NBC PREMIER LEAGUE
UKIANGALIA timu za Ligi Kuu Tanzania unaweza kusema bila hofu kuwa kiwango chake kimekuwa na kimewavutia wachezaji na makocha wengi. Ushindani wa timu mbalimbali kuelekea ubingwa wa Ligi hiyo umeonesha namna walivyojipanga na kushika nafasi mojawapo kati ya Ligi Kumi bora barani Afrika. Tanzania imekuwa kituo kizuri cha mpira wa miguu kuanzia Ligi Kuu ya Wanawake hadi wanaume.
Mathalani katika Ligi ya wanawake idadi kubw aya wachezaji kutoka Kenya, Rwanda, Burundi,Uganda na wengine toka Afrika Magharibi inaonesha jinsi kukua soka linavyoimarika nchini Tanzania. Tukibaki katika Ligi Kuu Tanzania kwa upande wa wanaume yapo mambo kadhaa ya kuangalia na kudhihirisha kuwa ni kivutio na kituo kizuri cha kufanya kazi.
Je Ligi Kuu inashika nafasi gani Afrika?
Miongoni mwa Ligi kubwa zinazotamba barani Afrika ni Ligi Kuu ya Tanzania. Zipo Ligi nyinginezo kama Afrika kusini,Tunisia,Morocco, Misri, Algeria zimekuwa na timu nyingi na zenye mafanikio katika mashindano ya Afrika. Ligi Kuu Tanzania inashika nafasi ya 6 katika ubora barani Afrika. Mafanikio ya vilabu viwili vya Simba na Yanga yamechangia kupandisha kiwango cha Ligi hiyo. Kwa upande wa Afrika Mashariki na Kati, Ligi Kuu Tanzania ndiyo nambari moja.
Nini siri ya kukua kwa Ligi Kuu?
Hakuna ubishi Ligi Kuu Tanzania ni kituo kizuri cha kufanya kazi. Katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Ligi Kuu ndiyo yenye mvuto na imekuwa chachu iliyowafanya viongozi wa CAF na FIFA kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji wa ufunguzi wa mashindano ya African Football League. Mashindano hayo yanajumuisha vigogo vya soka barani Afrika. Siri kubwa ya kung’ara kwa Ligi Kuu Tanzania ni uwepo wa wachezaji wa kigeni.
Uwepo wa wachezaji wa kigeni toka vilabu vya Afrika magharibi na baadhi kuitwa kwenye timu zao za Taifa ni sifa inayopandisha Ligi. Kwa mfano katika mashindano ya AFCON mwaka 2019 katika orodha ya wafungwaji bora lilikuwepo jina la Emmanuel Okwi ambaye alikuwa akitokea Ligi Kuu Tanzania. Kuanzia hapo idadi ya wachezaji wanaoitwa timu za Taifa za mataifa mbalimbali wamekuwa wakisakata kabumbu Ligi Kuu Tanzania.
Michuano ya AFCON mwaka 2023 kulikuwa na wachezaji wa vilabu vya Ligi Kuu katika timu za Taifa za Mali, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Nigeria,Tanzania kwa kuzitaja chache. Vilabu vya Yanga, Simba, Azam, Singida Black Stars vilifanikiwa kuwa wachezaji wake kwenye mashindano ya CAF. Msimu huu baadhi ya wachezaji wameongezeka kutoka Guinea.
Ni wachezaji kutoka Mataifa gani wapo Ligi Kuu?
Kipindi cha nyuma wachezaji wengi walitoka Ghana,Kenya,Uganda na Zambia. Hivi sasa ongezeko ni kubwa na kwamba wachezaji wanaosakata kabumbu Ligi Kuu na ambao wanatoka nje ya nchi wanatokea mataifa ya Nigeria, Cameroon, Kenya,Tunisia,Guinea, Uganda, Zambia, Malawi, Senegal na kadhalika.
Wachezaji wengi kutoka Afrika Magharibi wanavutiwa na Ligi Kuu kwa sababu imekuwa jukwaa zuri la kutangaza vipaji vyao. Baadhi ya wachezaji wa kigeni wamekuwa wakinunuliwa kutoka Ligi Kuu na kwenda kusakata kandanda katika nchi za Morocco,Tunisia,Misri na kwingineko. Timu mbalimbali za Ligi Kuu bila kujali ukubwa wake zimefanikiwa kuvutia wachezaji wa kigeni ambao wanaonesha vipaji vyao na kukuza thamani ya Ligi. Timu kama Tabora United, Fountain Gate,Singida Big Stars, Yanga,Simba, Azam, Namungo na nyingine nyingi zimekuwa sehemu ya kuwavutia wachezaji wa kigeni.
Makocha wenye viwango
Baadhi ya makocha wenye majina makubwa wlaiofundisha au wanaofundisha hadi sasa wanachangia kuleta mvuto wa Ligi Kuu. Nasredine Nabi raia wa Tunisia, alikuwa kocha maarufu barani Afrika ambaye aliifikisha Yanga katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho.
Ingawaje alikosa ubingwa lakini kandanda safi liliooneshwa na Yanga lilikuwa gumzo. Ujio wa makocha wa kigeni kama Didier Gomes, Miguel Gamondi, Pablo Martin, Milutin Micho na wengine umechangia kukuza ‘brand’ ya Ligi Kuu ya NBC na kuleta elimu mpya ya kusakata kandanda. Makocha wenye ujuzi wanavutiwa na majukwaa ambayo yanaonekana mara kwa mara kwenye mashindano ya Afrika. Mfano kila kocha angependa kuona anashiriki kuchuana mashindano ya Kimataifa na hivyo kunoa uwezo wake pia.
Malipo mazuri
Miongoni mwa sababu zinazovutia wachezaji wa kigeni ni malipo mazuri yanayolipwa na vilabu vya soka vya Ligi Kuu. Ingawaje hakuna takwimu sahihi lakinj wapo wachezaji wanaolipwa vizuri na baadhi wanapokea milioni 13 kwa mwezi na wengine hadi Milioni 30. Inaelezwa kuwa wapo wachezaji wenye majina makubwa wanavuta malipo manono na kuwa chanzo cha kuwavutia wengine kuja kuchezaji Ligi Kuu Tanzania. Endapo kungekuwa na malipo madogo bila shaka wachezaji wasingekimbilia Tanzania kucheza soka.
Udhamini mnono
Kuanzia udhamini binafsi wa vilabu na Ligi Kuu umekuwa mchango mkubwa katika maendeleo ya soka. Vilabu vimefanikiwa kupata wadhamini binafsi ambao wanatoa fedha zinazowezesha uendeshaji kuwa mzuri na kupunguza makali zaidi. Katika mchezo wa soka suala la uendeshaji linahusiana sana na upatikanaji wa fedha. Kwahiyo wadhamini wa Ligi Kuu wanapotoa fedha kwa vilabu ukiongeza na udhamini binafsi vinakuwa mchango mkubwa katika maendeleo ya Ligi Kuu.