*Mercedes wachekelea ushindi wa kwanza
Hatimaye Lewis Hamilton amepata ushindi wa kwanza tangu ajiunge na Mercedes, katika mashindano ya Formula One.
Hamilton aliyeona ushindi wake huo kama muujiza, anasema hawakuwa na wazo la ushindi hata kidogo, na hata katika hatua za mwisho bado alichokuwa akiangalia ni usalama wa matairi ya gari lake.
Alipata ushindi wa kwanza kwenye mashindano ya Hungarian Grand Prix, ambapo alidhibiti vyema gari lake na kuwafunika dereva wa Lotus, Kimi Raikkonen na yule wa Red Bull, Sebastian Vettel walioambulia nafasi ya pili na ya tatu katika mtiririko huo.
Tangu ajiunge na Mercedes, Hamilton alikuwa akisema bado alikuwa akijifunza na pia ingechukua muda kuizoea kampuni hiyo mpya, baada ya kuwa na McLaren kwa muda mrefu, ambapo alipata kusahau kwenda kuongeza mafuta kwenye kutuo cha Mercedes na kuegesha gari kwenye McLaren hatua iliyomsababisha kupoteza pointi zaidi.
Mark Webber wa Red Bull anayejulikana kwa uwezo wake mkubwa, alikuwa katika nafasi ya 10, lakini katika hatua za mwisho akachupa hadi ya nne, mbele ya Fernando Alonso wa Ferrari.
Ilikuwa furaha isiyo kifani kwa Hamilton na timu nzima ya Mercedes, ambapo sasa anakuwa pointi moja mbele ya Alonso kuendea ubingwa wa pili, lakini pointi 38 nyuma ya Vettel ambaye amejiweka sawa kutwaa ubingwa wan ne.
“Ni sahihi kusema kwamba nilikuwa na njaa ya ubingwa huu leo…ni muujiza,” alisema Hamilton, sababu kubwa ikiwa matatizo ya matairi ya Mercedes kwa siku za karibuni na hali ya hewa ya joto kali.
Hamilton ameshinda mara nne katika mashindano saba kwenye Hungaroring, ushindi wake ukiwa na McLaren mwaka 2007, 2009 & 2012, na sasa na timu yake mpya.