Menu
in , , ,

Leicester hawakamatiki

Tanzania Sports

Vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL) wameendelea kupaa, wakifikisha
pointi 69, zikiwa ni saba zaidi ya wanaowafuata, Tottenham Hotspur.

Leicester wamefika hapo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
Southampton katika mechi ngumu. Washindi walipata bao kupitia kwa
nahodha wao, Wes Morgan aliyefunga kwa kichwa dakika ya 38 na Saints
wakashindwa kurudisha.

Leicester, Spurs na baadhi ya timu zimecheza mechi 32, lakini Arsenal
walio nafasi ya tatu wakiwa na pointi 58, Manchester City wenye 54
katika nafasi ya nne na Manchester United wenye 53 katika nafasi ya
tano, wamecheza mechi 31 kila moja.

Lilikuwa bao la kwanza kwa Morgan msimu huu, akiunganisha majalo ya
Christian Fuchs. Nusura Southampton wafunge bao kupitia kwa Sadio Mane
aliyekuwa ameshafanikiwa kumzunguka golikipa Kasper Schmeichel, lakini
alipodhani ametia mpira kimiani, akakuta ukizuiwa na Danny Simpson na
kuendeleza bahati ya Foxes.

Iwapo Leicester watashinda mechi zao nne zijazo watatawadhwa kuwa
mabingwa wapya wa England, ikiwa ni mara yao ya kwanza. Wameushangaza
ulimwengu wa soka kwa jinsi walivyopanda chati, kwani Aprili mwaka
jana walikuwa mkiani mwa ligi.

Vijana hao wanaofundishwa na Mtaliano Claudio Ranieri wameshinda mechi
zao tano zilizopita kwa bao 1-0. Baada ya Spurs kupunguzwa kasi kwa
kwenda sare na Liverpool wikiendi hii, sasa Leicester wanapewa nafasi
kubwa kutwaa ubingwa.

Kwa kufungwa huko, Saints wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa
ligi, na ni mechi ya kwanza kupoteza katika nne zilizopita. Kocha wa
Saints. Ronald Koeman alilalamikia mwamuzi akisema walinyimwa penati,
akidai kwamba ni mechi ya tatu mfululizo wananyimwa penati zilizokuwa
haki yao kwa asilimia 100.

Alidai kwamba Jumapili hii shuti la Mane lilizuiwa kwa mkono na
Simpson, akasema walistahili penati na Simpson apewe kadi nyekundu,
vinginevyo wangepewa bao, lakini akashangaa waamuzi kukaa kimya tu.

Jumapili wiki ijayo Leicester watacheza na Sunderland wanaoshika
nafasi ya 18 wakiwa na pointi 27 wakati Southampton watapepetana na
Newcastle Jumamosi.

Katika mechi nyingine, Manchester United walipata ushindi mwembamba
dhidi ya Everton, kwa bao moja la Mfaransa Anthony Martial, kwenye
mechi ambayo walilipa jukwaa moja jina la Sir Bobby Charlton.

Martial aliipokea vyema majalo ya Tim Fosu-Mensah katika dakika ya 54
na kucheka na nyavu, ikiwa ni mechi ya tatu mfululizo kwa Everton
kufungwa katika EPL. Ushindi huo unawaacha United pointi moja nyuma ya
mahasimu wao – City, wakifukuzia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa
Ulaya.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version