MASHINDANO mbalimbali yanayofanyika hapa duniani yamekuwa yakilalamikiwa na wadau, makocha, wachezaji na mashabiki wa Soka. Hali ya matukio yanayotokea Ligi Kuu Tanzania nayo yamesababisha malalamiko mengi. Uamuzi mwingi unaofanywa au makosa ya waamuzi yameathiri baadhi ya timu. TANZANIASPORTS inachambua kwa kina juu ha mwenendo wa waamuzi wa Ligi Kuu duniani.
WAAMUZI WA EPL KWENDA LA LIGA
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ni miongoni mwa majina makubwa kwenye mchezo wa Soka. Yeye ndiye mwanzilishi wa mpango wa kuanzisha European Super League ambayo anaamini ingekuwa na thamani zaidi kuliko Ligi ya Mabingwa ya sasa ya Ulaya. Hivi karibuni klabu ya Real Madrid iliandika barua kwenda kwa Shirikisho la Soka nchini Hispania na waendeshaji wa Ligi hiyo maarufu kama La Liga. Katika barua yake Real Madrid walilalamikia uamuzi uliofanywa katika mchezo wao dhidi ya Espanyol uliochezwa huko Catalunya ambapo matukio kadhaa yaliashiria mwamuzi alishindwa kumudu mchezo. Pia Madrid wanalalamika juu ya maamuzi kadhaa ya waamuzi wa La Liga kwa madai yamekuwa chini ya kiwango na yameathiri Klabu yao. Pia katika mchezo dhidi ya Leganes , klabu ya Real Madrid mwamuzi alishindwa kumudu mchezo ikiwemo kutafsiri vibaya Sheria za Soka. Real Madrid hawakuishia kulalamika pekee bali wametoa pendekezo lao muhimu Kwa ajili ha kuinua Soka la La Liga. Madrid wanapendekeza Shirikisho la Soka nchini Hispania lianze kuwaajiri waamuzi kutoka Ligi Kuu England. Kwa mtazamo wa Real Madrid waamuzi wa EPL Wana kiwango kikubwa kuliko wale wa La Liga. Haijulikani Shirikisho la Soka litachukua uamuzi gani lakini hali hii inadhihirisha kuwa yapo matatizo ya waamuzi wa mchezo wa Soka kote duniani.
EPL KUNAWAKA MOTO
Liverpool ndiyo klabu iliyokumbana na maamuzi mengi yenye utata msimu uliopita. Kutokana na uamuzi wa utata uliwalazimisha chama cha waamuzi kuwaomba radhi kwa makosa yaliyowahi kutokea. Changamoto ya waamuzi imekuwa gumzo EPL. Waamuzi wanalalamikiwa namna wanavyotafsiri vibaya Sheria 17 za soka. EPL kuna matatizo ya uamuzi katika Sheria za kuotea, adhabu ya penalti, adhabu ya kadi za onyo na kutolewa nje. Ni sababu hiyo kadi aliyowahi kupewa Lewis Skelly ilifutiliwa mbali na kumruhusu kucheza mchezo uliofuata. Hii inadhihirisha kuwa hata EPL ambako Rais wa Real Madrid anaamini kuna waamuzi wazuri lakini wanakabiliwa na changamoto ileile ya kutafsiri vibaya Sheria 17 za soka.
LIGI KUU TANZANIA
Katika Ligi Kuu Tanzania malalamiko hayo ni mengi sana. Timu zinapata ushindi katika mazingira ya kutatanisha, adhabu za kadi za onyo,adhabu za penati, adhabu za kadi nyekundu, na maamuzi mengi ya waamuzi yamekuwa yakilalamikiwa. Malalamiko hayo yapo katika timu mbalimbali. Lakini waamuzi wamekuwa wakifanya makosa mengi kwenye mechi zinazohusisha timu za Simba,Yanga au Azam. Vilevile hata kwenye timu zingine kumekuwa na malalamiko ambayo waamuzi wanatakiwa kuyarekebisha.
SOMO LA KOMBE LA DUNIA

Hii Ina maana changamoto ya waamuzi ni jukumu kubwa la bosi wa waamuzi duniani Piereluigi Colina raia wa Italia. Wakati fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, Collina na wasaidizi wake waliingiza utaratibu wa muda wa nyongeza kuwa dakika 10 na zisizopungua 7. Hilo lilitokana na kugundulika kuwa muda wa kushangilia,kutoa matibabu,kuumia kwa wachezaji ni sehemu inayopunguza muda wa dakika 90 za mchezo. Kwa uamuzi wa kuongeza dakika 10 ulikuwa mzuri na umewapa waamuzi utawala zaidi viwanjani. Katika mazingira hayo ya malalamiko ya wadau, wachezaji na makocha wa Soka ni dhahiri FIFA, UEFA,CAF na mashirikisho mengine yenye dhamana yanalo jukumu la kuinua viwango vya waamuzi katika ngazi zote kuanzia klabu hadi timu za Taifa. Kulalamikiwa waamuzi ni sehemu ya mchezo na kutaka mabadiliko. Licha ya ongezeko la teknolojia bado waamuzi wamekuwa kwenye wingu la makosa mengi ya kutafsiri Sheria 17 za soka.
MADHARA YA WAAMUZI WABOVU
Baadhi ya Ligi barani Afrika zimeshuhudia wachezaji wakigombana na waamuzi viwanjani au baadhi ya viongozi nao huingia kwenye ugomvi na marefa kwa sababu wanashindwa kuvumilia makosa yao. Uwekezaji Mkubwa unaofanywa na Wafanyabiashara au wawekezaji kwenye mchezo wa Soka ni muhimu uendane na ubora wa waamuzi. Hilo ni eneo lingine ya kutupiwa jicho ili kuwa na waamuzi wenye viwango katika Ligi Kuu.