*Wachezaji aghali zaidi wapo huko
*Kigogo ataka wachezaji wote bora
Rais wa Ligi Kuu ya Hispania, Javier Tebas, amesema wanataka kuvutia wachezaji bora zaidi kwao ili kuibomoa Ligi Kuu ya England (EPL).
Tebas amesema kwamba kwa timu za La Liga kusajili wachezaji bora na ghali, watahamishia kwao nguvu za kiuchumi na kuwa ligi maarufu zaidi duniani.
Bosi huyo alitania kwa kusema hata wakiweza watachukua wachezaji bora zaidi 500 wa dunia ili wacheze nchini Hispania na kuifanya ligi yao iifunike ya England ambayo inafuatiliwa zaidi ya zote duniani.
Luis Suarez aliyenunuliwa kwa pauni milioni 75 na Gareth Bale kwa pauni milioni 85.3 ndio wachezaji wa karibu zaidi na ghali zaidi kutoka England kwenda Hispania.
“Hatutaacha kuwachukua, tunataka wachezaji bora zaidi 500 wa dunia hapa. Tunataka kuhakikisha sisi tunakuwa na klabu kubwa zaidi na wachezaji bora zaidi duniani wawe katika ligi yetu,” akasema.
Bale alinunuliwa Totteham Hotspur akahamia Real Madrid msimu uliopita wakati Suarez ndio kwanza anasubiri kuchezea Barcelona akitoka Liverpool.
Kadhalika nyota waliotamba kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil, James Rodriguez wa Colombia aliyekuwa mfungaji bora na Toni Kroos wa mabingwa Ujerumani wamejiunga Real Madrid kiangazi hiki.
Kadhalika, Real Madrid sasa wanajidai kwa kuwa mabingwa wa Ulaya wakati Sevilla ndio mabingwa wa Kombe la Europa.
Wachezaji kama David Beckham na Cristiano Ronaldo (mwanasoka bora wa dunia) nao waliondoka Ligi Kuu ya England (Manchester United) na kuingia Real Madrid katika La Liga.
Ukali wa Hispania utaonekana kwenye mechi ya watani wa jadi ambapo kutakuwa na wachezaji ghali na maarufu zaidi, wakiwamo Rodriguez, Kroos, Suarez Bale, Ronaldo, Neymar na baba lao, Lionel Messi.
Mabingwa wa Hispania, Atletico Madrid nao wamejikuna na kumsajili kwa pauni milioni 22 mchezaji kutoka Bayern Munich, Mario Mandzukic na wamekubali kuwalipa Real Sociedad pauni milioni 24 kumsajili winga Mfaransa aliyekuwa akiwindwa na timu za England, Antoine Griezmann.
Wachezaji watano ghali zaidi katika historia ya dunia walijiunga La Liga ambao ni Bale (£85.3m), Ronaldo (£80m), Suarez (£75m), Rodriguez (£71m) na Kaka aliyesajiliwa Madrid kutoka
AC Milan kwa pauni milioni 56.
Valencia wamekohoa pauni milioni 15 na kumsajili nyota Andre Gomes wa Benfica. Hata hivyo, baadhi ya klabu za Hispania, zikiwamo Atletico, Sevilla na Valencia zimeigia madeni makubwa katika jitihada za kuwashika Real Madrid na Barcelona huku Malaga na Rayo Vallecano wakipigwa marufuku mashindano ya Uefa kutokana na zigo la madeni linalotishia kuzifilisi timu hizo.
Mfumo wa La Liga ni kwamba kila timu inajadiliana na wadhamini kwa ajili ya matangazo ya kwenye televisheni, ambapo Barcelona na Real Madrid walipata pauni milioni 110 msmu uliopita huku timu nyingine zikiambulia kidogo sana.
Hiyo ni tofauti na England, ambapo Premier League hujadiliana na kuingia dili kwa pamoja kwa niaba ya klabu na msimu uliopita dili za TV ziliipatia pauni bilioni 3.018.
Tebas anajaribu kufukia pengo baina ya ligi mbili hizo kwa kuipandisha chati La Liga ili kuvutia masoko mapya kutoka Amerika na Asia, kwenye mabilionea wanaoonesha mvuto katika soka.