*Spurs washinda kwa mbinde
* Adebayor aachwa, hana timu
Leicester City wameendeleza rekodi yake nzuri ya kutofungwa, baada ya kupambana hadi kutoka nyumba kwa mabao 2-0 dhidi ya Aston Villa na kushinda kwa 3-2.
Kwa ushindi huo, baada ya mzunguko wa tano Leicester wamechupa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Villa walianza mechi vyema wakitawala mchezo, ambapo Jack Grealish alifunga bao zuri kutoka yadi 20. Carles Gil akafunga bao la pili na kuwaaminisha washabiki wa Villa wangeondoka na ushindi.
Hata hivyo, Leicester walijipanga na Ritchie de Laet akachomoa moja kabla ya Jamie Vardy kuwasawazishia Leicester.
Alikuwa ni Nathan Dyer aliyefunga bao la ushindi kwa Leicester kwa kichwa kizuri katika mechi yake ya kwanza. Alisajiliwa siku ya mwisho ya usajili kutoka Swansea.
SPURS WAWAPOKA POINTI SUNDERLAND
Spurs kwa muda wote walishindwa kuvuka vigingi vya Sunderland, kocha mahiri Costel Pantilimon akizuia hatari nyingi.
Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino anasema kwamba bao hilo linaonesha falsafa ya timu. Mchezaji wa zamani wa Spurs, Jermain Defoe anayekipiga Sunderland alipata nafasi nzuri zaidi lakini akashindwa kufunga.
Matokeo hayo yanawafanya Spurs kuwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Manchester City wanaongoza ligi wakiwa na pointi 15, wakifuatiwa na Leicester wenye 11, Arsenal na Manchester United wenye pointi 10 kila moja. Leo West Ham wanakipiga na Newcastle United.
SPURS WAACHANA NA ADEBAYOR
Klabu na mchezaji wamefikia mwafaka kwamba mkataba wa raia huyo wa Togo mwenye umri wa miaka 31 utenguliwe. Awali, aliachwa kwenye orodha ya wachezaji watakaokipiga EPL na Ligi ya Europa, lakini alibaki mchezaji wao.
“Tunamtakia Emmanuel hatima njema,” taarifa ta Spurs imesema, ikiwa ni baada ya kocha Pochettino kunukuliwa wiki iliyopita akisema kwamba Adebayor hakuwa akilini mwake wala kwenye mipango ya Spurs.
Alisajiliwa kwa pauni milioni tano 2012 akitoka Manchester City na alikuwa bado na mwaka mmoja kwenye mkataba wake. Alikuwa akitaka alipwe pauni milioni tano ili kuukatisha, vinginevyo angebaki akiendelea kupata mshahara pasipo kucheza.
Spurs hawajasema wameachana na Adebayor kwa makubaliano gani. West Ham walitaka kumsajili mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal na Real Madrid, lakini walighairi kutokana na mwenyewe kutaka mshahara mkubwa mno. Aston Villa pia walikuwa katika hali hiyo.
Hatima ya Adebayor ndani ya Spurs ilionekana kuzama kutokana na kuwapo washambuliaji Harry Kane na hivi karibuni raia wa Korea Kusini, Son Heung-min aliyeingizwa White Hart Lane kwa pauni milioni 22.