Vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL), Leicester wameendelea kuchanja
mbuga baada ya kupata ushindi mwembamba dhidi ya Norwich.
Ilikuwa mechi iliyodhaniwa kwamba ingemalizika kwa suluhu, lakini
vijana wa Claudio Ranieri walipata bao dakika ya 89.
Alikuwa ni Leonardo Ulloa aliyesababisha Leicester kuweka pengo la
pointi tano kileleni, baada ya kuunganisha majalo ya Marc Albrighton.
Pamoja na kwamba walicheza dhidi ya timu dhaifu na kutarajiwa
kuchomoza na ushindi mapema, Leicester ambao ni maarufu kwa jina la
Foxes hawakuwa kwenye kiwango chao cha juu na Norwich ndio
walitengeneza nafasi zaidi za kufunga.
Norwich waliwatega hivyo kwamba wenyeji walitegemea zaidi kupiga
mashuti kutoka mbali na waliendelea hivyo hadi Ulloa aliyetokea benchi
kupata fursa muhimu na kuitumia ipasavyo.
Laiti wasingefunga bao hilo, wangeweza kuondolewa kileleni Jumapili
hii ikiwa Arsenal au Tottenham Hotspur wangeshinda mechi zao, lakini
sasa wana uhakika wa kubaki kwenye kiti hadi mzunguko ujao, zikiwa
zimebaki mechi 12.
Norwich kwa kufungwa huko bado wapo nje ya eneo la kushuka daraja,
lakini wanafungana kwa pointi na waliomo humo, Newcastle, hivyo
watatakiwa kukaza mkanda kwenye mechi zilizobaki.
Katika mechi nyingine Jumamosi hii, West Ham waliwaadhibu Sunderland
kwa kuwapiga bao 1-0 na kuwaweka katka hatari kubwa ya kushuka daraja,
Southampton wakalala nyumbani kwao walipotandikwa 2-1 na Chelsea.
Stoke waliwazidi nguvu Aston Villa kwa 2-1, Watford wakatoshana nguvu
kwa 0-0 na Bournemouth wakati West Bromwich Albion waliwafunga Crystal
Palace 3-2.
Ligi hiyo inaendelea leo kwa Manchester United kuwakaribisha Arsenal
na Spurs watakuwa wenyeji wa Swansea.