Fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika zinatarajiwa kufanyika nchini Cameroon ifikapo Januari hadi Februari mwaka 2022. Zimesali siku chache kabla ya michuano kuanza kutimua vumbi nchini Cameroon, huku kukiwa na matukio mbalimbali yanayosisimua na kusikitisha kwa wakati mmoja.
Katika makala haya yanaangazia suala la uteuzi wa waamuzi wa kuchezesha mashindano hayo, ambapo hakuna marefa kutoka Ligi Kuu Tanzania hawajaitwa kuwa sehemu ya kuchezesha mashindano hayo makubwa barani Afrika.
TANZANIASPORTS imezungumza na wadau mbalimbali kuona sababu zinazochangia waamuzi wa Ligi kuu Tanzania na majirani zake kutopata nafasi za kuchezesha mashindano makubwa kama AFCON au Kombe la dunia. Kwa vile wadau wa soka wamekuwa wakijadili kwa wingi, makala haya ni zao la maoni yao.
KANUNI ZINAONGEA
“Waamuzi kuchezesha mashindano ya AFCON ni suala la mchakato. Ili kufika hapo AFCON lazima uchezeshe michuano ya chini ya hapo kama U-17,U-20 kisha CHAN na ndipo baadaye unaweza kuteuliwa kuchezesha AFCON. Kila ngazi ina miaka miwili ndio unakwenda ngazi nyingine. Hapo kwa waamuzi wetu anayekaribia ni Frank Komba ambaye tayari ameshachezesha CHAN. Ukiweza kufika AFCON basi utakuwa na vigezo vya kuchezesha michuano mikubwa ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 na 20 kisha utapewa michuano ya Olimpiki na baadaye utachezesha Fainali za Kombe la Dunia kwa wakubwa. Kote huko kunahitaji uoneshe uwezo,”
VIWANGO VIDOGO
“Marefa wetu ni sawa wanachezesha mechi nyingi za CAF na FIFA lakini nyingi zinakuwa zile za kuwania kufuzu. Lakini pale wanaposema sasa wanachagua waamuzi wa kuchezesha fainali kubwa kama hiyo, marefa wetu wanapungua uwezo kwa kuzidiwa na wenzao. Leo hii kila siku sisi wenyewe tunawalalamikia kuhusu uwezo wao, lakini ni aibu kwa taifa kama hili ambapo karibia wachezaji wote wa Afrika mashariki wana hamu ya kuja kucheza Tanzania ila tunakosa waamuzi wenye viwango vya juu. Katika nchi zote za Afrika mashariki wametoa waamuzi isipokuwa Tanzania. leo hii hata Djibout wanatoa waamuzi, sisi tunashindwa nini.”
TATIZO LA KUTAFSIRI SHERIA
“CAF hufanya athmini pia kwa mechi wanazochezesha waamuzi wa wetu, ufuatiliaji wa sheria za uamuzi pamoja na maoni ya wadau mbalimbali baada ya mechi, kwa Tanzania ni nadra sana kukuta waamuzi wetu kusifiwa baada ya mechi kwani mara nyingi husemwa vibaya. Maoni ya wadau baada ya mechi pia yana mchango wa kuamua ubora wa mwamuzi na ndio bodi za waamuzi chini ya CAF huchagua waamuzi, bodi haiwezi kupendekeza jina la mwamuzi ambaye anakosolewa kila mechi.”
LUGHA
Lugha ya mawasiliano ni miongoni mwa changamoto inayotajwa na wadau. Inaelezwa kuwa kwenye mashindano ya AFCON ni lugha mbili zinazotawala zaidi, Kiingereza au Kifaransa. “Idadi kubwa ya waamuzi wetu hawana uwezo wa kuzungumza Kifaransa. Mataifa mengi yanayofuzu kule yanatumia lugha ya Kifaransa, japo yapo yanayotumia lugha ya Kiingereza. Hizi lugha ni muhimu, kwahiyo mwamuzi anatakiw akuimudu angalau moja kati ya hizo”
Hata hivyo baadhi wanaona maoni hayo yanafifisha uwezo wa waamuzi, kwamba mwamuzi anakuwa na uwezo wa kutafsiri sheria uwanjani hata kama hatakuwa na uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha na mataifa kama Cameroon, Mali, Morocco au Tunisia ambako lugha zao ni Kifaransa na Kiarabu zaidi. Hata hivyo suala hili la lugha baadhi wanaona si kigezo ingawa lina mchango.
PROGRAMU
“Chama cha waamuzi kinatakiwa kuandaa waamuzi wapya, wangali vijana ambao watakuwa na nafasi ya kujifunza. Watafutwe kila kona ya nchi, wachezeshe mashindano madogo ya watoto au vijana. hii itawajengea uwezo. Programu hii iwe endelevu, maana siku hizi tunaona hata Somalia na Djibout wanakuja juu kwenye suala la waamuzi wa mpira Afrika. Itafutwe siri ya hawa majirani kuwa na waamuzi wazuri siku za karibuni,”