Ligi Kuu ya Hispania – La Liga inatarajiwa kuanza tena mwishoni mwa mwezi ujao – Mei.
Rais wa La Liga, Javier Tebas anasema kwamba kwa mwenendo wa virusi vya corona ulivyo, huenda wakarejea uwanjani mwishoni mwa mwezi huo, akiweka tarehe 28 kama yenye uwezekano.
Wadau wameanza mjadala juu ya jinsi ya kurejea kwa ligi ambayo hadi inaahirishwa kwa muda usiojulikana Barcelona na Real Madrid walikuwa wakikabana koo kileleni. Wakati baadhi ya wadau wa soka kama Pep Guardiola na Lionel Messi wametoa msaada kwa taifa hilo, Guardola amempoteza mama yake kwa homa hiyo kali ya mapafu maarufu kwa jina la COVID-19.
Hakuna timu ya Hispania iliyocheza mechi yoyote ya ushindani tangu Machi 11 mwaka huu, pale Atletico madrid walipowapiga Liverpool na kuwavua ubingwa wa Ulaya katika Ligi ya Mabingwa (UCL).
Tebas, hata hivyo, anasema kwamba La Liga haitarejea hadi hatua za dharura zilizowekwwa hadi Aprili 26 ziondolewe na mamlaka husika. Anakadiria kwamba klabu zitakuwa katika hali mbaya kifedha, ambapo ikiwa ligi itabatilishwa kabisa huenda zikapoteza hadi euro bilioni moja hivi.
Tebas anasema kwamba kuna tarehe tatu zinazojadiliwa kwa pamoja na Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), akisema wanazingatia matakwa ya nyakati na usalama wa wadau watakaohusika kwenye mechi hizo. Anasema kwamba licha ya Mei 28, tarehe nyingine wanazojadili kwa ajili ya michuano ya Ulaya ni Juni 6 au Juni 28.
“Hatuwezi kutaja tarehe kamili. Hiyo tutapewa na mamlaka ya Serikali ya Hispania. Hata hivyo bado tunao muda wa kurudi uwanjani kwa ajili ya mazoezi kujiandaa kumalizia kipande cha msimu kilichokatwa na virusi hivyo hatari,” anasema Tebas.
Kiongozi huyo anasema hawataki kufikiria kushindwa kumalizia La Liga wala michuano ya Ulaya, kwa sababu hasara itakuwa kubwa sana kwa klabu, watu binafsi pamoja na Bodi ya La Liga ambayo imebakisha raundi 11 kukamilisha msimu wa soka wa 2019/2020.
Inaelezwa kwamba kwa hali ilivyo, katika muda mfupi ujao uwezekano ni kucheza mechi bila watazamaji, baada ya wachezaji na maofisa wote wanaotakiwa kuingia uwanjani kupimwa na kuhakikiwa kwamba hawana madhara ya ugonjwa huo hatari.
Tebas anasema kwamba ukitazama madhara ya kiuchumi yanayoweza kutokea, ikiwa ni pamoja na kutoka kwenye mashindano ya kimataifa, klabu za Hispania zinaweza kukosa mapato ya haki za televisheni iwapo hawatarudi kumalizia mechi hizo. Kwamba wakati wakiacha kabisa watapoteza kadiri ya euro bilioni moja, wakicheza bila watazamaji itakuwa euro milioni 300.
Anasema kwamba hata wakirudi na kucheza na watazamaji, tayari kuna hasara ambayo imeshatokea, kiasi cha euro milioni 150. Uefa wamewataka nchi mbalimbali kutofuata mfano wa Ubelgiji ambao wametangaza kumaliza ligi kuu yao bila timu zote kuwa zimekamilisha mechi zao.
Uefa wanasema kwamba iwapo mataifa yatachukua hatua kama hiyo, kuna hatari ya klabu zao kuzuiwa kushiriki kwenye michuano ya UCL na Ligi ya Europa. Kua kundi kazi linalohusisha wawakilishi kutoka Chama cha Klabu za Ulaya linatarajia kuwasilisha pendekezo kabla ya katikati ya Mei mwaka huu juu ya lipi la kufanya.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kuona kwamba mechi za ligi za nyumbani zichezwe wikiendi na mechi za Ulaya zichezwe katikati ya wiki. Mapendekezo mengine ni kuhakikisha wanamaliza ligi hiyo Juni au Julai na mechi za Ulaya kumalizwa Agosti.
Bosi huyo anasema kwamba kila nchi ni tofauti na nyingine; kwamba England wana mashindano matatu, Hispania na Italia wanayo mawili mkononi wakati Ujerumani wanazo timu 18 kwenye Ligi Kuu – Bundesliga wakati wengine wote wanazo timu 20.
Kwenye ligi zenye zitakazojikuta kuwa na matatizo kwenye kalenda zao za ndani zitatakiwa kuwasiliana na Uefa kwa ajili ya kupata ufumbuzi kiuratibu na kwa mashauriano ili kuhakikisha msimu unamalizika vyema kwa kuzingatia mashindano ya Ulaya ya klabu.
La Liga tayari wamepokea asilimia 90 ya fedha za haki za matangazo ya televisheni. Hata hivyo, bado asilimia 28 ya mechi hazijachezwa kwa hiyo ikiwa itashindikana ligi kumalizika itamaanisha kwamba fedha zitarejeshwa na hivyo klabu kuingia kwenye madeni kwa sababu tayari walio wengi wameshazitumia kwa vile hawakujua kwamba janga la corona lingekuja.
Ligi ya Hispania imekuwa ikitafuta msaada kutoka kwa achezaji ili wakubali kukatwa sehemu ya mapato yao kusadia kusuluhisha janga la corona. Hakuna makubaliano hadi sasa, wachezaji wa Barcelona na Atletico Madrid wakifikia makubaliano binafsi na klabu zao.