KIUNGO mkongwe na mahiri aliyeachwa na Chelsea, Frank Lampard anatarajiwa kujiunga na Manchester City.
Lampard aliyemaliza mkataba wake Chelsea baada ya kuitumikia kwa miaka 13, alisajiliwa na New York City FC ya Marekani inayotarajia sasa kumtoa kwa mkopo achezee mabingwa hao wa England.
Lampard (36) alikuwa nahodha msaidizi wa Chelsea na anakipiga pia Timu ya Taifa ya England, ambapo hivi karibuni ameonekana kuchokwa na Chelsea lakini iwapo wangejua uwezekano wa yeye kutinga Etihad huenda wangemwongeza mkataba.
Mchezaji huyo alifunga mabao 211 katika mechi 649 alizochezea Chelsea na hadi sasa ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya klabu hiyo, jambo alilolipigania sana alipokaribia ukingoni.
Lampard amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili nchini Marekani, lakini ligi yao haianzi hadi Machi mwakani, hivyo anatarajiwa kucheza London hadi Januari, ikielezwa kwamba wiki ijayo atafika kwenye viwanja vya mazoezi vya Man City ili kocha Manuel Pellegrini atazame ufiti wake kabla ya kuanza kubeba jukumu jipya.
New York City pamoja na New York Yankees zina umiliki mmoja, ambapo majuzi wamefikia makubaliano ya Man City kutoa wachezaji wake kwa mkopo kucheza New York kama njia ya kuwakuza.
Japokuwa hadi asubuhi ya Jumamosi Man City hawakuwa wamesema chochote juu ya suala hilo, inadaiwa kwamba Lampard atasaini mkataba wa kuichezea klabu katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya kadhalika.
Man City walipotwaa ubingwa msimu uliopita, Chelsea walishika nafasi ya tatu ambapo waliondoka bila taji lolote msimu huu, wakiwaacha City na Arsenal kufurahia makombe makubwa, huku Man United wakitwaa Ngao ya Jamii.
Lampard alianza soka yake West Ham, ambako baba yake pia alicheza. Mchezai wa zamani wa Hispania, David Villa (32) naye amasajiliwa na klabu hiyo ya MLS na amekwenda kwa mkopo Melbourne FC, ambao ni washirika kikampuni wa Manchester nchini Australia.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Man City, Ferran Soriano amesema kwamba sababu mojawapo ya Villa na Lampard kukubali kusajiliwa na klabu hiyo ni kwa vile wanafahamu nani anamiliki na kuendesha klabu hiyo.
Lampard amechezea England mechi 106 na bado hajaamua kustaafu soka ya kimataifa. Wachezaji kadhaa wa MLS wamekuwa kwa mkopo kwa klabu za Ligi Kuu ya England nyakati za mwisho wa msimu, ikiwa ni pamoja na Clint Dempsey aliyeenda Fulham, Landon Donovan pale Everton, Robbie Keane Aston Villa naThierry Henry kwa klabu yake ya zamani, misimu michache iliyopita.