya tatu katika misimu minne, Arsenal wamepangwa kucheza na mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich katika hatua ya makundi.
Pamoja nao, ni Olympiakos wa Ugiriki na Dinamo Zagreb wa Croatia, ambapo Arsenal watahitaji stamina na utimamu wa mwili kwani safari ya kwenda Croatia itakuwa siku chache tu kabla ya kucheza tena ugenini kuwakabili Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL).
Safari hii, mechi baina ya Arsenal na Bayern zitafuatana, kwa maana kwamba wakishapepetana nao ugenini Oktoba 20, hawatacheza na timu nyingine kwenye kundi lao badala yake watarudiana na Bayern hao hao Novemba 4.
Vijana wa Arsene Wenger watataka kuwalipizia kisasi wale wa Pep Guardiola, huku kiungo Aaron Ramsey akionesha kutotishwa na kundi lao, kwani anasema kwamba jamaa hao wameshakutana nao siku zilizopita, bali akaeleza huwa kuna msisimko mkubwa kila ratiba inapotolewa.
Ni mara mbili sasa vijana hao wa Bavaria wamewatupa Arsenal nje ya michuano hiyo katika misimu mitatu, lakini bado Wenger ana nafasi ya kusonga mbele kwenye mtoano katika zile 16 bora, ikiwa atachanga vyema karata zake, wakiwa na safari mbili ndefu za Ugiriki na Croatia ambazo huchosha.
Tayari Bayern wameanza tambo na vita ya maneno dhidi ya The Gunners, wakiwaambia wasahau kabisa kushika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao. Mlinzi Jerome Boateng amenukuliwa akisema kwamba siku zote hupenda kucheza dhidi ya Arsenal na kwamba wana bahati na London.
Ratiba hiyo inaonesha kwamba mabingwa wa England, Chelsea watakuwa kundi moja na klabu ya zamani ya bosi wao, Jose Mourinho, kwa maana ya Porto wa Ureno ambao aliwapa ubingwa wa Ulaya 2004. Ureno pia ndio nyumbani kwa Mourinho, ‘The Only One’, kama anavyojiita.
Wengine kwenye kundi hilo ni Dynamo Kiev wa Ukraine, ikimaanisha safari nyingine ndefu kwa wawakilishi wa England na pia wamo Maccabi Tel-Aviv wa Israel. Chelsea na Porto wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele.
Manchester City wao watakabiliana na Juventus wa Italia waliofika fainali ya UCL msimu uliopita lakini pia watapata mtihani dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Europa, Sevilla wa Hispania na klabu ya Ujerumani ya Borussia Monchengladbach.
Manchester United waliofuzu juzi kwa UCL kwa mechi ya mtoano ya mkondo wa pili dhidi ya Club Brugge wa Ubelgiji watakwenda nyumbani kwa bosi wao, Lous van Gaal kucheza na PSV Eindhoven, alikotoka mshambuliaji wao, Memphis Depay kiangazi hiki.
United pia watakabiliwa na safari ndefu ya kwenda Urusi, kwani kwenye kundi lao wamo CSKA Moscow lakini pia wana safari fupi tu ya Ujerumani kuwakabili VfL Wolfsburg. Katika kundi jingine kuna klabu za Benfica, Atletico Madrid, Galatasaray na Astana.
Droo inaonesha kwamba mabingwa wa Ulaya, Barcelona watakuwa kundi moja na Bayer Leverkusen, AS Roma na BATE Borisov wakati kundi jingine lina Paris St-Germain, Real Madrid, Shakhtar Donetsk na Malmo. Kunakundi linalojumuisha Zenit St Petersburg, Valencia, Olympique Lyon na Gent.
Kila timu itacheza mechi sita kwenye hatua ya makundi, ambapo mechi za awali zitakuwa Septemba 15 na 16. Klabu zote nne za England zimeepuka kukabiliana na klabu kubwa za Hispania – Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid ambazo huzipa tabu.