Liverpool wabanwa, Spurs chali
Bosi mpya wa Liverpool, Jurgen Klopp amebanwa kwenye mechi ya kwanza katika uwanja wa nyumbani wa Anfield kwa sare ya 1-1 dhidi ya timu ya Rubin Kazan iliyokuwa na wachezaji 10 tu kwenye mechi ya Ligi ya Europa.
Wageni walianza kupata bao kupitia kwa shuti zuri la juu la Marko Devic dakika ya 15 tu ya mchezo na muda mfupi baada ya hapo nahodha wao, Oleg Kuzmin alitolewa nje baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kwa mpira mbaya.
Hiyo inamaanisha kwamba Kazan walicheza pungufu kwa zaidi ya saa nzima, lakini Liverpool wakashindwa kutumia nafasi hiyo kujipatia ushindi, licha ya kutawala mchezo kwa asilimia 73.
Walisawazisha bao hilo dakika ya 37 kupitia kwa Emre Can kutokana na mpira wa adhabu ndogo. Mshambuliaji wa kati Christian Beneteke aliyetokea benchi alikaribia kufunga lakini shuti lake likagonga mwamba. Hii ni sare ya tatu mfululizo kwa Liverpool walio katika kundi B.
Liver walijitahidi kutia shinikizo kwenye lango la wapinzani wao dakika za mwisho lakini walishindwa kabisa kuipenya ngome na kufumania nyavu, huku wakiangaliwa na wamiliki wa klabu hiyo, Wamarekani John Henry na Tom Werner. Katika mechi ya ligi kuu dhidi ya Tottenham Hotspur ugenini wikiendi iliyopita, Klopp pia alibanwa na kuambulia sare.
Baada ya mechi hii, Klopp atakuwa tena nyumbani Anfield kuwakaribisha Southampton Jumapili hii kabla ya kusafiri kwenda kurudiana na Kazan Novemba 5. Liverpool hawajapata kushinda mechi zao nane zilizopita kwenye Ligi ya Europa au Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo walitoa sare tano na kufungwa tatu.
SPURS WACHAPWA NA ANDERLECHT
Tottenham Hotspur wameangukia pua ugenini baada ya kufungwa 2-1 na Anderlecht kwenye michuano hiyo hiyo, licha ya kuongoza kwa bao la mapema la Christian Eriksen. Bao hilo lilipatikana baada ya ngome ya wenyeji kujichanganya.
Hata hivyo Guillaume Gillet alisawazisha bao kwa upande wa Anderlecht kabla ya mfungaji wao mahiri, Stefano Okaka kutilia msumari wa mwisho. Nyota wa Spurs aliyetamba sana msimu uliopita, Harry Kane, aliingizwa kipindi cha pili, akapata nafasi nzuri ya kufunga lakini akababaika mbele ya kipa Silvio Proto.
Timu zote zilionesha soka safi ya kushambulia lakini Spurs walipoteza nafasi nyingi mapema mchezoni, na kama kuna wa kulaumiwa zaidi ni Erik Lamela. Anderlecht wanashika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji, maarufu kama Jupiler League.
Pande mbili hizi zitakutana tena White Hart Lane nyumbani kwa Spurs Novemba 5. Katika kundi lao, Monaco waliwafunga Qarabag 1-0 na kukwea kileleni. Spurs wamekwenda sare mechi zao tatu zilizopita katika mashindano yote nab ado hawajaonesha makali msimu huu.
Bosi wa Spurs, Mauricio Pochettino alisema kwamba amekasirika, kukerwa na kukatishwa tama na hali iliyowapata, akisema kwamba hana maneno sahihi ya kuelezea, kwani walianza vyema mchezo, wakatengeneza nafasi nyingi lakini wameishia kufungwa baada ya kupoteza mwelekeo.
Timu hiyo ya London Kaskazini inasafiri kwenda Bournemouth Jumapili hii kwa ajili ya mechi ya ligi kuu na Novemba 2 watakuwa wenyeji wa Aston Villa aliko kocha wao wa zamani, Tim Sherwood.
Katika matokeo mengine, Molde waliwafunga Celtic 3-1, Fernebahce wakawashinda Ajax 1-0, Apoel Nic wakawazidi nguvu Asteras Tripolis kwa 2-1. Schalke walitoshana nguvu 2-2 na Sparta Prague, AZ Alkamaar wakaloa nyumbani kwa 0-1 dhidi ya FC Ausburg.
Matokeo mengine yanaonesha kwamba Partizan Belgrade walilala nyumbani 0-2 dhidi ya Athletic Bilbao kama Bordeaux walivyochapwa 1-0 na FC Sion, FK Qabala wakalala 1-3 dhidi ya Borussia Dortmund wakati PAOK Salonika wakienda suluhu na FK Krasnodar.